Mkuu wa Mkoa K’njaro atangaza operesheshi sita

Mbunge-wa-Jimbo-la-Mvomero-Amos-Makala-akifafanua-jambo-kwa-wananchi-hawapo-pichani.Mkuu wa Mkoa (RC) wa Kilimanjaro, Amos Makalla, ametangaza operesheni sita kabambe zikilenga kukomesha uhalifu, kuhimiza uwajibikaji, kulinda afya za wananchi na kutunza mazingira. 

RC Makalla alitangaza operesheni hizo kwenye kikao cha kazi kilichowahusisha wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro, wakurugenzi, wakuu wa idara na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa wilaya za mkoa huo.

Operesheni alizotangaza ni:

1: Operesheni udhibiti upikaji na uuzwaji gongo; na unywaji aina yoyote ya pombe wakati wa kazi

2: Operesheni udhibiti uhalifu Mkoa wa Kilimanjaro

3. Operesheni udhibiti dawa za kulevya 4. Operesheni udhibiti upitishaji na usafirishaji wahamiaji haramu

5. Operesheni udhibiti ukataji miti na uchafuzi wa mazingira; na 

6: Operesheni kushughulikia wazembe na watoa huduma zisizoridhisha katika ofisi za umma

Kwa kuonesha amedhamiria kuona mafanikio kwenye operesheni tano za mwanzo, Makalla alimkabidhi Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro simu kutoka kampuni ya tigo yenye namba 0659-300-600.

Simu hiyo ni mahususi kwa watumiaji wote wa mawasiliano ya mtandao wa tigo. Huduma zote za kupiga, kupeleka ujumbe mfupi wa maandishi (SMS), picha mnato na picha za video ni bure.

“Namba hizi zibandikwe kwenye vituo vyote vya polisi, ofisi zote za Serikali, kila ofisi za kijiji, kata, zahanati, vituo vya afya na kila mahali popote ambako mwananchi anaweza kuiona. Huduma hii ni bure kuanzia kupiga, kutuma meseji, picha za kawaida, picha za video, WhatsApp na kadhalika. Mwananchi akiona tukio awasiliane na kamanda kwa namba hii mara moja ili tushirikiane kukomesha uhalifu huu.

“Kwa kweli napenda kuona Mkoa wa Kilimanjaro ukiwa wa mfano katika kukabiliana na masuala haya niliyotangaza operesheni,” alisema Makalla. Kwa watumiaji wa mitandao mingine, RC Makalla amesema watatumia namba hiyo kwa huduma alizozitaja kwa kuzilipia kwa viwango vya kampuni ya simu inayotumiwa na mwananchi.

Pia anaandaa namba maalumu kutoka Vodacom kwa ajili ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, dawati la kero ambayo itatumiwa na wananchi kupeleka SMS na kupiga simu wasiporidhishwa na huduma.

“Namba hiyo itawekwa mapokezi hospitali zote, vituo vya afya, zahanati na ofisi zote za Serikali kuanzia ngazi ya kijiji, kata wilaya na mkoa,” alisema.

Sambamba na hilo, amehimiza agizo la Serikali kwa watumishi wa umma kuvaa kitambulisho chenye jina la kila mtumishi ili kurahisisha utambuzi kwa watumishi wanaohudumia vizuri na wale wanaotoa huduma zisizofaa kwa wananchi.

Ameagiza wakuu wote wa wilaya na wakurugenzi wao kila siku ya Alhamisi wasikilize kero za wananchi kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa saa 8 mchana.

“Vikao hivyo ni mahususi kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi. Watumishi mbalimbali wawepo, lakini ambao hawapaswi kukosekana kabisa ni watu wa ardhi. Hao lazima wawepo maana mkoa wetu kero namba moja ni migogoro ya ardhi. Maofisa ardhi lazima wawepo kujibu maswali na kutoa majawabu kwa kero za wananchi.

“Siku ya Alhamisi hakuna DC kuwa na ziara, kazi yake na watumishi wengine ni kusikiliza kero za wananchi ili kero zinazoweza kumalizwa ngazi ya huko, ziiishie huko huko badala ya kufika kwangu au katika ngazi za juu serikalini.

