Mpendwa msomaji, Watanzania sasa tunawindana kama digidigi, tunang’oana meno na tunatoboana macho. Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda, ametekwa na kutendewa unyama huu.

Tukio hili limekuja miezi michache baada ya mwandishi Daudi Mangosi kuuawa na polisi Septemba mwaka jana. Kesi inaendelea. Mwandishi Shaaban Matitu amepigwa risasi na polisi. Mwandishi wa Radio Kwizera Kigoma, Issa Ngumba, ameuawa mwaka huu.

 

Charles Misango, Edson Kamukara na wengine wa Tanzania Daima wamehojiwa. Kuna kasi ya kuzorota kwa uhusiano kati ya vyombo vya dola na wanahabari.


Sitanii, ndani ya mwezi mmoja ameuawa Mchungaji Mathayo Kachila (45) huko Buseresere, Padre Evarist Mushi ameuawa kwa kupigwa risasi, na Imamu wa Msikiti wa Mwakaje Zanzibar, Sheikh Ali Khamis Ali (65), ameuawa kwa kupigwa kisu shambani mwake. Haya ni baada ya Dk. Stephen Ulimboka kufanyiwa kama alivyofanyiwa Kibanda, Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga, kumwagiwa tindikali na matukio mengi ya ukatili. Ninalojiuliza ni je, Taifa letu linakwenda wapi?


Kama Taifa tumelegea. Mabalozi wa nyumba 10 wamepoteza nafasi zao. Wageni, wavuta bangi na dawa za kulevya wanahama mtaa hadi mwingine bila mamlaka kuwa na taarifa yoyote.

 

Sitanii, Serikali irejee mpango wa usalama wa miaka iliyopita. Matukio haya tunayoyaona wala si ishara, ndiko kupotea kwa amani kwenyewe.


Utaratibu huu mpya wa kila mtu kuchukua sheria mkononi umewafikisha pabaya Somalia, Rwanda, DRC na Burundi. Najua polisi mkiamua mnaweza kutenda, hebu liokoeni Taifa hili.


Pili nijadili ushindi wa Rais Mteule, Uhuru Kenyatta. Nimefuatilia kwa karibu kampeni za uchaguzi Kenya. Muda wote Kenyatta amekuwa akiahidi kujenga taifa moja, lenye mshikamano na lenye ajira za kutosha.


Nampongeza Kenyatta kwa ushindi alioupata na hasa kauli hii kuwa analenga kujenga KENYA MOJA.


Nasisitiza Kenya Moja kwa maana kwamba ipo dhambi kubwa iliyomwingiza madarakani Uhuru, sasa itampasa kukabiliana nayo.


Sitanii, dhambi hii si nyingine, bali ni ukabila. Kenya ni taifa lenye kila nafasi ya kuendelea. Wakoloni walijenga miundombinu ya kila aina kwa taifa hili tofauti na Tanganyika. Wamejengewa viwanda msingi, lakini ukabila umewakwamisha.


Binti mmoja Jumamosi asubuhi aliiambia televisheni ya Citizen: “Nimefurahi sisi Wakikuyu na Wakalenjini tumeshinda.” Uhuru Kenyatta ni Mkikuyu na makamu wake, William Ruto, ni Mkalenjini. Unaweza kupima ukubwa wa tatizo. Wenye kujua wanasema zimepigwa kura za ukabila.


Kenya imekuwa na marais wanne sasa. Jomo Kenyatta (Mkikuyu), Daniel arap Moi (Mkalenjini), Mwai Kibaki (Mkikuyu) na Uhuru Kenyatta (Mkikuyu).


Kwa mantiki hiyo basi, nasema Uhuru anayo kazi ya kupambana na ukabila nchini Kenya. Wapo wanaosema kilichoshinda si Muungano wa Jubilee dhidi ya wa CORD, bali ni ushindi dhidi ya Waluo (Raila Odinga) na makabila mengine madogo madogo.


Sitanii, Kenyatta na Ruto wanashitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya ICC kutokana na uhalifu dhidi ya binadamu uliotokana na vurugu za uchaguzi wa mwaka 2007. Ni wazi utaibuka mgogoro wa kidiplomasia.


Uhuru na Ruto ikiwa hawatakwenda au watakwenda mahakamani wakatiwa hatiani, kimataifa ni mgogoro mkubwa. Kuna hatari ya Kenya kuwa kama ilivyokuwa Sudan chini ya Rais Omar el Bashir. Baadhi ya mataifa hawatapakanyaga.


Kwa Afrika, Muungano wa Afrika (AU) umeweka msimamo wa kutoruhusu Rais aliyepo madarakani kwenda The Hague kushitakiwa ICC. Kwa mantiki hiyo, Uhuru atakuwa na fursa ya kutembelea nchi zote za Afrika kasoro Malawi, ambako Joyce Banda anasema yeye atamkamata yeyote anayetakiwa ICC.


Sitanii, wakati mgogoro huo wa kidiplomasia ukiendelea, hii ni nafasi kwetu Watanzania. Tanzania ijiandae kuwa mlango wa kuingilia Afrika Mashariki.

Yote kwa yote, nasisitiza mambo mawili. Ukabila udhibitiwe Kenya na waandishi nchini wasisulubiwe.


990 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!