Mwekezaji katika mgodi wa uchimbaji wa madini ya tanzanite na mmiliki wa Kampuni ya TanzaniteOne Mining Ltd, anadaiwa kufanya hujuma katika biashara ya madini nchini.

Mwekezaji huyo ambaye anamiliki asilimia 50 ya mgodi huo anaelezwa kufanya hujuma ya kutorosha madini katika mgodi huo na kuyasafirisha nje ya nchi bila kuishirikisha Serikali ambayo ni mbia wake kupitika Shirika la Taifa la Madini (STAMICO). Stamico pia wanamiliki asilimia 50 ya hisa katika mgodi huo.

Tanzania ndiyo nchi pekee inayozalisha tanzanite duniani, lakini India inaongoza kwa kuuza tanzanite nyingi ikifuatiwa na Kenya katika soko la dunia na hivyo kuwapo taarifa kuwa inatoroshewa katika nchi hizo.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya mgodi vimeidokeza JAMHURI kuwa umekuwa utamaduni kwa mwekezaji huyo kutorosha madini ya tanzanite na kuyauza kinyume cha taratibu.

Inaelezwa kuwa tangu TanzaniteOne walipoingia ubia na Stamico wamekuwa na mchezo wa kutoa ripoti za uongo za uzalishaji wa madini huku zikionesha kiwango kidogo kinachopatikana tofauti na hali halisi ya uzalishaji.

JAMHURI imedokezwa kuwa awali madini hayo yalipopatikana yalikatwa kupelekwa sokoni, lakini kinachofanyika sasa mawe yenye madini yanapopatikana hutolewa mgodini kinyemela na kupandishwa juu bila kuhusisha pande mbili na kukimbizwa kusikojulikana, huku mengine yakiuzwa kwa wafanyabiashara wakubwa wa madini jijini Arusha.

Imedaiwa kuwa wiki mbili zilizopita, TanzaniteOne walipata madini ya kiwango cha juu ambayo yanakadiriwa kuwa zaidi ya kilo 150.

Mtoa taarifa anasema Jumamosi ya Februari 27,2016 wamiliki wa TanzaniteOne waliingia katika chumba cha kuhifadhia madini mgodini hapo ‘strong room’ wakiwa na mabegi mawili ambapo moja lilikuwa na mawe machafu na kuyabadili na madini ambayo waliondoka nayo na kuacha mawe yasiyo na viwango hivyo.

“Siku ya Jumamosi tarehe 27/2/2016 mlinzi akiwa Amani Ndege, mabosi ambao ni Faisal, Gonga na Ridhwani waliingia strong room na kubadili madini. Kesho yake tarehe 28, askari aliyekuwa zamu ni Imani Mbunda, na Kamanda wa Section, alikuwa Mayengo Sostenes, lakini katika hali isiyo ya kawaida, mkuu wa ulinzi alikuja na kumbadilisha na kumweka Remta ambaye ni mgeni.

“Mchezo huu waliufanya kwa kushirikiana na baadhi ya watu wa Stamico pamoja na mtu wa kamera ambaye aliizima kuepuka kuonesha tukio hilo,” anasema mtoa taarifa.

Inaelezwa kuwa wawekezaji hao wamechukua zaidi ya kilo 50 za madini yaliyopatikana yanayokadriwa kuwa na thamani zaidi ya billion 200 na kutokomea nayo kusikojulikana, hivyo kupunguza uzito wa madini halisi yaliyopatikana mgodini hapo.

Anaeleza kuwa umekuwa mchezo wa wawekezaji hao kuondosha madini mgodini na kuyasafirisha nje ya nchi kwa kutumia baadhi ya watu ambao huletwa kwa kazi hiyo mgodini hapo.

Anasema Machi 6, saa 6:20 usiku, vijana wapatao 10 wenye asili ya Kihindi walifika mgodini hapo wakitokea mpaka wa Namanga. Vijana hao walikuwa wamebebwa na gari aina na Land Cruiser Na T 748 DFW linalomilikiwa mdogo wake Faisal huku mizigo yao ikipakizwa kwenye gari namba T 143 ASC.

