Jeshi la Polisi mkoani Mwanza ‘limebinafsisha’ baadhi ya shughuli zake kwa taasisi binafsi kwa madai ya kukosa vitendea kazi sahihi.





Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro (kulia) akiwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI na kuthibitishwa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, Sophia Jongo, umebaini kuwa kazi ya kutoa stakabadhi inayothibitisha upotevu wa vitu (loss report) hivi sasa inafanywa na taasisi binafsi kwa niaba ya Jeshi la Polisi mkoani humo.

Kama hilo halitoshi, wananchi wanaohitaji huduma hiyo hutozwa Sh 5,500 ikiwa ni asilimia 1,100 zaidi ya kiwango cha Sh 500 ambacho hutakiwa kutozwa kwa huduma hiyo.

Katika kiwango kinachotozwa na watu binafsi kutoa huduma hiyo, ni Sh 500 tu huingia katika mfuko wa serikali huku Sh 5,000 zikichukuliwa na wafanyabiashara hao wanaofanya kazi hiyo ya kutoa ‘loss report’ kwa niaba ya Jeshi la Polisi.

Hatua ya Jeshi ka Polisi mkoani Mwanza kutoa ruhusa kwa watu binafsi kufanya kazi ambazo zinapaswa kufaywa na jeshi hilo inakwenda kinyume cha agizo lililotolewa na Rais Dk. John Magufuli takriban miaka mitatu iliyopita.

Katika agizo hilo, Rais Dk. Magufuli alipiga marufuku shughuli zozote za kijeshi kufanywa na raia kama sehemu ya mkakati wa kulinda na kutunza siri za jeshi hilo.

Mwandishi wa habari wa JAMHURI ni mmoja wa watu waliopatiwa huduma hiyo ya kupewa ‘loss report’ ya Jeshi la Polisi kupitia stationery iliyopo karibu na Kituo cha Polisi cha Nyakato, jijini Mwanza.

Stationery hiyo ya mtu binafsi iliyoandikwa mlangoni BD, inafanya kazi ya kutoa ‘loss report’ kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo.

Mtu anayehitaji huduma hiyo anapofika dukani hapo kwanza huulizwa iwapo anafahamu gharama za huduma hiyo, kisha huelezwa utaratibu, ikiwamo kutakiwa kulipa Sh 5,500 kwa ajili ya huduma hiyo.

Pamoja na kiwango hicho cha juu ambacho duka hilo hutoza kwa ajili ya huduma hiyo, lakini hakuna risiti mahususi inayotolewa kuonyesha malipo hayo.

Aidha, duka hilo halina hata risiti za EFDs ambazo wafanyabiashara wanapaswa kuwa nazo.

Kwa mujibu wa maelekezo ambayo mwandishi alipewa na wahudumu wa stationery hiyo, yapo maduka kadhaa kama hayo ya watu binafsi ambayo hutoa ‘loss report’ kwa wananchi wanaohitaji.

Mwenye duka

Akizungumza na JAMHURI kwa njia ya simu, baada ya mwandishi kulipa Sh 5,500 na kupewa ‘loss report’ yenye nembo ya Jeshi la Polisi na saini ya Mkuu wa Jeshi hilo (IGP), mmiliki wa stationery hiyo ambaye alikataa kutaja jina lake, amekiri kuwa duka lake huwa linatoa huduma hiyo kwa gharama ya Sh 5,500.

“Hii ni biashara yangu. Sh 5,500 uliyotozwa siyo yote inakwenda Jeshi la Polisi. Polisi yao ni Sh 500 tu, nyingine ni yangu, maana mimi ndiye ninatoa huduma,” mmiliki wa duka hilo ameliambia JAMHURI.

Mwandishi alipomtaka ampatie risiti halali ya malipo ya Sh 5,500 kwa ajili ya huduma ya kupatiwa ‘loss report’, mmiliki huyo wa duka aling’aka: “Sina risiti kwa sababu ofisi hii ni mpya.”

Hata hivyo, mwandishi aliweka mkazo wa kupatiwa risiti kwa sababu ni haki yake baada ya kufanya malipo, mmiliki huyo aliagiza risiti iliyoandikwa kwa kalamu kutoka duka jingine liitwalo, S&A Stationery ambayo inaonyesha kuwa linamilikiwa na Salma L. Ndende.

Risiti hiyo imeandikwa ‘IPC rosriport’ 5,000, ikifuatiwa na neno II ‘Contror’ number 500.

Kwa mujibu wa uchunguzi, punde mwananchi anapolipa Sh 5,500 hupewa risiti ya benki inayoonyesha malipo yamepokewa kwenda Polisi Tanzania kiasi cha Sh 500.

Wakizungumzia hali hiyo, baadhi ya wakazi wa jijini Mwanza wamemuomba Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, kutoka hadharani kueleza kwa nini huduma hiyo ya kijeshi inatolewa na watu binafsi.

“Hata Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, atueleze inakuwaje huduma ya ‘loss report’ katika Mkoa wa Mwanza zinatolewa na wafanyabiashara binafsi? Yaani siri za kijeshi anapewa raia tu wa kawaida, akae nazo, ahudumie wananchi, tena kwa gharama za juu za Sh 5,500… halafu Polisi wanapewa Sh 500 tu. Hii inaingia akilini kweli?” anahoji mmoja wa wakazi wa Jiji la Mwanza aliyedai kukumbana na kadhia hiyo.

