Na Charles Ndagulla, Moshi
Tegemeo la kutajirika kwa wakazi zaidi ya 20 katika halmashauri ya Wilaya ya Moshi Vijijini
kupitia mradi wa ufugaji wa sungura wa kisasa, limetoweka baada ya kuachwa na
wawezeshwaji wao, kampuni ya Rabbit Bilss Tanzania.
Viongozi wa kampuni hiyo iliyoanza kuhamasisha na kuwahudumia wakazi hao tangu mwaka
2016, hivi sasa hawawafikii wafugaji hao na sasa wafugaji sungura hao hawajui mahali pa
kupata huduma kama chakula, dawa na soko la mifugo hiyo.
Mmoja wa wafugaji hao, Christomoo Tenga, ameliambia JAMHURI kuwa baada ya hamasa na
uhakika waliyopewa na kampuni hiyo kuhusu biashara ya sungura, miongoni mwao walikopa
fedha kutoka taasisi tofauti hivyo kuwa katika hatari ya kufilisiwa ikiwa hali hiyo haitapata
utatuzi.
Amesema kampuni hiyo yenye makao yake eneo la Ngaramtoni mkoani Arusha,
iliwahamasisha kufuga sungura kwa makubaliano ya kwamba wangewanunua sungura
watakaozalishwa.
Tenga amesema kuwa hatua hiyo iliwahamasisha wananchi wengi na ‘kuchangamkia’ fursa
hiyo ikiwa ni pamoja na kukopa fedha wakiamini biashara hiyo itawalipa vizuri.
Kwa mujibu wa Tenga, kampuni hiyo iliwauzia sungura jike kwa shilingi 95,000 na dume
likithaminishwa kwa shilingi 45,000 wakati banda la kuwahifadhi liliuzwa kwa shilingi milioni
moja.
Hata hivyo, amedai kuwa tangu Julai mwaka jana, viongozi wa kampuni hiyo waliowaingiza
katika biashara ya sungura hawajaonekana, ingawa kabla ya kutoweka kwao, wapo waliowauza
pasipo kulipwa, akiwamo yeye anayedai shilingi 403,000.
“Walijitangaza kwenye vyombo vya habari, wakafanya semina za uelimishaji na kutuhakikishia
kuwa sungura mmoja anaweza kuzaa watoto sita hadi 10 na wanazaa mara tano kwa mwaka,
sasa wametuacha hatuna soko la mifugo hiyo,” amesema.
Tenga amesema maelezo ya kampuni hiyo yalidai sungura mmoja angezaa ‘vifaranga’ 40 kwa
mwaka na akitunzwa vizuri kwa muda wa miezi mitano, anaweza kuwa na uzito wa kati ya
kilogramu mbili na nusu hadi tatu huku kilo moja ikipangwa kununuliwa kwa shilingi 8,000.
Kutokana na mchanganuo huo, Tenga amesema kwa mfugaji aliyeanza na mtaji wa majike 10
alitarajia ‘kuvuna’ shilingi milioni nane kwa mwaka.
Mfugaji mwingine, Luid Jones, ameeleza kutumia mtaji wa shilingi milioni nne kuwekeza kwenye
mradi huo, baada ya kuhamasishwa na Rabbit Bilss Tanzania.
Amesema fedha hizo alikopa benki na kuzitumia kwa ujenzi wa mabanda pamoja na kununua
sungura kutoka kampuni hiyo waliofikia 200.
Hata hivyo, amesema ni takribani mwaka mmoja sasa sungura hao wamekosa soko baada ya
kutoweka kwa kampuni hiyo, hivyo kuiomba Serikali yenye kuwa na kumbukumbu zao isaidie
kuwapata ili haki itendeke na kuwadhibiti wawekezaji hasa wa kigeni wanaokiuka taratibu.
Amesema wafugaji wa sungura hao wanaingia gharama za kuwalisha, kuwatibu, mishahara na
posho kwa wanaowatunza na kwamba soko la uhakika ili kurejesha gharama hizo ni kupitia
ununuzi wa kampuni hiyo.
Amesema hivi sasa ana wasiwasi wa kutaifishwa kiwanja chake alichoweka dhamana benki, ili
kupata mkopo alioutumia kuingia katika biashara hiyo.
Dk Fabian Mosha, mmoja wa madaktari wa mifugo walioshiriki kutoa mafunzo ya ufugaji bora
wa sungura kwa wananchi hao, ameshindwa kuelezea hali hiyo kwa madai kwa undani kwa vile
ameacha kazi katika kampuni hiyo kwa miezi sita sasa.

Lakini amewashauri wafugaji hao kuwa na umoja na kudai haki yao kwa kutumia mikataba
waliyoingia na kampuni hiyo.
“Kama hawatakuwa na mikataba ya kisheria waliyoingia na kampuni hiyo, inaweza kuwa shida
kupata haki zao,’’ amesema.
Hata hivyo, JAMHURI halikuweza kupata ushirikiano kutoka kwa maofisa wa kampuni hiyo,
kwani simu ya mmoja wa maofisa hao aliyetajwa kwa jina la Rose Kurubone iliita bila majibu.
Baadaye ofisa huyo aliomba atumiwe ujumbe mfupi wa maandishi kwa kile alichodai yupo
kwenye kikao lakini hakujibu. Pia Kurubone alipigiwa simu na Mhariri wa Habari wa JAMHURI
lakini simu yake haikupokewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu yake
ya kiganjani hakujibu.
mwisho.

4092 Total Views 3 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!