Vijana hao awali walizuiwa kuingia Mirerani na maafisa wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kutokana na kutokuwa na nyaraka zilizowaruhusu kuingia nchini, hivyo walilazimika kwenda nchini Kenya kwanza na kutumia njia ya barabara kurejea nchini.

Pia inadaiwa kuwa mwekezaji huyo amekuwa na kawaida ya kutotoa takwimu za kweli za uzalishaji madini za kila siku kwa serikali.

JAMHURI ilifanya mahojiano na Mkurugenzi wa Stamico, Zena Tuguta, na anasema kuwa hana taarifa zozote kuhusiana na utoroshwaji wa madini na kuwa apewe muda wa kufuatilia kwa ukaribu.

Zena anaendelea kusema kuwa iwapo jambo hilo limetokea ni lazima ahusishe timu yake iliyopo mgodini pamoja na vyombo vya ulinzi maana ni kinyume na taratibu za nchi.

Alipoulizwa iweje yeye asipate kusikia jambo hilo ambalo limefanyika wiki mbili zilizopita wakati ofisi yake ni mmoja wa wamiliki wa mgodi huo, akasema ni mpaka apokee taarifa kamili na kuwa mambo yanayohusu wizi yanahusisha timu za uchunguzi.

Kamishna Msaidizi wa Madini na Mkaguzi Mkuu wa Madini, Injinia  Ally Samaje, anasema ofisi yake haijapata taarifa hivyo itafutilia kwa kina.

Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhungo, anasema hivi karibuni alikuwa mkoani Arusha kuwa alisikia uwepo wa wizi mkubwa wa madini na kuwa alithibitishiwa kuwa unafuatiliwa kwa kina.

“Walinithibitishia kuwa wanafuatilia kila kitu, hayo unayosema ni zaidi ya hayo maana ni zaidi. Nilikuwa Arusha na niliongea  nao kwa hiyo wacha nicheki tena nitarudi kwako,” anasema Prof. Muhongo.

Akizungumzia utoroshwaji wa madini nchini, anasema ni kweli kumekuwa na utoroshwaji wa madini nchini, lakini tayari ofisi yake imeanza kubuni mbinu mpya za kukabiliana na wizi huo.                                                                                                   

Mwekezaji huyo pia anadaiwa kukiuka sheria za uchimbaji madini kwa kupasua miamba bila kuzingatia athari zinazoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na usalama wa mgodi na wafanyakazi wake, ambapo miamba ambayo iliachwa kwa ajili ya usalama wa mgodi imekuwa ikivunjwa.

Katika ripoti ya ukaguzi iliyofanywa na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini ya Desemba 8, 2015 imebainisha kuwapo kwa ukiukwaji wa taratibu za uchimbaji madini na kuhatarisha usalama wa mgodi na wachimbaji wake.

Mwekezaji huyo anadaiwa kukodisha wachimbaji binafsi ambao huingia mgodini na kuchimba madini ambayo huondoka nayo.

Baadhi ya wafanyakazi wanaeleza kuwa mwekezaji huyo amewaachisha kazi watu wanaoonekana kuwa kikwazo katika utoroshwaji wa madini mgodini hapo.

“Hataki kusikia kuhusiana na wanachama wa chama cha wafanyakazi ambao walikuwa wakihakikisha sheria zinafuatwa mgodini. Watu wameachishwa kazi kinyume na taratibu. Tunashindwa kumuelewa huyu mwekezaji nguvu hii anaitoa wapi. Ingawa tumesikia kuna wakubwa nyuma yao.

“Kamati ya ulinzi na usalama ya mikoa mitatu, ilifika mgodini na kukuta hao wachimbaji waliokodishwa. Walipohoji uongozi ukawadanganya kuwa wameletwa mgodini kwa ajili ya kufanya usafi, jambo ambalo si kweli,” anasema mtoa taarifa wetu.