“Kero kwa wananchi ni nyingi na zinawafanya waichukie Serikali yao bila sababu. Hilo nasema sasa basi. Nasisitiza, ofisa ardhi lazima awepo kwenye kikao hicho bila kukosa. Mkikaa vikao bila ofisa ardhi itakuwa bure. Mkifanya vikao hivi mtagundua madudu mengi sana. Hapa hakuna excuse, DC mbane DED. Hakuna mtu kutuma mwakilishi.

“Maofisa kilimo waende vijijini wahamasishe kilimo. DC aone uhaba wa chakula kama kigezo cha kukosa uteuzi, kilimo cha umwagiliaji kipewe kipaumbele.

“Waratibu wa elimu wasimamie elimu. Wapo wengine wanaendesha bodaboda, nawaagiza mtoke sasa mkaone kinachofanyika katika shule.

“Kuhusu kipindupindu, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameusifu mkoa wetu kwa kudhibiti ugonjwa huo. Lazima wataalamu wa afya wapiti kote waone hali ya ugonjwa na dawa ikoje, maana tunapokea wagonjwa kutoka Manyara.

“Uchezaji pool kwa vijana uwe wa muda maalumu. Muda mrefu utumiwe na vijana kufanya kazi ili kuendana na dhana halisi ya ‘Hapa Kazi Tu’ ya Mheshimiwa Rais John Magufuli.

“Wahamiaji haramu wanachafua sifa ya mkoa wetu. Ni aibu wakikamatwa mikoa mingine ya mbali kama Morogoro au Mbeya wasema walipitia Holili au sehemu yoyote ya Mkoa wa Kilimanjaro. Tuzuie kabisa biashara hii. Nawapongeza Uhamiaji… wanafanya kazi kubwa. Naagiza kazi hii ya kudhibiti wahamiaji haramu na usafirishaji binadamu iwe ya kudumu.

“Naagiza kila kiongozi mwenye dhamana kuhakikisha anashiriki katika kukomesha uhalifu. Majambazi na wahalifu wengine wasipewe nafasi katika mkoa wetu.

“Hilo liende sambamba na mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Same wamefanya kazi kubwa sana katika vita hii ya mirungi. Kuna taarifa ya kuwapo mashamba 921 ya mirungi, lakini imebainika yapo zaidi ya 1,500. Tayari uteketezaji wa hiari umefanikisha kuteketeza ekari 200 (asilimia 73). Asilimia iliyobaki wanagoma kuteketeza wenyewe. Tutapambana nao, hatutorudi nyuma hata kwa hatua moja. Tumejipanga kuishinda vita hii,” anasema Makalla.

Kwa upande wa kero za wananchi, RC Makalla anawasisitiza viongozi wenzake kwa kuwaagiza: “Tushughulike na matatizo ya watu. Holili kuna watu wamepewa double allocation ya viwanja tangu mwaka 2006. Miaka yote wananchi wanalalamika, wananchi wanaonewa, wanapewa risiti feki. Nimeagiza wale maofisa ardhi waliohamishwa warejeshwe wajibu mashitaka. Hatuwezi kukubali hali hii iendelee maana inawafanya wananchi waichukie Serikali yao.”

Kuhusu utengenezaji, uuzaji na unywaji gongo, RC Makalla amesema tatizo hilo ni kubwa Wilaya ya Rombo, na kwamba anashukuru juhudi za uongozi, akiwamo Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, za kujitokeza kukabiliana na janga hilo.

“Kuna unywaji gongo uliopindukia, kuna watendaji wanaandika barua na kupiga mihuri wakiwa baa, unywaji pombe muda wa kazi marufuku,” amesema.

Pia Mkuu wa Mkoa alikemea tabia ya watumishi wa umma kutumia muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii badala ya kuwahudumia wananchi.

“Kuna ma-admin (waendesha mitandao), muda mrefu wanatazama mle kuangalia wachangiaji, wanaangalia nani aingie, na nani atoke. Haangalii mafaili ya ofisi. Wakati mwingine akiingia akiona kimya anauliza ‘humu ndani mbona kimya?’ Admin anafanya kazi ya twitter, yujo Instagram, yuko kwenye magazeti. Sikatazi kuwa admin, lakini timiza kwanza wajibu wako. Wapo wanaolalamika na kuomba mishahara iongezwe! Rais kasema mnampima kwa siku 100, ninyi mmetekeleza wajibu wenu? Tutekeleze wajibu wetu kama viongozi,” alisema.