Mbowe+na+Peoples+Power+2Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, anasema; “Rais Jakaya Kikwete na CCM yake wamekwama na atatukabidhi nchi Oktoba.”
 Mbowe, ambaye yuko kwenye ziara ya kuimarisha chama katika mikoa ya Kanda ya Ziwa, anasema kwamba kukwama kwa CCM ni kushindwa kufuata hata ratiba ya kuteua mgombea wa chama hicho.
 “Niseme jambo moja kubwa. Naomba unisikilize kwa makini. Rais Kikwete na chama chake wamekwama. Hawawezi tena. Kwa sababu wanatafakari mgombea atakayechuana na wa Ukawa. Hawamuoni, maana yake nini? Wanajua ni nafasi ya Ukawa kuongoza nchi,” anasema Mbowe.


 Anasema kwamba Chadema kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani wamejipanga kushika dola, “na kwamba kama kuna watu walifikiri Ukawa ni mchezo wa kuigiza, bali ujue wao ndiyo wanaofanya maigizo.”
 Mbali ya Chadema, Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) unaundwa na vyama vya NLD, inayoongozwa na Dk. Emmanuel Makaidi, CUF (Profesa Ibrahim Lipumba) na NCCR-Mageuzi chini ya James Mbatia.
  Vyama hivyo vilitiliana saini ya kushirikiana kwenye uchaguzi kwa kuachiana maeneo ya kuwania ubunge na udiwani kulingana na nguvu ya ushawishi.


  Mbowe anasema kwamba kamwe Ukawa hawatarudi nyuma kwenye mapambano ya kuikomboa nchi hii, iliyoshikwa na CCM na wazazi wake (TANU na ASP) kwa zaidi ya nusu karne.
  Anasema kwamba Watanzania wa sasa huwezi kuwadanganya na ndiyo maana chama hicho kikongwe kwa sasa kinatetereka kumpata hata mgombea wakati imebaki miezi sita kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
  Anasema kwamba Rais Kikwete alianza kukwama mapema kwani hata kwenye mabadiliko ya mawaziri mwaka 2012 alilazimika kuteua makada wengine kuwa wabunge ili awape uwaziri.


 “Alimteua Profesa Sospeter Muhongo kuwa mbunge na akampa uwaziri wa Nishati na Madini, Janet Mbene akawa Naibu Waziri wa Fedha na hata Saada Mkuya ili naye awe Waziri wa Fedha, sasa amekwama kwenye urais,” anasema Mbowe na kuongeza: “CCM hawana mtu wa kupambana na Ukawa. Ikifika Oktoba ushindi ni wa Ukawa na atakabidhi nchi, na tuna matumaini makubwa kupata ushindi.”


Anasema; “Safari hii ngoma nzito, hawa ni watani wa jadi lakini ushindi ni wa kwetu sisi,” anasisitiza Mbowe na kwamba Watanzania wote wenye sifa ya kupiga kura wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.
 “Hata kama kuna wagonjwa, wabebwe kwa machela wakajiandikishe na kuitumia haki yao ya msingi ya kupiga kura kuwachagua viongozi wawatakao,” anasema mwanasiasa huyo Mbunge wa Hai, mkoani Kilimanjaro.


 “Serikali isiruhusu wizi wa kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, ili kuiepusha nchi yetu na matatizo ya kisiasa yanayoweza kujitokeza,” anasema Mbowe wakati anazindua kambi ya vijana katika Kijiji cha Luhemeli, Wilaya ya Nzega mkoani Tabora.
 Hata hivyo, ameitaka Serikali kuendesha Uchaguzi Mkuu kwa uhuru na haki na si kuendeleza vitendo vya kudhulumu haki ya wananchi, ya kuchagua viongozi wawatakao.
 Pamoja na hayo, chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kimeieleza JAMHURI kwamba nguvu pekee iliyosalia kwa CCM ni kutumia mabavu kuchukua madaraka — iwe ni nafasi ya urais, ubunge au udiwani katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Kwa mujibu wa chanzo hicho ambacho kilikataa kuandikwa jina gazetini, maofisa wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakipewa maagizo kutoka kwa viongozi waandamizi wa CCM, kwamba wahakikishe chama hicho cha siasa kinapata ushindi kwa njia yoyote ile hata ikiwezekana kwa nguvu ya dola.


  Imeelezwa kwamba agizo hilo, ambalo limekuwa likitolewa mara kwa mara katika vikao vya maofisa wa jeshi hilo, linaambatana na maonyo makali ikiwa ni pamoja na kushushwa vyeo pale CCM itakapopoteza nafasi yoyote katika uchaguzi.
  “Kwa sasa hali ni ngumu mno kwa CCM kutokana na matukio mengi ya kifisadi yanayoibuka kila kukicha na hivyo kukosa hoja yoyote inayoweza kuwaaminisha wananchi kuwa bado inafaa kuongoza,” kimeeleza chanzo hicho.


