ngorongoro entrance2Kusimamishwa kazi kwa wahasibu watano na watumishi wengine 15 wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa tuhuma za ubadhirifu wa mabilioni ya shilingi za Mamlaka hiyo, kunatajwa kuwa hakujamaliza wimbi la ufisadi katika Mamlaka hiyo.

JAMHURI imethibitishiwa kuwa kuna mtikisiko mwingine mkubwa utakaoikumba NCAA ambao utashuhudia wengine wakitimuliwa.

Ngorongoro, Mamlaka inayokusanya mabilioni ya shilingi kila mwaka huku kiasi kikubwa kikiishia mifukoni mwa watumishi kadhaa wasio waaminifu, imekuwa kwenye hali hiyo kwa miaka mingi.

Chanzo cha habari kinasema kuwekwa kando kwa watumishi hao pekee, ingawa ni hatua murua, hakutakuwa na maana endapo majipu makubwa, akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Pius Msekwa, hawatashitakiwa kwa ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Duru za uchunguzi zinaonesha kuwa wakati fulani Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), ilishamwandalia mashitaka Msekwa, lakini uongozi wa Awamu ya Nne ukafuta kusudio hilo ili ‘kulinda heshima’ ya mkongwe huyo wa siasa nchini.

Madudu katika Ngorongoro yameanikwa zaidi wakati wa uongozi wa Waziri Khamis Kagasheki, ambaye Kamati aliyoiunda ilibaini ufisadi wa kutisha uliosababisha kufukuzwa kazi na kusimamishwa kwa vigogo kadhaa.

Kwenye Bodi ya wakati huo, pamoja na wajumbe wengine, pia alikuwamo Spika wa sasa wa Bunge, Job Ndugai.

Uamuzi mzito uliochukuliwa na Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA, Balozi Mwanaidi Maajar, ulikumbana na vikwazo vingi kutoka kwa wakubwa akiwamo Waziri wa Maliasiali na Utalii wa wakati huo, Lazaro Nyalandu.

Inaelezwa kuwa Nyalandu alifanya kila aliloweza ili Balozi Maajar asiwatimue watuhumiwa wa ufisadi, lakini mwanamama huyo akawa amesimama kidete na hatimaye kuwawajibisha baadhi ya waliotuhumiwa.

Hata hivyo, uchunguzi wa JAMHURI kutoka vyanzo vya habari vya uhakika, umebaini kuwa bado kuna juhudi kubwa zinazofanywa na mmoja wa viongozi wakubwa katika mmoja wa mihimili ya dola, anayetaka waliofukuzwa kazi waachwe huru.

Kazi hiyo tayari imeshaanza kufanywa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Dk. Mary Mwanjelwa, ambaye hivi karibuni wakati wa vikao vya Kamati, alidai maelezo kutoka kwa uongozi wa NCAA akidai unatoa madai ya uongo dhidi ya watumishi wake.

Hata hivyo, kuna taarifa za uhakika kuwa Dk. Mwanjelwa anafanya hivyo ili kumnusuru mmoja wa vigogo wa NCAA aliyefukuzwa na anayetajwa kuwa na uhusiano wa kijamii na mmoja wa viongozi waandamizi katika mmoja wa mihimili ya dola.

Wiki iliyopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, alifanya ziara ya ghafla katika Mamlaka hiyo na kutangaza kuwasimamisha kazi kwa tuhuma za ufisadi wa mabilioni ya shilingi wahasibu Maria Njau, Joseph Ntwala, Ally Amiry, Joseph Msafiri na John Mlambo.

Watumishi wengine walihamishwa kikazi kwenda sehemu mbalimbali za wizara hiyo. Nao ni Meneja Mipango, Joseph Mshana; Kaimu Meneja Ikolojia, Patrice Matay; na Injinia Isra Misama ambaye ni Meneja wa Huduma za NCAA.

Wengine ni wafanyakazi wawili wa Idara ya Utalii – Amina Ponera na Richard Hyri; wahasibu wawili – Agatha Ambrose na Lugoba Lyambogo; Charles Mayuya (PMU); Mtunza Stoo, Edmund Sabutoke; na watumishi wawili wa Idara ya Fedha – Fanuel Mfinanga na Jonathani Mugisha.

Pia wamo Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Esther Makacha; Mtunza kumbukumbu za NCAA, Rebecca Missoji, mtumishi wa Idara ya Hifadhi, Emmanuel Nyangaro, na mtumishi wa Idara ya Ujirani Mwema, Francis Kone.

“NCAA ilikuwa shamba la bibi, kila mtumishi alikuwa akichota mabilioni ya shilingi kama anavyotaka bila ya kuchukuliwa hatua yoyote. Wahasibu walifikia hatua ya kukosa huruma na fedha za umma na kudiriki kuchakachua mfumo mzima wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato ya Mamlaka na kujiingizia fedha katika akaunti zao,” alisema Profesa Maghembe.

Watumishi wa NCAA wanatajwa kuwa na ukwasi mkubwa wa mali – nyumba na magari. Wengi wanatajwa kuwa na ghorofa kadhaa katika miji ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Moshi.

Mathalani, mmoja wa watumishi waliofukuzwa mwaka jana, aliandaa sherehe ya kuzaliwa mwanae na akapanga magari kadhaa ya kifahari ili mtoto aweze kuchagua alilopenda. Jina lake tunalihifadhi kwa sasa.

