* Uhamiaji yawagawia vibali kinyemela

* Wizi mifugo ya wazawa wakithiri, mazingira yaharibiwa

 

Wakati Serikali kupitia kwa Mkuu wa Operesheni Kimbunga, Simon Sirro, ikijigamba kufanikiwa katika kazi ya kuwakamata wahamiaji haramu na kuwarudisha kwao, JAMHURI imebaini kuwa wahamiaji wengi wanaishi na mifugo yao katika Pori la Akiba la Kimisi, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, huku wakikingiwa kifua na baadhi ya vigogo wa Idara ya Mifugo, na Uhamiaji wilayani hapa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili tangu operesheni hiyo ilipoanza, umebaini kuwa baadhi ya vigogo wa idara hizo waliigeuza kazi hiyo kuwa mradi wa kujineemesha kinyume cha lengo lililokusudiwa na Serikali, hali ambayo imesababisha kuwapo kwa migogoro isiyoisha baina ya wenyeji wa eneo hilo na wahamiaji haramu.

 

Migogoro hiyo ambayo chanzo chake ni baadhi ya vigogo wa Idara ya Uhamiaji kuwagawia kama njugu wahamiaji haramu vibali vya kuishi nchini kwa muda, ambao kwa kiburi cha vibali hivyo wameamua kuvamia na kujenga katika maeneo ya wazi yaliyotengwa na Serikali za Vijiji husika kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya umma.

 

Hali hiyo imesababisha viongozi wa vijiji husika kuishi kama wakimbizi, huku wakihofia kuuawa kwa kinachoelezwa kuwa Serikali wilayani Ngara imeziba masikio.

 

Tukio la hivi karibuni, ambalo linadaiwa kuchochewa na baadhi ya vigogo wa idara za Uhamiaji, na Mifugo waliowekwa mfukoni na kufanya watakavyo kinyume cha taratibu za nchi, ni la wafugaji wawili kuuawa kinyama kwa kukatwa kwa panga na kuchomwa mikuki na wananchi. Pia ng’ombe 12 waliuawa katika tukio hilo kijijini Kasulo.

 

Chanzo cha mauaji hayo kimeelezwa kuwa ni uhasama wa muda mrefu kati ya wananchi na wafugaji hao, wanaodaiwa kuingiza mifugo kijijini hapo bila ridhaa ya Serikali ya Kijiji, bali kwa mgongo wa vigogo wa idara za Uhamiaji, na Mifugo.

 

Waliouawa kwenye tukio hilo lililotokea Septemba 19, mwaka huu, saa 11:00 jioni ni Ngabo Godfrey (24) na mwingine ambaye hakutambulika mara moja na kwamba ng’ombe waliouawa kwa kuchomwa mikuki na kukatwa mapanga, nyama zao zilichukuliwa na wananchi hao kwa ajili ya kitoweo.

 

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngoma B, kijijini Kasulo, lilipotokea tukio hilo, Simon Nzakaya, aliieleza JAMHURI kuwa miili ya wafugaji hao ilipatikana siku moja baada ya mauaji na tayari watu wanane waliokuwa wakishikiliwa na vyombo vya dola kwa mahojiano zaidi.

 

Hata hivyo, baadhi ya watu walizitupia lawama baadhi ya mamlaka za Serikali zikiwamo Idara ya Uhamiaji, Mifugo na Halmashauri ya Wilaya kupitia Kitengo cha Sheria, kwa kushindwa kuchukua hatua mapema mara baada ya kuombwa kuingilia kati mambo ya uvamizi wa wafugaji katika eneo hilo.

 

“Mgogoro huu si wa leo… wenzetu Idara ya Uhamiaji, Mifugo na Mwanasheria wetu wa Halmashauri walishakuwa mawakala wa wafugaji na wahamiaji haramu… na ndiyo sababu za mauaji kama haya maana wananchi wameshachoka… na ninakueleza ndugu mwandishi huu ni mwanzo tu, iwapo Serikali haitazinduka ikasafisha idara hizi na kuleta wazalendo, mauaji hayatakoma maana wafugaji wanaoingia kinyemela kupitia mlango wa nyuma ni wengi,” amesema mmoja wa wanakijiji aliyeomba kutotajwa jina gazetini.