  Imeelezwa pia anguko jingine la CCM linatokana na mnyukano mkali wa kisiasa unaowahusu makada wake walioibuka na kujinadi mapema kuwania nafasi ya urais kwa tiketi ya chama hicho. Makada waliojitokeza na kujinadi mapema kinyume na taratibu za chama hicho na kufungiwa kwa mwaka mmoja na Kamati ya Maadili ya CCM, ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, ambaye amekuwa akifuatwa na makundi mbalimbali yanayomshawishi kugombea nafasi hiyo ya urais.


  Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, Naibu Waziri, Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngereja.
  Chadema kwa upande wao kabla ya kujiunga na Ukawa wamekuwa wakikubalika mbele ya CCM kwa sababu ya kuingia kwenye fikra za Watanzania na kwenye sanduku la kura.


  Tangu kuanzishwa kwa Chadema miaka 23 iliyopita na kushiriki chaguzi mbalimbali, chama hicho kimekuwa kikifanya vyema kwenye nafasi hasa za ubunge, udiwani pamoja na viongozi wa vijiji na mitaa.
Chadema haikusimamisha mgombea wa urais mwaka 1995 hali kadhalika mwaka 2000, kwa kile kinachoelezwa kuwa ni demokarsia ya kusapoti vyama vyenye nguvu kwa nyakati hizo.


  Mathalani mwaka 1995, Chadema ilimsapoti Augustino Mrema na 2000 ilimsaidia Profesa Lipumba wa CUF, lakini iliweka wagombea katika nafasi nyingine.
 Rekodi inaonesha kwamba mwaka 1995 Chadema ilipata wabunge wanne wa majimbo na madiwani 42; wakati mwaka 2000 ilivuna wabunge watano na madiwani 75. Katika uchaguzi huo uliofanyika kwa mara ya kwanza uliohusisha vyama vingi baada ya miongo kadhaa, CCM ilionesha jinsi ilivyokuwa imepoteza mvuto.


  Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 29, 1995, mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa, alipata kura 4,026,422 wakati mgombea wa NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema, alipata kura 1,808,616. Mkapa aliyepigiwa kampeni na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wapigakura walikuwa 6,846,681, hivyo, Mkapa alipata asilimia 61.82 wakati Mrema akipata asilimia 27.77.
  Kwa upande wa wabunge, kati ya viti 232 vilivyokuwa vinagombaniwa, CCM ilipata 186 sawa na asilimia 80.17 huku NCCR-Mageuzi ikipata 16 sawa na asilimia 6.9 ya viti vilivyogombaniwa. Mwaka 2000 katika uchaguzi wa pili na wa kwanza bila ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kuwapo, CCM ilifanya vizuri zaidi kuliko miaka mitano nyuma.


  Rais Mkapa akiingia ngwe ya pili alipata asilimia 71.74 ya kura zote za urais (5,863,201), wakati Prof. Lipumba wa CUF akipata asilimia 16.26 ya kura za urais (1,329,077) na Mrema akigombea kwa mara ya pili akipata kura 637,077.
  Wapigakura waliojiandikisha walikuwa 10,088,484 na waliopiga kura wakiwa 8,517,598 sawa na asilimia 84.4. Kwa upande wa Bunge, kwenye uchaguzi huo CCM ilipata viti 202 kati ya viti 231 vilivyogombaniwa wakati CUF ikipata viti 16.
  CCM iliongeza asilimia yake kutoka asilimia 80.17 na kufikia asilimia 87.45. Idadi ya kura za wabunge iliongezeka kutoka asilimia 59.22 miaka mitano iliyopita kufika asilimia 65.19 wakati kwa CUF walipunguza kutoka asilimia 21.83 hadi asilimia 12.54.
  Mwaka 2005, katika uchaguzi ambao CCM ilimteua Jakaya Kikwete kama mgombea wake, alionekana kuwa mshindi mapema kwa sababu alionekana kubeba matumaini makubwa. Wapigakura waliojiandikisha walikuwa 16,401,694 na waliojitokeza kupiga kura walikuwa 11,875,927 sawa na asilimia 72.4. Kikwete alipata kura 9,123,952 sawa na asilimia 80.28.


  Prof. Lipumba wa CUF aliyejaribu bahati hiyo kwa mara ya tatu mfululizo, alipata kura 1,327,125 wakati Freeman Mbowe wa Chadema akipata kura 668,756 sawa na asilimia 5.88.
Kwa upande wa wabunge CCM iliendelea kufanya vizuri zaidi. Kati ya viti 232 vilivyokuwa vinagombaniwa CCM ilipata viti 206 wakati CUF ikipata viti 19 na Chadema vitano. CCM ilipata asilimia 69 ya kura za wabunge wakati CUF ikipata asilimia 14 na Chadema ikipata asilimia 8.20.