“Hawa bila kuwafilisi mali zao Serikali ya Dk Magufuli itakuwa haijafanya kitu. Wana mali nyingi sana, na zinajulikana ingawa wengine kwa sasa wanahaha kubadili umiliki wake,” kimesema chanzo chetu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mwanzoni mwa mwaka huu, JAMHURI iliripoti kuwa vigogo wanne wa NCAA walifukuzwa kazi, na wengine watatu wameshushwa vyeo kwa makosa ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Takukuru mkoani Arusha iliwafungulia kesi vigogo hao pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa NCAA, Bernard Murunya. Kwa sasa Murunya ni Mbunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki.

Waliofukuzwa ni Meneja Huduma za Utalii, Veronica Ufunguo; Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Elinipendo Mwambo, Mhasibu Msaidizi, Veneranda Baraza, na  Keshia, Daniel ole Moti.

Pamoja na kufukuzwa, wanne hao walitakiwa warejeshe mamilioni ya shilingi waliyojipatia kwa njia zinazoelezwa kuwa si halali, na hivyo kuiingizia Mamlaka na Serikali hasara.

Hatua ya kuwafukuza ilichukuliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka hiyo, kupitia Kamati yake ya Nidhamu iliyochunguza tuhuma zilizowakabili.

Habari kutoka ndani ya Bodi zilisema kulikuwa na mvutano mkali kwenye suala hilo, kutokana na baadhi ya vigogo hao kupita huku na kule (kwa viongozi wakuu wa kitaifa wa Awamu ya Nne) wakitafuta kukingiwa kifua.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu, ni miongoni mwa waliotaka vigogo wote waachiwe kwa madai kwamba kilichotakiwa ni “kufungua ukurasa mpya” wa utendaji kazi.

Pamoja naye, kuna kiongozi mwingine mwandamizi ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ambaye mmoja wa waliowajibishwa ni mtoto wa ndugu yake.

“Ana mtoto wa ndugu yake, kila mara alitaka hii kashfa itupwe, lakini uongozi wa Bodi ukasimama imara. Huwezi kuamini, kuna wakati walidiriki kusema Rais (Jakaya Kikwete) ameagiza uchunguzi dhidi ya watuhumiwa uachwe, lakini baadaye ikabainika zilikuwa mbinu tu za kukwamisha uchunguzi,” alisema mmoja wa wajumbe wa Bodi.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Uendeshaji, Injinia Joseph Mallya, alistaafishwa na kutakiwa arejeshe dola 11,140 za Marekani.

Waliorejeshwa kazini kwa wakati huo na kushushwa vyeo ni Meneja Huduma za Uhifadhi, Amiyo Amiyo, Meneja Maendeleo ya Jamii, Justice Muumba, na Nickson Nyange aliyekuwa Ofisa Uhusiano.

Pamoja na kushushwa vyeo, waliamuriwa warejeshe dola 18,000 za safari walizojipatia kwa njia zisizo halali. Kati ya wote hao, taarifa zinasema ni Nyange pekee aliyekubali kurejea kazini. Amiyo na Dk. Muumba walifungua kesi wakipinga uamuzi wa Bodi.

Miongoni mwa malalamiko yao ni kwamba Bodi haikuwapa fursa ya kujitetea kwa kina waliposhitakiwa kwa makosa yaliyokuwa yakiwakabili ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.

Murunya, Ufunguo, Shaddy Kyambile (aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha) na Mkurugenzi wa Kampuni ya Cosmos wameshafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za ubadhirifu wa dola 68,000 za Marekani kwa ununuzi wa tiketi za ndege, na malipo kufanywa mara mbili.

Awali, vigogo hao walisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi. Uamuzi wa kuwasimamisha ulitolewa na Bodi ya NCAA iliyoketi katika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam Novemba 4, mwaka jana.

Bodi iliagiza Menejimenti ya NCAA ihakikishe Polisi wanashirikiana na Mwenyekiti wa Tume Maalumu iliyokagua NCAA na mawakili wa nje ya Mamlaka hiyo ili kufanya uchunguzi na hatimaye watuhumiwa wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.

Aliyekuwa Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Murunya, Bodi ilisema anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na kutosimamia vema majukumu yake na kuisababishia hasara kubwa NCAA.

Wakurugenzi na mameneja wengine nao walitakiwa wafike mbele ya Bodi wajieleze kutokana na kukabiliwa na tuhuma za uzembe na kutowajibika. Miongoni mwao walikuwa ni Bruno Kawasange, Joseph Mshana, Injinia Isra Missana, Patrice Mattay na Adam Akyoo.

Bodi iliwataka wote waliochukua, au waliotumia mali za NCAA vibaya wazirejeshe mara moja.

Katika hatua nyingine, aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi NCAA, Leonard Minzi, alistaafu Novemba 8, 2014. Johnson Saiteu Laizer aliteuliwa kuwa Kaimu Meneja wa Kitengo cha Uratibu wa Ununuzi.

Kikao cha Bodi ya NCAA cha Novemba 4, mwaka jana; pamoja na Mwenyekiti Balozi Maajar, wajumbe wengine waliohudhuria walikuwa ni Donatus Kamamba, Lucas Selelii, Lukonge Mhandagani, Juma Pinto, Dk. David Mrisho, Laban Moruo, Metui ole Shaudo, Dk. Aikande Kwayu, Francis ole Siapa na Dk. Freddy Manongi (Katibu wa Bodi na Mhifadhi wa NCAA). Mjumbe mwingine, Job Ndugai, hakuhudhuria.  

Wakati wa kujadiliwa kwa dondoo ya viongozi wanaopaswa kuwajibishwa, wajumbe wanne walitangaza mgongano wa maslahi kutokana na kuwapo kwao kwenye Bodi iliyopita ambayo ufisadi huo ulifanyika chini ya uongozi wao. Wajumbe hao ni Shaudo, Selelii, Moruo na Kamamba.

By Jamhuri