Faisal Sharbat anasema mwishoni mwa Februari walipata kilo100 za tanzanite na kwamba madini hayo yapo.

Alipoulizwa kuhusiana na wao kuingia chumba cha kuhifadhia madini na kuyabadilisha na mawe, akasema hizo ni habari za uongo na kuwa siku hiyo hawakuingia humo kwani tangu siku uzalishaji huo ulipotokea hawajafika mgodini.

JAMHURI ilipotaka kufahamu madini hayo yanavyohifadhiwa akasema hiyo ni siri ya kampuni na kuwa hata uuzwaji wake utakuwa wa kipekee maana utakuwa wa uwazi zaidi kuondokana na minong’ono ya aina yoyote.

“Kupatikana kwa madini ni kweli kabisa, lakini mtu akitaka kuongea anaongea tu. Hizo hoja zingine ni uongo na kutaka kutuchafua, mzigo bado upo na upo salama kabisa. Na kuhusu sisi kuhusika kufanya uhujumu sio kweli, bali kuna wafanyakazi ambao walikuwa wakituhujumu hapo awali sasa tumewabana wasiibe maana walikuwa wanatuhamisha na kutupindisha hivyo tunakosa uzalishaji,” anasema Faisal.

 Suala la uingizwaji wa vijana 10 kutoka nje ya nchi, anasema ni kweli vijana hao waliingia nchini kupitia uwanja wa ndege wa KIA na kuwa walizuiwa kuingia nchini kutokana na kutokuwa na vibali vya kazi bali walikuwa na risiti tu za vibali hivyo, jambo lililoifanya Serikali kuwazuia wakaamua kuwapeleka nchini Kenya kusubiri upatikanaji wa vibali hivyo.

Hata hivyo, amekana vijana hao kuingizwa nchini kinyemela na kueleza kuwa bado hawajaingizwa nchini na kuwa taarifa hizo ni uzushi na uongo.

Kuhusiana na kukodisha mgodi kwa wachimbaji wadogo, anasema hawajawahi kufanya hivyo na kwamba waliwahi kuwa na makubaliano na mmoja wa wachimbaji wadogo kufukua mgodi (contract task) kwa vipindi vifupi.

Pia anasema suala la kampuni hiyo kuchimba nguzo za mgodi, anasema: “Huo udhaifu sio sisi. Hata wafanyakazi wamekuwa wakipiga nguzo waweze kupata maslahi yao, lakini tayari Kamishna Injinia Samaje alishakuja na kusema kuwa mgodi upo salama. Hivyo nakuhakikishia hayo yanayosemwa siyo kweli ni uongo.”

Desemba 2015, raia wa India anayedaiwa kuwa mfanyabiashara wa  madini, Anurag Jain, alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akiwa na vipande 264 vya madini aina ya tanzanite yenye uzito wa kilo mbili.

Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Alex Magayane, anasema mtuhumiwa alikamatwa uwanjani hapo akijiandaa kusafirisha madini kwenda Hong Kong ambayo yalikuwa na thamani ya Sh bilion 2.5.

Katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Novemba mwaka huu Wakala wa Madini wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) wamekamata madini yanayotoroshwa katika viwanja vya ndege katika matukio 23 tofauti.

Kifungu cha 6(4) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2015 kinaipa mamlaka Serikali kutaifisha madini yanayokamatwa yakipelekwa nje ya nchi kinyemela.

Katika kipindi cha miaka miwili na nusu kuanzia Julai, 2012 hadi Desemba, 2015, Serikali imepoteza kiasi cha shilingi billion 18.9 kupitia utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi kupitia viwanja vya ndege. 

Sekta ya madini nchini inachangia asilimia 3.5 ya uchumi lengo la kisera ni kuwa ifikapo mwaka 2025, madini yatakuwa yanachangia asilimia 10.

By Jamhuri