wpid-Charles-KitwangaWafanyakazi wa Kampuni ya Usangu Logistics wanatarajia kuiburuza kampuni hiyo kortini kutokana na kuchapwa viboko, kufukuzwa kazi kinyume cha sheria na kunyimwa stahiki.

Wanasema mwajiri wao mwenye asili ya Kiarabu, amekuwa akiwachapa bakora na kuwakata mishahara bila sababu za msingi, akiwarejesha kwenye historia ya utawala wa kikoloni, jambo ambalo halina nafasi kwenye Serikali ya kutetea wanyonge ya Rais Dk. John Magufuli.Wameieleza JAMHURI kwamba kesi walizozifungua awali kuhusu kunyanyaswa na kuporwa haki zao ikiwamo mishahara, wanakusudia kuzifungua upya kwa kuwa sasa wana imani kubwa na utawala wa Rais Dk. Magufuli.

Wanasema watendaji wengi katika Serikali zilizopita walikuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa kuwanyima haki, kwa sababu za kuendekeza kile kinachodhaniwa kuwa kurubuniwa kwa rushwa na maslahi binafsi.

Kampuni hiyo pia imedaiwa kujihusisha na ukwepaji wa kodi za Serikali kwa kutumia namba bandia za magari ambazo zimekuwa zikibadilishwa mara kwa mara na kuiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuchunguza na kudai kodi yote iliyokwepwa na kwamba wako tayari kutoa ushahidi.

Wanasema Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Ibrahim Ismail, amekuwa akiwakata Sh 25,000 kila mfanyakazi (Red payment voucher) na haijulikani anakopeleka makato hayo.

“Kwa upande wa mafundi akitoa maelekezo ya kutengeneza gari na tukichelewa kukamilisha kwa muda anaoutaka yeye, anatukata mshahara kila mmoja Sh 200,000 na kwa watu watano anachukua milioni moja au zaidi.

“Mishahara yetu ni midogo, wengine tunalipwa Sh 150,000 hadi Sh 250,000 kwa mwezi ambazo anatudhulumu kwa madai ya kutuadhibu kwa kutokamilisha matengenezo ya magari kwa muda aliotupangia na pia hutuchapa viboko kama wanyama. Tunateswa mno Watanzania na watu hawa,” ameeleza mfanyakazi mmoja.

Wafanyakazi hao wameeleza kuwa wamekuwa wakipeleka malalamiko Kituo cha Polisi cha Buguruni, Dar es Salaam,  Wizara ya Kazi, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa zaidi ya kusikia kuwa baadhi ya maafisa wamekuwa wakipewa fedha na kutochukua hatua zozote na kuwaacha wanaotoa taarifa za manyanyaso wakifukuzwa kazi bila utaratibu.

Wanadai kampuni hiyo inasafirisha mafuta ya petroli na bidhaa mbalimbali nchi za Afrika Mashariki na Kusini, lakini katika hali ya kushangaza wakati wa kupakia mizigo magari hayo hubandikwa namba bandia.

“Ubadilishaji huo wa namba za magari hufanyika wakati wote wa safari ikiwa ni ukwepaji wa kodi za Serikali,” anasema mmoja wa wafanyakazi.

Vyanzo vya habari kutoka TRA vimeeleza kwamba uchunguzi dhidi ya kampuni hiyo kukwepa kodi na kumiliki namba bandia za magari unafanyika, na ikibainika hatua zitachukuliwa mara moja dhidi ya wahusika.

 

Mmoja aeleza alivyofukuzwa bila utaratibu

Saitoti Oyaya anasema kuwa aliyefukuzwa kazi bila utaratibu na Usangu Logistics (T) Ltd. Machi 14, 2014, alifungua shauri Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Kanda ya Dar es Salaam, lililopewa namba CMA/DSM/ILA/239/14/1281 dhidi ya mwajiri wake (Usangu Logistics (T) Ltd) na kushinda.

Saitoti anasema awali shauri hilo halikupata suluhu katika hatua ya usuluhishi, hivyo akaamua kuwasilisha shauri hilo katika hatua ya uamuzi Agosti 13, 2014 akiwakilishwa na mwakilishi binafsi, Zakaria Jorojig, na upande wa mlalamikiwa uliwakilishwa na Tulianus Mtafungwa, Meneja Usalama wa kampuni hiyo.

Katika shauri hilo, hoja zilizokuwa zikibishaniwa ni endapo mlalamikiwa alikuwa na sababu halali zilizofanya mlalamikaji aachishwe kazi, endapo mlalamikiwa alifuata utaratibu halali wakati wa kumwachisha kazi mlalamikaji na nafuu zipi kila upande unastahili.

Mwakilishi wa mlalamikaji akitoa ushahidi mbele ya Tume hiyo, anasema mlalamikaji (Saitoti Oyaya) alikuwa mfanyakazi wa mlalamikiwa kama mlinzi Aprili, 2012 kwa ujira wa Sh 155,000 kwa mwezi.

