BiasharaMwishoni mwa Februari mwaka huu nilikuwa nikisafiri kutoka Wilaya ya Mvomero kuelekea Kilombero mkoani Morogoro. Nilipofika Morogoro mjini niliingia kwenye basi moja ambalo linafanya safari zake kati ya Morogoro mjini na Ifakara.
 Muda niliokata tiketi katika basi hilo ilikuwa ni saa tisa na nusu jioni, lakini ndani ya hilo basi nilikutana na abiria ambao walikata tiketi majira ya saa tatu asubuhi! Kila abiria aliyekuwa anakata tiketi pale alikuwa akidanganywa muda wa kuondoka kwa basi husika.    Wale waliokata tiketi saa tatu asubuhi waliambiwa basi lingeondoka saa nne na mimi wakati ninakata tiketi saa tisa na nusu niliambiwa kuwa basi linaondoka saa kumi kamili!


Kilomita mbili baada ya kuondoka stendi kuu ya Morogoro saa kumi na moja jioni; kondakta akatutangazia abiria ya kwamba basi hilo halitaendelea na safari ya Ifakara kwa sababu idadi ya abiria ni wachache. Kondakta akadai kuwa kutokana na uchache wa abiria tuliomo haitawalipa kulipeleka basi huko.
Walichofanya wakakodi basi dogo na kuamuru abiria tuingie humo. Kwa bahati mbaya sana idadi ya abiria tuliokuwamo kwenye basi la awali tulikuwa ni wengi kushinda idadi ya siti za hili basi dogo. Abiria wengi waliokosa siti wakalazimika kusimama wakati tiketi zao zilikuwa zinaonesha nambari ya siti kwa basi la awali.


Abiria tusio na makuu ndiyo tulioingia kwenye basi lile dogo lakini kuna ambao waliwasha moto kuhusu uhuni wa basi lile na wakakataa katakata kubadilishiwa gari eti kwa sababu ya kusema hailipi. Nilimsikia abiria mmoja akisema maneno yafuatayo kwa hasira na ukali mwingi.
Kama ingekuwa basi limeharibika ningekubali, lakini mnaleta uhuni wa kusema eti haitawalipa, kwani mnavyoomba leseni Sumatra si mlijua kuna siku mtapata abiria na siku nyingine mtakosa?


Imeandikwa wapi katika leseni ya kuwa abiria wakiwa wachache katika basi, safari iahirishwe? Nitakufa na ninyi ili niwafundishe adabu muache kutuonea. Mnadhani Watanzania wa siku hizi ndiyo wale wa zamani wa kuwapelekesha kama maboga?
 Baada ya kuona pamekuwa pa moto, wafanyakazi wa lile basi kubwa ilibidi wawavute pembeni wale abiria waliowasha moto na kuzungumza nao. Sielewi walifikia mwafaka gani lakini abiria wale walishikilia msimamo wa kutoingia kwenye basi lile dogo. Tuliondoka Morogoro saa moja kasoro jioni huku abiria wote wakiwa wanalalamika, kujiapiza na kupiga kelele.


 Katika siti niliyokaa ndani ya lile basi dogo kulikuwa na mama mmoja ambaye baada ya kumsalimia alinieleza kuwa anaona sura yangu kama siyo ngeni. Nilipomueleza kuwa huenda aliniona kwenye gazeti la JAMHURI, alishtuka mno na kusema, “Hee, kumbe wewe ndiyo Sanga? Wawoo! Kila wiki nazisoma makala zako.”


Kisha akauliza kwa hisia kali, “Kwa nini hujawapigia kelele hawa wahuni (wenye basi) wakati wewe ni mwandishi? Hivi unajua ungejitambulisha kwao na kuwapiga mkwara, wangeogopa sana na wasingefanya uhuni waliotufanyia?”
Yule mama niliendelea kuongea naye njia nzima, lakini kwa swali lake la hisia nilimjibu hivi; Wakati abiria wote mlikuwa mkipiga kelele na kulilaani hili basi, mimi fikra zangu zilikuwa kwa mmiliki wa hili basi. Huko aliko nina uhakika hafahamu kuwa vijana wake wanamharibia biashara.
Katika masuala kama haya huwa ninafunga kinywa changu na kusali nikimuombea mjasiriamali mwenye biashara husika.


 Kwa sababu ninafahamu kama mwenye basi hili angekuwapo hapa; asingetumia lugha ya kibabe, asingeonesha ukaidi na asingekubali kuona jina la basi lake linachafuliwa. Nikaendelea kumueleza, kuwa siwezi kutumia uwezo wangu wa kuandika kwa ajili ya kuchafua biashara ama kampuni ya mwingine hata kama wawe wamekosea kiasi gani.


Ninaamini kuwa kuwalinda wajasiriamali wenzangu ni kuandika mema yao ama kukaa kimya kwa makosa yao. Msimamo wa kukaa kimya inapotokea uvurundaji kama wa lile basi lililotushusha unaweza kuonekana ni kutokuwajibika; lakini sifichi mamangu, kabla sijaandika chochote kuhusu biashara ama kampuni yoyote; huwa kwanza najiuliza hivi:  


