*Jaji Warioba, Mbunge walumbana ukumbini

Wabunge kadhaa wameikosoa Katiba ya sasa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wametoa mapendekezo mazito wakipendekeza yaingizwe kwenye Katiba mpya.

Wamependekeza mafisadi, wala rushwa na wahujumu uchumi wauawe kwa risasi, au kwa kunyongwa, ikiwa ni njia ya kukomesha maovu hayo na kuhamasisha matumizi sahihi ya rasilimali za umma.

 

Pia wamepinga mamlaka makubwa ya Rais, umri wa kugombea urais, nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya, wabunge wa viti maalumu, utaratibu wa kuwapata mawaziri, mfumo wa Muungano na Serikali kwa jumla. Walitoa mapendekezo hayo mbele ya Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya, chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, katika ukumbi wa Msekwa, mjini Dodoma, mwishoni mwa wiki.


Awali, Jaji Warioba aliwaomba watoe maoni yanayojikita katika misingi ya Taifa ikiwamo ya uhuru, haki, umoja, amani, uzalendo, maadili, Muungano, muundo wa Serikali na wajibu wake kwa wananchi.

 

Kuhusu adhabu kwa mafisadi, wala rushwa na wahujumu uchumi, Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alitaka Katiba mpya iidhinishe adhabu ya kuwaua kwa kuwanyonga.


“Katiba mpya itamke hadharani adhabu ya kumnyonga mhujumu uchumi. Hakuna sababu ya kusema tunalinda haki za binadamu kwa mhujumu uchumi.


“Wananchi wengi wanakosa matibabu vijijini na kufa kwa sababu ya ubinafsi na masilahi ya mtu mmoja,” alisema Machali.

 

Mapendekezo hayo yaliungwa mkono na wabunge wengi, wakiwamo Nyambari Nyangwine wa Tarime (CCM) na Mbunge wa Mkanyageni, Said Suleiman Said (CUF), aliyetaka wala rushwa wauawe kwa kupigwa risasi. Hata hivyo, Mbunge wa Viti Maalumu na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Stella Manyanya (CCM), alitaka Katiba ijayo ifute adhabu ya kifo, badala yake wahalifu wahukumiwe kifungo cha maisha na kazi ngumu gerezani.

 

“Adhabu ya kifo mara nyingi haitekelezwi nchini, hivyo iondolewe, badala yake mtu ahukumiwe kifungo cha maisha na kazi ngumu,” alisema Manyanya.

 

Kwa upande mwingine, wabunge wengi walitaka Katiba mpya impunguzie rais madaraka ili kuviwezesha vyombo mbalimbali vya uamuzi kama Mahakama, Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kufanya kazi kwa uhuru unaokidhi matakwa ya umma.

 

Mbunge wa Tumbe, Rashid Ali Abdallah (CUF), alitaka Katiba mpya imwondolee rais madaraka ya kuwasamehe watu waliohukumiwa kifungo gerezani.

 

Baadhi ya wabunge waliopendekeza Rais apunguziwe madaraka ni Machali, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema-Iringa Mjini), Zitto Kabwe (Chadema-Kigoma Mashariki), Ezekiel Wenje (-Chadema-Nyamagana), Dk. Hamis Kigwangalla (CCM-Nzega), Cecilia Paresso (Viti Maalumu-Chadema) na Mohamed Juma Mnyaa (CUF-Mkanyageni).

 

Pamoja na mambo mengine, walitaka Katiba itakayoundwa imwondolee rais madaraka ya kuteua majaji na viongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, badala yake wachaguliwe na wananchi.

 

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba, Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhani aliyefuatana na Jaji Warioba, alitaka kujua iwapo wabunge wanamaanisha kuwa majaji na viongozi wa tume hiyo nao wawe wanafanya kampeni za kuomba kuchaguliwa na wananchi kama ilivyo kwa wanasiasa.

 

Mbunge Paresso alifafanua kuwa utaratibu mzuri unaopaswa kutamkwa kwenye Katiba mpya, ni kutangaza majina ya wanaoomba ujaji na kuyapeleka kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.

 

Kuhusu umri wa kugombea urais, wabunge Ali Kessy (CCM-Nkasi), Nyambari Nyangwine (CCM-Tarime), Zito Kabwe (Chadema-Kigoma Kaskazini, Dk. Kigwangalla (CCM-Nzega), ni miongoni mwa waliopendekeza umri uwe kati ya miaka 35 na 55 badala ya miaka 40 na kuendelea, kwa mujibu wa Katiba ya sasa.