Julai, 2012 alibadilishwa kitengo na kuwa mkaguzi wa mgari. Hata hivyo, hakukuwa na badiliko la ujira akiwa chini ya mkuu wake wa Idara ambaye ni Afisa Usafirishaji. Agosti alibadilishwa kazi na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo kwenda kwenye kitengo cha ununuzi wa spea za magari ambako mlalamikaji aliwajibika kwa Afisa Ununuzi wa Spea, Taji Mohamed Abasi.

Katika kitengo hicho alifanya kazi mbili – ununuzi wa spea na huduma ya chakula kwa viongozi wake wa kazi – na ujira wake kwa mwezi ulikuwa Sh 270,000.

Anasema amefanya kazi kwa uaminifu mkubwa na kuzingatia taratibu zote. Hata hivyo, siku moja alipewa maelekezo na mwajiri wake kwamba atafute spea ambayo ni screw ya inchi 4 na asipoipata asifike kazini na kazi hiyo aliifanya kwa siku mbili bila mafanikio.

Jumanne, Februari 18, 2014 anasema aliitwa na Afisa Rasilimali Watu, Grace Charles, aliyemweleza kwamba hatakiwi kufanya kazi ya aina yoyote kutokana na maelekezo aliyopewa kwa njia simu na mkurugenzi.

Aliporudi kutoka katika majukumu yake nje ya ofisi siku hiyo hiyo ambayo ilikuwa ni ya tatu ya utafutaji wa spea hiyo bila mafanikio, alizuiwa na mlinzi kuingia ndani ya ofisi, yakiwa ni maelekezo kutoka kwa mwajiri wake.

“Sikupewa barua yoyote zaidi ya kukabidhiwa kwa mlinzi wa getini na kuelezwa kuwa sitakiwi tena kuingia eneo la kazi la mwajiri na kwamba nimefukuzwa kazi.

“Pamoja na kuachishwa kazi bila utaratibu nililipwa Sh 930,000 mbele ya Tume ikiwa ni makato ya mshahara Sh 500,000, likizo 270,000 na mshahara nusu kwa mwezi wa pili wa siku 18,” anasema.

Mlalamikaji anapinga kuachishwa kazi na mlalamikiwa kinyume na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004 ambayo inaeleza bayana juu ya sababu na taratibu halali wakati wa kusitisha ajira kifungu cha 37 (1), (2) a na b (i), (ii), (c).

Saitoti ameshinda shauri hilo na mlalamikiwa kuamuriwa kumlipa fidia ya mshahara wa miezi 12, hati ya utumishi na kiinua mgongo na vyote vikifikia jumla ya Sh 3,385,385 na uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 88 (8) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6 ya 2004.

“Uamuzi huu utekelezwe ndani ya siku 14 tangu utolewe, aidha nafasi ya marejeo ipo wazi kwa upande wowote usioridhika na uamuzi huu,” imeeleza nakala hiyo ya uamuzi iliyotolewa na Tume Desemba 30, 2015 na kusainiwa na Mwamuzi wa shauri hilo, Fungo E. J.

Hata hivyo, mlalamikiwa hajatekeleza maelekezo aliyopewa na Tume hiyo hadi sasa na badala yake amekata rufaa Mahakama Kuu.

 

Waliochapwa viboko

Waliochapwa viboko na wamiliki wa kampuni hiyo ni Langson Nyansulu na Ali Dauda na kufungua mashauri yao mwaka 2013.

Wengine ni Sam Mwakarobo, Joseph, Augustine Msigwa ambao ni madereva waliofungua mashauri yao mwaka 2015 ambayo hayajapatiwa ufumbuzi hadi sasa.

“Tuna familia zetu hadi wajukuu, tumeingizwa tena katika utumwa huu wa kuchapwa bakora na Waarabu hawa waliokuwa wakilindwa na baadhi ya watendaji katika utawala uliopita, na sasa hatutakubali kudhalilishwa namna hii,” ameeleza mmoja wa wafanyakazi hao.

Baadhi ya wafanyakazi wameielezaJAMHURI kwamba uongozi wa kampuni hiyo umeanza kuwapa vitisho na kuwasaka waliotoa habari kuhusu manyanyasho na ukwepaji wa kodi kwa kutumia namba za magari za bandia.

 

Uongozi wa Usangu

JAMHURI ilimtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa Usangu Logistics (T) Ltd, Ibrahim Ismail, kwa mara nyingine bila mafanikio.

Hata hivyo, wiki iliyopita, Mkurugenzi wa Fedha, Saad Ismail, ambaye pia ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni hiyo, amezungumzia unyanyasaji wa wafanyakazi na ukwepaji wa kodi za Serikali, kwa kutumia namba bandia katika magari yake. Amesema hawezi kushangazwa na malalamiko hayo kwani mfanyakazi anaweza kusema chochote.

Hata hivyo, hakutaka kuzungumza zaidi kwa madai kwamba yeye si msemaji wa kampuni, bali atafutwe Mkurugenzi.

By Jamhuri