 

Gazeti hili, mbali ya kuzungumza na baadhi ya wananchi kwenye vitongoji vya Njiapanda na Ngoma B ilikofukuta migogoro hiyo na kuelezea kero wanazokumbana nazo kutoka kwa wafugaji na wahamiaji haramu inayosababishwa na kukithiri kwa rushwa, pia limefanya mahojiano na baadhi ya viongozi wa maeneo hayo wakatoa dukuduku zao.

 

Brighton Kemikimba, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Njiapanda, amesema tatizo la uingizaji wa mifugo kutoka ndani na nje ya nchi kuja kijijini hapo na maeneo mengine ndani ya Wilaya ya Ngara, limechangiwa kwa kiasi na idara ya Mifugo na ya Uhamiaji ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikiwapa wafugaji hao vibali kinyume cha sheria.

 

“Idara hizi mbili, hususan ya uhamiaji imesababisha maeneo tunayoishi kugeuzwa kambi za kufugia mifugo ya wahamiaji… maana wamekuwa wakifika kisha kujimilikisha maeneo ya kufugia na kuishi bila kufuata taratibu za umilikaji wa ardhi.

 

“Watu tukiwa hatuna hili wala lile tunashtukia wapo kijijini… kama viongozi tumeshafanya vikao vya kijiji, mikutano ya hadhara ya vijijji na kutoa maazimio hawa watu waondoke katika ardhi yetu na warudi walikotoka, lakini cha kushangaza wamekuwa wakikimbilia Uhamiaji na kupewa ‘pamiti’ kinyemela, jambo ambalo limezidisha migogoro kila uchao na hatujui la kufanya,” amesema Kemikimba.

 

Alifafanua; “Sheria ya Ardhi Namba 5 ya mwaka 1999 ya Vijiji inatoa mamlaka kwa Serikali ya Kijiji kuyajadili maombi ya watu wanaoomba kuhamia kijiji husika, na mkutano wa hadhara wa kijiji ndiyo hutoa mamlaka kwa wahusika kuishi eneo hilo, lakini hayo yote hayafanyiki, badala yake mamlaka za kijiji zimeporwa na Uhamiaji.”

 

Naye Silvester Katongale, mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kasulo, amesema malalamiko yao kuhusiana na Idara ya Uhamiaji kugawa vibali kwa wahamiaji ambao wamekuwa wakivamia maeneo yao bila kufuata taratibu, ni ya muda mrefu na kwamba hata Mkuu wa Wilaya aliyekuwapo, Luteni Kanali Nyakonji, alijaribu kufuatilia bila mafanikio.

 

“Huyu DC aliwahi kuagiza iundwe kamati ya kufanya sensa ya mifugo iliyoingizwa kinyemela ili ijulikane idadi yao, lengo likiwa kuangalia uwezo wa kijiji, lakini alikwama na hakuna kilichofanyika, badala yake wahamiaji na mifugo yao wanaendelea kuingia, yaani imekuwa vurugu kubwa kwani watu wenye asili ya Rwanda wamekuwa mbogo kana kwamba hii ni ardhi yao.

 

“Wizi wa mifugo ya wenyeji umetawala kutokana na wingi wa wafugaji wavamizi kuingia kila kukicha na pia kumejitokeza uharibifu mkubwa wa mazingira kwani hali ya mazingira ilivyokuwa awali na sasa ni tofauti na inavyoonekana, wilaya imeshindwa, hivyo tunamwomba Rais Jakaya Kikwete aingilie kati,” amesema Katongale.

