Ee Mungu, tuepushie mauaji, mateso haya
Ee Mwenyezi Mungu, muumba wa mbingu na ardhi, na vitu vyote vilivyomo, tuepushie janga hili la mauaji na mateso ya kikatili dhidi ya Watanzania.
Mungu wetu mwenye rehema, tuepushie wimbi hili la kiibilisi maana katika siku za karibuni, baadhi ya wananchi wakiwamo viongozi wa dini na waandishi wa habari, wameuawa na kuteswa kikatili nchini, huku watekelezaji wengi wa uovu huo wakiishia kutokamatwa na vyombo vya dola.
Tazama ee Mungu, mwaka 2011, mwandishi wa habari aliyekuwa mhariri wa Gazeti la Kasi Mpya, Richard Masatu, aliumizwa hadi kupoteza maisha katika mazingira tatanishi jijini Mwanza.
Ee mola, mwaka jana (2012) pia, Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, alitekwa, akateswa na kuumizwa nusura aage dunia, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Lakini pia ee Mungu, mwaka huo huo, mwandishi wa habari aliyekuwa mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, aliuawa kwa kulipuliwa na silaha ya moto akiwa ametiwa nguvuni na askari polisi mkoani Iringa.
Pia mwanzoni mwa mwaka huu, ee Mungu wetu, mwili wa mwandishi wa habari, Issa Ngumba, uliokotwa porini baada ya kuuawa kikatili na watu wasiojulikana mkoani Kigoma.
Baadaye tena mwaka huu huu, Mchungaji Mathayo Kachila wa Kanisa la Pentecost Assembles of God, aliuawa kinyama katika vurugu baina ya waumini wa Kiislamu na Kikristo mkoani Geita. Kifo hicho sasa kinazorotesha shughuli za kiroho katika eneo hilo.
Kama hiyo haitoshi ee Mungu mweza wa yote, Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana huko Zanzibar. Ameacha pengo katika kanisa hilo. Ee Muumba wetu, bado mwaka huu huu, huko huko Zanzibar, Sheikh Ali Khamis Ali ameripotiwa kuuawa kwa kushambuliwa na vitu vyenye ncha kali. Hili ni pigo kwa Waislamu na Watanzania kwa jumla.
Wili iliyopita, ee Mwenyezi Mungu, Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006), Absalom Kibanda, amevamiwa na kushambuliwa vibaya nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.
Ee Mungu wetu uliye mbinguni, Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ni miongoni mwa waandishi wa habari wanaotegemewa na jamii ya Watanzania katika kutafuta maendeleo ya kweli nchini.
Ee Mwenyezi Mungu, mlolongo nilioutaja hapo juu ni sehemu ndogo ya matukio mengi ya kikatili yaliyowakumba baadhi ya Watanzania. Watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) na vikongwe nao wamekuwa wakiuawa bila huruma nchini. Hali hii inatisha!
Ee Muweza wa yote, tuepushie mauaji na mateso haya. Wataalamu, viongozi wetu na watu wanyonge wanapukutika Tanzania! Tuonee huruma sisi wanao.
Inawezekana ee Muumba wetu, matukio hayo si ya bahati mbaya bali yamepangwa na watu wachache wenye sababu zao za kishetani. Wajaalie rehema waweze kutambue kuwa wanatenda kinyume cha mapenzi yako.
Ee Mungu wetu mwema, pia wajaalie viongozi wa Serikali waimarishe mipango-mikakati ya kukabili matukio ya aina hiyo kuwaondolea wananchi hofu ya kuvamiwa, kuteswa na kuuawa kikatili ndani ya nchi yao huru.
Kwa upande mwingine, ee Mungu, wajaalie viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini uwezo wa kutosha, kuhimiza waumini kuhakikisha wanajiepusha na vishawishi vya kujiingiza katika vurugu za kidini nchini.
Ninaamini kwamba wewe Mungu wetu, una uwezo wa kuingilia kati na kuwashinda watu wote wanaotekeleza mwongozo wa shetani kwa kuwatisha, kuwateka, kuwatesa na kuwaua kinyama wanao hapa Tanzania.
Ee Mola wetu, wengi tunapenda kuona tunaishi katika Tanzania salama, kuenenda katika mapenzi yako na kuepuka kila aina ya dhambi. Tuwezeshe katika hilo.
Basi kwa haya machache, ee Mwenyezi Mungu wetu mwenye rehema na upendo, uliona vema kutuleta duniani tuishi salama na kukutumikia wewe, onesha muujiza wako kwa kutuepushia matukio ya mauaji na mateso yasiyo mapenzi yako. Amina.