“Umri wa kugombea urais uwe kati ya miaka 35 na 55. Bunge letu lisijae wastaafu kwa sababu wao wana kiinua mgongo, waachie vijana, haiwezekani Bunge lijae wastaafu wanaokuja kusikilizia tu,” alisema Kessy na kuwavutia wengi kwa jinsi alivyozungumza kwa kujiamini.


“Ninaunga mkono umri wa kugombea urais uanzie miaka 35, lakini usiwe na kikomo, uendelee hata mpaka miaka 80 ilimradi mtu ana uwezo wa kuongoza,” alisema Nyangwine, aliyetafsiriwa kuwa alikuwa akimpigia debe Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Stephen Wasira, ambaye ni mmoja wa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wenye umri mkubwa wanaotajwa kutaka kuwania urais mwaka 2015.

 

Naye, Kabwe alisema, “Hakuna sababu ya ku-limit umri wa kugombea urais, ninapendekeza mwenye haki ya kupiga kura awe na haki ya kugombea urais.”

 

Kuhusu nafasi za wakuu wa mikoa na wilaya, wabunge wengi walisema hawaoni haja ya kuendelea kuwapo, hivyo wakapendekeza Katiba mpya iruhusu mameya na wakurugezi watendaji wachaguliwe na wananchi.

 

Kuhusu nafasi za wabunge wa Viti Maalumu, wabunge wengi hasa wanaume, walipendekeza Katiba ijayo isizitambue, badala yake wanawake wagombee na kushindanishwa kwa ajili ya kuchaguliwa kama ilivyo kwa wanaume.

 

“Viti Maalumu vifutwe, wanawake washindanishwe kwa ajili ya kuchaguliwa kutokana na uwezo wao kwani wengi wao wanaweza,” alisisitiza Mchungaji Msigwa.

 

Kuhusu uteuzi wa mawaziri, wabunge wengi walipendekeza Katiba itakayoundwa iruhusu wateuliwe kutoka nje ya Bunge, ili kuwafanya wawajibike kwa umakini na bila kupendelea majimbo yao na chama chochote cha siasa.

 

Suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar lilitolewa maoni na karibu wabunge wote, ambako wengi walitaka uendelee chini ya Serikali tatu (Tanganyika, Zanzibar na Muungano) na wachache wakitaka mfumo wa sasa wa serikali mbili (Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar) uendelee. Jaji Warioba na Mbunge Mussa Kombo walichangamsha mkutano pale walipolumbana kwa muda, wakati mbunge huyo akitoa maoni kwamba Muungano uliopo uvunjwe na uundwe wa mkataba. Malumbano yao yalikuwa kama ifuatavyo:

 

Jaji Warioba: Unakula muda, umeshatumia dakika tatu.

Kombo: Mheshimiwa Mwenyekiti, hata dakika moja, nipe muda wangu au unataka niondoke?

Jaji Warioba: Ukiondoka shauri yako, usinitishe.

Kombo: Sasa wewe ‘chairman’ isije ukawa karaha kuliko mimi ninayetoa maoni. (kisha akaondoka ghafla kutoka eneo la mbele kurudi katika kiti chake).

 

Kwa upande mwingine, Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), alipendekeza Katiba mpya iitake Serikali kuwa na utaratibu mzuri wa kujenga uzalendo, nidhamu ya uongozi na utendaji kuanzia kwa watoto hadi kwa wakubwa.

 

Kuhusu udini, Mchungaji Msigwa alitaka suala hilo lifafanuliwe vizuri kwenye Katiba mpya, kuwezesha wananchi kuwa huru kuabudu dini zao katika Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Anne Makinda (CCM-Njombe Kusini), aliwahimiza wabunge kuendelea kujitokeza kwa wingi kutoa maoni ya Katiba mpya kwa kuzingatia kwamba Katiba ndiyo uhai wa nchi.

 

Akiahirisha kipindi hicho cha kupokea maoni ya wabunge kilichodumu kwa saa nne na robo, Jaji Warioba alisema Tume inakaribia kukamilisha hatua ya kwanza ya kukusanya maoni ya mtu mmoja mmoja kabla ya kuanza hatua ya pili ya kukusanya maoni ya makundi mbalimbali, vikiwamo vyama vya siasa na madhehebu.


1410 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!