Polisi wakiri

Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, limekiri huduma hiyo ya kutoa ‘loss report’ kutolewa na wafanyabiashara binafsi kwa niaba ya jeshi hilo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Sophia Jongo, anasema jeshi hilo limewapa kazi hiyo wafanyabiashara binafsi kutokana na wao kutokuwa na kompyuta za kutolea huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Kamanda Jongo, malipo halali ambayo huchukuliwa na jeshi hilo kwa ajili ya huduma ya kutoa ‘loss report’ ni Sh 500 tu na Sh 5,000 huchukuliwa na wafanyabiashara hao.

Hata hivyo, Kamanda Jongo alionyesha kusikitishwa na kiasi hicho kikubwa cha fedha ambacho wafanyabiashara hao huchukua kupitia huduma hiyo.

“Zamani malipo yote yalikuwa yanalipwa kwa Mhasibu wa Jeshi la Polisi. Lakini serikali ilibadili utaratibu na kuanza kupokea malipo kwa njia ya kielektroniki. Sasa sisi Polisi hatuna kompyuta za kutoa huduma za malipo ya aina hiyo,” anasema na kuongeza:

“Kwa hiyo, wafanyabiashara walichangamkia tukakubaliana wawe wanatoa ‘loss report’ kwenye stationery zao binafsi. Malipo ya Polisi kwa ajili ya huduma hiyo ni Sh 500 tu siyo zaidi ya hapo. Hiyo Sh 5,000 ni biashara yao, hatuwezi kuwapangia.”

Hata hivyo, Kamanda Jongo anasema IGP Sirro analishughulikia suala hilo ili kuliwezesha Jeshi la Polisi kutoa huduma hiyo badala ya kuwaachia wafanyabiashara binafsi.

Aidha, amewataka wafanyabiashara wanaotoa huduma hiyo kuwaelewesha wananchi kuwa gharama halisi za kupata ‘loss report’ ni Sh 500 tu na si Sh 5,500.

“Alipaswa awaeleweshe kwanza. Anaposema gharama ya ‘loss report’ ni Sh 5,500 anakosea. Maana gharama halisi ya Polisi ni Sh 500 tu. Hiyo nyingine ni yake na wananchi waeleweshwe hivyo. Pia, hakupaswa kukupa risiti bandia kutoka stationery nyingine, tena risiti ya karatasi. Ina maana yeye ataingiaje kwenye rekodi ya TRA kwamba amelipa mapato kwa kutumia hiyo risiti ya ofisi nyingine?” anahoji Kamanda Jongo wakati akitoa ufafanuzi kwa gazeti hili.

Watiwa mbaroni

Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi mkoani hapa limewatia mbaroni watu saba kwa tuhuma za kujifanya maofisa wa Usalama wa Taifa kutoka Ikulu.

Watu hao wanasadikiwa kuwatapeli wananchi na baadhi ya watumishi wa serikali katika Jiji la Mwanza, kwa kujifanya wapo kwenye kazi maalumu, kisha kuwajengea hofu ya kiutendaji na kutengeneza mazingira ya rushwa.

Akizungumza hivi karibuni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Murilo, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Chalanga William Chalanga (45), mkazi wa Pasiansi, Mwanza na Arusha.

Kwa mujibu wa RPC Murilo, watuhumiwa wengine ni Hamis Seleman Mwalimu (25), fundi magari na hujifanya mlinzi (bodyguard) wa Chalanga William Chalanga.

Wengine ni Philipo Petro (35), mkazi wa Usagara wilayani Misungwi, pia ni dereva wa Chalanga William Chalanga, Elia Vincent Gunda (30), anayedai kuwa yeye ni Mchungaji wa Kanisa la EAGT lililopo Kisesa, Wilaya ya Magu.

“Hassan Mohamed Juma, miaka 29, mkazi wa Mkolani, fundi wa IT, Selemani Joramu Karanga, miaka 25, anajifanya mlinzi wa Chalanga William Chalanga, anayejifanya ni Afisa Mkuu wa Ikulu, na Michael Richard mkazi wa Morogoro,” Kamanda Murilo anasema.

RPC Murilo ameueleza umma kuwa suala hilo haliwezi kukubalika na kupewa nafasi katika jamii inayofuata mfumo wa utawala wa sheria.

Kwa mujibu wa Kamanda Murilo, matukio hayo yametokea kati ya Disemba 27, 2019 na Januari 2, 2020 katika maeneo ya Nyakato, Wilaya ya Nyamagana, ambako washitakiwa walikutwa wakitumia gari la kubebea wagonjwa lenye namba za usajili T 751 BNL aina ya Toyota.

“Walikamatwa na makachero na wakaendelea kujitambulisha kuwa wao ni maofisa Usalama wa Taifa  kutoka Ikulu. Lakini walipohojiwa kwa kina ilibainika ni matapeli wenye lengo la kuwababaisha watu kwa malengo binafsi,” RPC Murilo anasema.

By Jamhuri