  Mwaka 2010 Chadema ilichukua nafasi ya NCCR-Mageuzi na CUF ambavyo vilikuwa ndivyo vikibeba kombe la wapinzani. Ulipofika Uchaguzi Mkuu wa 2010, waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 20,137,303. Hii ilikuwa ni mara 2.3 ya waliojiandikisha kupiga kura mwaka 1995.
  Hata hivyo, idadi ya waliojitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi ule ilikuwa ni 8,626,283 sawa na asilimia 42.8 wakati mwaka 2005 waliojitokeza kupiga kura wakiwa asilimia 72.4 mwaka 2010 ilipungua asilimia 29.6.


  Rais Kikwete alipata kura 5,276,827 sawa na asilimia 62.83 wakati Dk. Willibrod Slaa, mgombea wa Chadema akipata kura 2,271,941 sawa na asilimia 27.05 ya kura za urais huku Prof. Lipumba (akijaribu kwa mara ya 4) akipata asilimia 8.28 ya kura za urais.
  Kutoka kura 9,123,952 alizopata mwaka 2005 hadi kura 5,276,827 ni anguko kubwa kwani alipoteza angalau kura 3,847,125. Hata hivyo, Dk. Slaa, ambaye hakuwahi kugombea urais kabla, alipata kura hizo hapo juu akiinyanyua Chadema kuliko ilivyokuwa kwa Mbowe mwaka 2005.
  Kwa upande wa wabunge kati ya viti 239 vilivyokuwa vinagombewa, CCM ilipata viti 186, CDM ilipata viti 23 wakati CUF ikipata viti 24.


Matokeo ya 2010 yanaakisi kwa namna ya ajabu matokeo ya 1995 wakati mwamko wa upinzani wa vyama vingi uliporudishwa na kushirikishwa kwenye uchaguzi.
  Hali kadhalika, wakati Rais Kikwete akitetea nafasi yake mwaka 2010, Chadema ilivuna jumla ya wabunge 49 wakiwamo 23 wa majimbo na madiwani 467; na katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki ikaongeza kiti kimoja cha Joshua Nassari.
  Mwaka 1995, Mkapa alishinda kwa asilimia 61.82, mwaka 2010 Kikwete alishinda kwa asilimia 62.83 wakati huohuo mwaka 1995 Mrema (Upinzani) alipata asilimia 27.77 mwaka 2010 Dk. Slaa alipata asilimia 27.05.


  Mwaka 1995, mshindi wa tatu, Profesa Lipumba, alipata asilimia 6.43, wakati 2010 mshindi wa tatu (Lipumba) alipata asilimia 8.28 wakati mwaka 1995 kati ya viti 232 vilivyogombewa CCM ilipata 186 mwaka 2010 kati ya viti 239 vilivyogombewa, CCM ilipata viti 186.
Mwaka huo wa 1995, chama kikuu cha upinzani nchini CUF kilipata viti 24, mwaka 2010 chama kikuu cha Upinzani nchini Chadema kilipata viti 23.


  Kadhalika, Mbunge wa zamani wa Musoma, Paul Ndobho, amezungumzia hali ya sasa ya CCM na kusema; “Ni hatari kubwa kwa CCM kwani inazidi kukataliwa ndani ya fikra za Watanzania na zaidi sana imezidi kukataliwa kwenye sanduku la kura.”
  Ndobho anasema kwamba matokeo hayo hususani yale ya uchaguzi wa marudio yanaonesha, licha ya CCM kushinda, bado inazidi kukataliwa na maelfu ya Watanzania, na kwamba kuanzia uchaguzi wa 2010 na chaguzi ndogo zilizofuatia, zinaonesha hadi hivi sasa CCM bado inazidi kukataliwa na hilo ni jambo la hatari.


  “Hata pale ambako inashinda, bado inashinda kwa tofauti ya kura chache ikilinganishwa na huko nyuma. Tatizo ni ufisadi, lakini CCM bado haijapata majibu ya kuzuia kukataliwa kwake,” anasema Ndobho.
  Matokeo ya uchaguzi katika maeneo ya vijiji na vitongoji, CCM ilipata ushindi wa asilimia 79.81 (vijiji) na 79.83 katika vitongoji, wakati kwenye mitaa ambayo ipo sehemu za mijini ilishuka zaidi na kupata asilimia 66.66, ikilinganishwa na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1999, ambako ilipata asilimia 89.2 katika mitaa, asilimia 91 katika vitongoji na asilimia 91.6 katika vijiji.


  Katika uchaguzi wa mwaka jana, CCM ilipata vijiji 7,290 ikifuatiwa na Chadema yenye vijiji 1,248. CUF ilishika nafasi ya tatu kwa kuwa na vijiji 946 ikifuatiwa na UDP yenye vinne na TLP na NLD vyenye viwili kila kimoja.
  Katika nafasi za wenyeviti wa mtaa, CCM imechukua jumla ya mitaa 2,116. Vyama vingine na nafasi zao kwenye mabano ni Chadema (753), CUF (235), ACT (9), NCCR-Mageuzi (8) wakati vyama vya TLP, UMD, UDP na NRA vimepata mtaa mmoja kila kimoja.

By Jamhuri