Wafaulu bila kujua kusoma wala kuandika

Na Alex Kazenga
MVOMERO
Wakati matokeo ya darasa la saba kwa mwaka jana nchini yakionesha ufaulu kuongezeka kwa
asilimia 72.76 ikilinganishwa na 70.36 ya mwaka 2016, imebainika kuwapo waliofaulu bila kujua
kusoma wala kuandika.
Uwepo wa hali hiyo ya watoto kufaulu bila kujua kusoma wala kuandika, imebainika hivi karibuni
kupitia uchunguzi uliofanywa na JAMHURI katika Kijiji cha Kambala, Wilaya ya Mvomero
mkoani Morogoro.
Shule ya Msingi Kambala ni kielelezo cha shule zinazolalamikiwa na wananchi kufaulisha
wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika.
Katika matokeo ya darasa la saba ya mwaka jana, shule hiyo ya msingi Kambala ilishika nafasi
ya 32 kati ya shule 68 zilizopo Wilaya ya Mvomero na 328 kati ya shule 490 za mkoani
Morogoro ‘ikiambulia’ nafasi ya 4,796 kitaifa, kati ya shule 9,736.
Katika mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka jana, shule hiyo ilikuwa na watahiniwa 51
ambapo wanafunzi 37 walifaulu kujiunga na sekondari miongoni mwao wakiwamo wasiojua
kusoma na kuandika.
Lucia Jacob (14) (si jina lake halisi) ni mmoja wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka
jana shuleni hapo na kufaulu mtihani akiwa hajui kusoma wala kuandika.
JAMHURI limezungumza na mtoto huyu na kujiridhisha pasipo shaka kwamba hajui kuandika
na kusoma. Hata alipotakiwa kuandika majina yake ama kusoma mahali palipoandikwa jina la
kijiji anapoishi na wazazi wake (Kambala), alishindwa.
Taarifa kutoka vyanzo tofauti zinaeleza kuwa tatizo hilo halipo kwa Lucia pekee, bali wanafunzi
wengi hasa wasichana wanahitimu elimu ya msingi pasipo kujua kusoma ama kuandika.
Serikali yalalamikiwa
Wazazi wa Kijiji cha Kambala wanamlalamikia Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Kambala kwa
kuwafaulisha watoto wasiojua kusoma wala kuandika, hivyo hawawezi kuwapeleka sekondari
watoto wao kwani wamefaulu huku hawajui kusoma wala kuandika.
Afisa Mtendaji wa Kijiji Ngayama, Mussa, anasema kwamba ni kweli tatizo hilo limetokea kijijini
hapo na kutaja kaya tano ambazo zina wanafunzi anaowafahamu waliofaulu ilhali hawajui
kusoma wala kuandika.
Miongoni mwa kaya zilizotajwa, mzazi wa mwanafunzi Lucia ndiye aliyekuwa tayari kuonesha
ushirikiano na kumruhusu mwanae kuzungumza na JAMHURI huku kaya nyingine zikigoma
kufanya hivyo.
Ili kujiridhisha na hali hiyo JAMHURI lilimpatia shilingi elfu kumi (10,000) mwanafunzi Lucia
kama mtego, kwamba endapo akiweza kuandika majina yake yote na la kijiji chake hiyo hela
ingekuwa zawadi yake.
Lucia alishindwa kuandika, hata alipoandikiwa chini majina yake yote na jina la kijiji chake
hakuweza kusoma, zaidi ya kuyachekea maandishi na kuishia kuonesha tabasamu la aibu
mbele ya watoto wenzake na baba yake mzazi.
Kwa mujibu wa utafiti wa kihabari uliofanyika kijijini hapo, wapo wanafunzi wa kike
wanaoelekezwa na wazazi wao kuionesha jamii kwamba hawajui kusoma na kuandika ili
‘kufungua’ fursa ya kuolewa.
Sangaine Mbekwa ni baba mzazi wa wa Lucia, anathibitisha kwamba tangu alipojiunga shuleni

hapo, mwanae huyo hakuwa na maendeleo mazuri ya kitaaluma.
“Shule ya Kambala haina walimu wa kufundisha watoto wetu, mimi nashangaa imewezekanaje
mwanangu kufaulu kwenda sekondari wakati hajui kusoma wala kuandika!” amesema
Sangaine.
