Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Mafuta na Maji (EWURA) sasa imepiga hatua nyingine na kufanikiwa kudhibiti uchakachuaji wa mafuta ya dizeli na petroli, baada ya kuanza kutumia teknolojia ya vinasaba (maker).

Meneja Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo, ameiambia Jamhuri kuwa Mamlaka hiyo kwa sasa imeingiza teknolojia mpya inayodhibiti uchakachuaji kwa kiwango cha juu.

“Teknolojia tunayotumia sasa inaitwa teknolojia ya vinasaba. Mafuta yanapoingia nchini tunayawekea vinasaba. Mfanyabiashara akiyachanganya tu tukiingiza kwenye maabara yetu, inatupa matokeo kama mafuta hayo yalikuwa yanakwenda nje ya nchi yameingia katika soko letu inasema au mafuta ya taa au maji yameongezwa.

“Tena teknolojia hii haibuni. Inakueleza kabisa na mwingizaji wa mafuta yaliyotumika kuchakachua mengine, kwani tunapoweka vinasaba tunakuwa tumeainisha ni yapi ya kutumika ndani, ni yapi yanapita tu na yatatumika nje ya nchi. Hii ni komesha,” alisema Kaguo.

Baada ya EWURA kuwa imefanikiwa kudhibiti uchakachuaji uliokuwa ukitumika wa kuingiza mafuta ya taa mengi na kuyachanganya na dizeli, kwa sasa imeibuka mbinu mpya.

Baadhi ya mashirika yanaagiza mafuta na kuonyesha kuwa yanapelekwa nje ya nchi, wakati uhalisia hayavuki mipaka ya nchi.

Hali hii imezaa kupungua kwa kiwango cha mafuta ya taa yanayoingizwa nchini baada ya kodi ya mafuta hayo kupandishwa, lakini kiwango cha mafuta ya taa yanayopitia kwenye bandari ya Dar es Salaam kwenda nje ya nchi kinaonekana kuongezeka.

“Tumekwishakamata wafanyabiashara kadhaa kwa kutumia teknolojia hii na sasa tunawaonya kuwa sheria inaturuhusu kumfungia maisha  mfanyabiashara anayechakachua mafuta. Tumepata kuchukua hatua kama hizi huko Moshi, na hatutasita kufanya hivyo kwa wengine. Wajue kama wao ni wajanja teknolojia imewazidi ujanja,” alisisitiza Kaguo.

Meneja huyo alisema athari kubwa zinazotokana na uuzaji wa mafuta yaliyochakachuliwa ni pamoja na uharibifu wa magari na mitambo, mazingira, kuikosesha serikali kodi na kuanzisha ushindani wa kibiashara usio wa haki kwa wanaoingiza mafuta nchini kihalali.

1137 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!