 Je, hiki ninachoandika kama ningekuwa ni mimi, biashara yangu ama kampuni yangu inaandikwa hivi, ningejisikiaje? Majibu ya swali hili ndiyo hutengeneza makala zangu zote za biashara na uchumi unazozisoma.   Nafahamu kuwa viatu vya ujasiriamali ni vizito; mtu anaweza kukurupuka kukusema vibaya pasipo kufahamu ikiwa wewe unahusika moja kwa moja ama laa. Nipo makini sana na kalamu yangu.
  Mimi nilishuka Kilombero na yule mama aliendelea na safari yake ya Ifakara, lakini safari ile ilinipa kutafakari na kuwahurumia wajasiriamali wengi. Nikaikumbuka kampuni nyingine ya mabasi ambayo siku hizi siioni tena. Wafanyakazi wa kampuni ile enzi zile ikiwa kileleni iking’aa walikuwa na nyodo kupindukia.
  Siku moja nilikuwa na ndugu yangu mmoja mfanyabiashara aliyepo Tunduma na tukafika katika ofisi zao kukata tiketi za kwenda Dar es Salaam. Mkatisha tiketi akatuambia kuwa tiketi zimeisha.
 Siku za baadaye niliambiwa kuwa wafanyakazi wa mabasi yale walikuwa na mtindo wa kumtazama mtu mavazi na mwonekano wake kabla ya kumpa tiketi. Ukivaa rafu rafu hupewi tiketi! Kitendo hiki kilisababisha watu wengi kuhisi wanadharauliwa na hivyo wakaanza kusambaza maneno mabaya kuhusu mabasi yale.


 Kilichotokea! Kuna wakati basi la watu sabini lilikuwa likiondoka stendi likiwa na abiria saba tu! Katika mazingira kama haya ambayo unaendesha kampuni ama biashara kwa hasara haiwezekani ukastahimili katika soko.
Kwenye ujasiriamali wafanyakazi ni pasua kichwa kweli kweli. Uzembe, ujinga na upumbavu wa wafanyakazi wengi umesababisha wajasiriamali wengi kutoendelea, kuyumba ama kufilisika kabisa.
 Unaweza kutafuta mtaji kwa jasho jingi na ukaanzisha duka, unamuweka mfanyakazi auze hapo lakini wengi hawawi waaminifu. Kama ni duka anaweza kuanza kufuja mali ama kuiba. Shemeji zangu Wahehe huwa wana msemo huu; ‘Mtu anakuja kuomba kazi akiwa ananyenyekea na kuweka mikono nyuma, lakini akishapata anaanza kuiweka mikono mbele na anaweza kukufokea hata wewe bosi wake!’


 Kwa hawa wafanyakazi wazembe jambo  baya kuliko yote ni pale inapotokea hawaheshimu, kuwathamini wala kuwajali wateja. Wafanyakazi vimeo huwa hawana uchungu na biashara yako, iwe unauza ama huuzi, iwe unapata hasara ama faida, hawajali! Wanachojali wao ni mshahara wao unaowalipa, basi!
 Usiombe biashara yako ikaingia kwenye tanuri la kusemwa vibya, utajuta. Mathalani, lile basi liliotufanyia uhuni pale Morogoro kila abiria alikuwa akijiapiza kuwa hatakaa apande tena lile basi na wengine wakaweka nadhiri ya kuwajulisha ndugu, marafiki na jamaa zao kuhusu hatari ya basi lile kwamba halifai kupandwa.   Unategemea nini kwa majaaliwa ya kampuni ile kama si kushuhudia kupungua kwa abiria wanaopanda mabasi yao?


  Kama hili tumeshalifahamu ya kuwa wajasiriamali tuna hatari ya wafanyakazi wazembe kutufilisi, je, tufanyaje? Kulalamika haitatusaidia! Kusema tumuachie Mungu ni uzembe! Kuendelea kuvumilia ni kujirudisha nyuma! Tupende ama tusipende wajasiriamali tunalazimika kuchukua hatua za makusudi za kutuwezesha kuwa na wafanyakazi bora watakaojenga biashara pamoja nasi na si wale wanaobomoa.


  Nilichogundua ni kuwa wajasiriamali wengi hatujui namna ya kuajiri pamoja na namna ya kuwafundisha wafanyakazi. Wengi wetu huwa tunazoazoa bora wafanyakazi. Na kinachotuponza ni kupenda vya dezo. Tunapenda kuwabeba ndugu zetu wa karibu bila kujali ubora wao, ilimradi tu tuwe tunawalipa kidogo ama kutowalipa kabisa.


 Fikiria wewe unamiliki basi ama duka halafu unamuweka ndugu yako asiye na uwezo wala vigezo vya kufanya kazi kwa ustadi, unategemea nini? Sana sana ataanza kujitukuza na kujiona yeye ndiye kila kitu katika biashara husika. Hata majigambo yake kwa wengine itakuwa ni cheo chake cha undugu kwako.
 Inabidi ufike wakati ambapo mjasiriamali unapiga hesabu za biashara yako halafu unatafuta wafanyakazi wa kiwango na vigezo kuhimili biashara yako. Hakuna maana ya kusema eti unabana matumizi ya kuwalipa watu mishahara ilhali unaelekea kufilisika.


Nimewahi kueleza namna ya kuwatendea wafanyakazi tunaowaajiri katika makala iliyokuwa na kichwa ‘Mjasiriamali na sayansi ya kuajiri’. Mara zote nimekuwa nikiwatahadharisha wafanyabiashara na wajasiriamali kuepuka mtego wa kuwa wadhulumaji kwa wafanyakazi wao.
Mara zote mfanyakazi unayemuajiri katika biashara zako huwa anafahamu kiwango cha faida unayozalisha. Kitendo cha wewe kumlipa kiduchu kinazalisha sumu mbaya sana. Matokeo yake ni kukuibia, kupoteza morali wa kazi na hatimaye kuwavuruga wateja wako.
Nihitimishe kwa kuwasihi wajasiriamali kuwa makini tunapoajiri watu katika biashara zetu kwa sababu wengine wanaweza kugeuka mawakala wa shetani kutufilisi. Niwatakie kila la heri katika mapambano makali ya kiujasiriamali.

2130 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!