Alipohojiwa kuhusu mbinu za wazazi kuwaozesha watoto wa kike kwa visingizio vya kutojua
kusoma wala kuandika, amesema hata kama zipo lakini si kwa mtoto wake huyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kambala, Emmanuel Ibrahim, anasema kwamba wanafunzi wanaofaulu
mtihani wa darasa la saba pasipo kujua kusoma wala kuandika, ni hali anayoilezea kwamba
inaustaajibisha umma hususani kijijini hapo.
“Watu wengi wanailalamikia mitihani inayotungwa siku hizi, kwamba inakuwa na majibu na
anachotakiwa kufanya mtoto ni kufuta mahali penye jibu sahihi…huoni hilo kama ni tatizo?”
alihoji Emmanuel.
Amesema suala la watoto kufaulu bila kujua kusoma wala kuandika linaweza kuchangiwa na
ukosefu wa walimu shuleni hapo.
Pia amesema utoro wa wanafunzi uliokithiri ni miongoni wa vyanzo vya wanafunzi kuhitimu
elimu ya msingi na pengine wakiwa hawajui kusoma ama kuandika.
Shule ya Msingi Kambala kwa mwaka jana ilikuwa na jumla ya wanafunzi 465 na walimu watatu
tu wanaofundisha shuleni hapo.
Shule ya hiyo inakabiliwa na uhaba wa walimu tangu mwaka 2016, baada ya mwalimu mmoja
kwenda masomoni na mwingine kustaafu baada ya muda wake wa kufanya kazi kuisha.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Kambala, Mbelwa Joseph, anasema wanajitahidi kadri
iwezekanavyo kuhakikisha watoto wanajua kusoma na kuandika, lakini wanakwamishwa na
mahudhurio mabaya yanayochangiwa na wanafunzi wengi kujihusisha na uchungaji wa
ng’ombe.
“Tuliwapima watoto wote waliofanya mtihani wa darasa la saba shuleni hapo …suala la mtoto
huyo kufaulu bila kujua kusoma wala kuandika haliwezekani,” amesema Mbelwa.
Hata hivyo, Mwalimu Mbelwa anakubali kuwapo changamoto ya watoto kutoyamudu masomo
ya darasani, hivyo wameanzisha utaratibu wa kuwakumbushia wanafunzi kuanzia darasa la
tano hadi la saba masomo ya kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).
Kwa mujibu wa tafiti za taasisi ya Hakielimu kwa mwaka 2012, jumla ya wanafunzi 5,200
walibainika kufaulu kujiunga kidato cha kwanza bila kujua kusoma wala kuandika.
Idadi hiyo iligundulika baada ya udanganyifu uliokuwa umejitokeza katika mtihani wa darasa la
saba na kusababisha wanafunzi 9,736 kufutiwa matokeo.
Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Elimu, Mafunzo na Ufundi waliamuru wanafunzi wote
wanaoripoti shuleni kwa kipindi hicho kupewa mtihani wa majaribio wa kupima uwezo wao wa
kusoma, kuandika na kuhesabu (KKK).
Kwa upande wa ripoti ya taasisi ya Uwezo ya mwaka 2015, asilimia 16 ya watoto wa darasa la
saba mwaka 2014 walihitimu bila kuwa na uwezo wa kusoma mafunzo ya hadithi rahisi ya
Kiswahili ya darasa la pili.
Ripoti hiyo ilionesha asilimia 23 ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba hawakuwa na uwezo
wa kufanya hesabu rahisi za kiwango cha darasa la pili.
Mwalimu Naghuhiwa Elisante ni Mratibu Elimu Kata ya Mkindo, amesema si rahisi kuwapo
mwanafunzi anayehitimu darasa la saba pasipo kujua kusoma ama kuandika, hasa katika shule
zilizopo katani humo.
Amesema hali hiyo ni kutokana na wanafunzi wanapofika darasa la sita hawaingii darasa la
saba pasipo kujua kusoma wala kuandika.
Elisante amesema muundo wa mitihani inayotungwa kwa kumwelekeza mwanafunzi kuchagua
jibu sahihi, unaweza kuchangia wanafunzi wengi kufaulu pasipo kujua kusoma ama kuandika.
Mwakilishi wa Ofisi ya Afisa Elimu wilayani Mvomero, Mwalimu Nimrodi Mahenge, amesema

“Sina uhakika kama kuna watoto hao, kwani kabla ya kufanya mtihani wa darasa la saba
wanafanyiwa majaribio.”
Pia ameongeza kuwa mwanafunzi ambaye hawezi kusoma na kuandika, hana uwezo wa kujaza
fomu ya kujaza namba za mtihani inayojazwa kabla ya mwanafunzi kufanya mtihani wa darasa
la saba.
Mahenge amesema suala la watoto kutokujua kusoma wala kuandika katika Wilaya ya
Mvomero, ni changamoto ambayo wameamua kuishughulikia kwa nguvu zote.
Amesema utafiti wao wa awali ulibainisha ili kuweza kuepukana na changamoto hiyo,
wanatakiwa kuihusisha jamii nzima ya Mvomero hasa wafugaji ambao hawana mwamko wa
elimu.
Mahenge amesema mradi wa tusome pamoja ambao umetambulishwa mkoani Morogoro,
utafanya vyema kwani umepunguza tatizo kama hilo lililokuwa likiusumbua Mkoa
wa Shinyanga.
“Shinyanga ni moja ya mikoa yenye historia ya kuwa na wanafunzi wasiojua kusoma wala
kuandika,” amesema.
Tusome Pamoja ni mradi unaodhaminiwa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani
(USAID) ukiwa na lengo la kuwawezesha kutumia mbinu bora katika utoaji wa elimu kwa shule
za msingi zilizo katika maeneo yasiyo na mwamko wa elimu.
Kwa mujibu wa Mahenge, moja ya matokeo ya mradi huo ni kuundwa kwa Ushirikiano wa
Wazazi na Walimu (UWAWA) unaoshughulikia uboreshaji mazingira katika sekta ya elimu ili
yamwezeshe mwanafunzi kufaulu.
Amesema ushirikiano huo unaolenga kubaini changamoto za mtoto mmoja mmoja kutoka kila
familia, utamwezesha mwalimu kutambua maeneo sahihi ya kumsaidia darasani.
Mahenge amesema katika kuboresha mazingira hayo, wanafunzi wa madarasa ya tano, sita na
saba wanalazimika kufundishwa kusoma na kuandika kwa kila somo wanalofundisha.
“Kutokana na watoto wengi kuonekana wanasumbuliwa na suala la KKK (Kuhesabu, Kusoma
na Kuandika), tumepitisha utaratibu wa kufundisha masomo haya hadi kwa madarasa ya juu
kwa kumtaka mwalimu ayagusie anapokuwa anafundisha masomo mengine kwa madarasa ya
tano, sita na saba,” amesema Mahenge.
Mdau wa masuala ya elimu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) (jina
linahifadhiwa), amesema kukosekana kwa ‘sauti ya pamoja’ kama Taifa kuhusu elimu ya msingi
ni chanzo cha matatizo yanayoikabili sekta hiyo.
Amesema Serikali ina sera ya kutokaririsha mtoto darasa, hivyo kinachofanyika ni kupitisha
watoto wa shule za msingi kujiunga sekondari hata kama hawana sifa.
John Nchimbi, Msemaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), amesema mtihani wa kuchagua jibu
sahihi hauchangii watoto kufaulu bila kujua kusoma wala kuandika, bali sababu nyingine
zinazopaswa kujulikana kwa kufanya utafiti.
Amesema karibU nchi zote za Afrika Magharibi zinatumia mtihani wa kuchagua katika mitihani
yao Ghana ikiwa kinara; iliyoanza kutumia mfumo huo tangu miaka ya 1960 na hawajapata
madhara yoyote.
Ameongeza kuwa lengo la kuanzisha mfumo huo ni kupata njia bora ya kutahini wanafunzi na si
vinginevyo.
Hali kama ilivyojionesha kwa Shule ya Msingi Kambala inaelezwa kuwapo kwa shule nyingine
wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro na pengine katika maeneo mengine ya nchi.
Hivyo ni wajibu wa Serikali na wadau wengine kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyo bora, ili
wanapohitimu wawe na uwezo ukiwamo wa kujua kusoma na kuandika.
mwisho