 

Mwingine aliyeathiriwa na wimbi la wahamiaji kuvamia na kuweka makazi kijijini hapo kinyume cha taratibu, ni Dauda Yunusu, mjumbe wa Serikali ya Kijiji na Mjumbe wa Kamati ya Wafugaji na Ardhi katika Kijiji cha Kasulo.

 

Yunusu amesema; “Niliposikia Rais akitoa tamko la kuhakikisha wahamiaji haramu wanakamatwa na kurejeshwa kwao nilifarijika nikijua ndiyo mwisho wa migogoro hiyo, lakini cha ajabu zoezi [kazi] nzima lilihujumiwa na Idara ya Uhamiaji ambayo kwa makusudi iligeuza operesheni hiyo kuwa kitegauchumi kwa kuwagawia kinyemela wahamiaji vibali vya kuendelea kuishi nchini bila ridhaa ya kijiji husika.

 

“Unavyoniona ndugu mwandishi mimi, Brighton, na Afisa Tarafa ya Nyamiyaga, pamoja na Serikali ya Kijiji tumeshitakiwa mahakamani na Evarist David na Medadi Muhutu, ambaye ni asili ya Rwanda, lakini ana kibali cha kuishi nchini na kwenye kesi hiyo namba 35/2012 tunadaiwa milioni [shilingi] 17 na ukichunguza yote ni kwa kuwa tunapigania ardhi yetu, badala ya kuondoka wanatuburuza mahakamani, hii ndiyo Serikali tunayoitumikia kwani hata halmashauri imetutelekeza kupitia mwanasheria wake,” ameongeza.

 

Yunusu amekwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa usimamizi mbovu wa sheria ndiyo chanzo cha matatizo waliyonayo, kwani pamoja na Rais Kikwete kutoa tamko la kuwaondoa wahamiaji haramu na mifugo yao, watu wanaolisha mifugo katika misitu ya hifadhi ukiwamo wa Kimisi hawakuondolewa, badala yake walipatiwa vibali vya kuendelea kuishi humo.

 

Amedai pia kwamba wahamiaji haramu waliokamatwa katika Msitu wa Kimisi na ardhi ya Kasulo na kuonekana hawana vigezo vya kuishi nchini walirudishwa nchini kwao, lakini cha kushangaza mifugo yao ilibaki nchini pamoja na wafanyakazi wao wanaolisha mifugo.

 

Baadhi ya wahamiaji haramu waliorudishwa kwao wakiacha mifugo na wafanyakazi wao kwenye ardhi ya Tanzania katika Kijiji cha Kasulo ni Benoni Mnyechwi, Kadugala, Katubu na watoto wa ndugu wa mzee Bulalisi wameondoka huku mifugo yao ikiendelea kubaki yalipo makazi yao katika Kitongoji cha Kamuri katika Kijiji cha Kasubo, jambo linaloashiria watarudi nchini.

 

Ameiomba Serikali ifanye jitihada za kunusuru hali hiyo, kutokana na ukweli kuwa operesheni imefanyika ndivyo sivyo kinyume cha matarajio ya Rais Jakaya Kikwete, hasa ikizingatiwa kuwa bado kuna wahamiaji wanaoishi katika Msitu wa Hifadhi Kimisi wakiwa na mifugo yao.

 

“Serikali iingilie kati hawa watu waondolewe katika Msitu wa Kimisi na waliohodhi ardhi ya wazawa kinyemela kwa kisingizio cha kuwa na vibali walivyopata kinyemela waachie ardhi ya watu, vinginevyo yanaweza kutokea machafuko au mauaji kama yaliyotokea ya wafugaji na mifugo yao kuuawa kinyama.

 

“Na hili si la kufanywa tena na Serikali ya Ngara maana imeshindwa kudhibiti mianya ya rushwa, iundwe tume kuchunguza na kunusuru hali hii maana Uhamiaji wamekuwa wakitoa vibali vinavyowaruhusu kuishi nchini kwa muda, jambo ambalo limewafanya wananchi kukosa imani na idara hiyo,” amesema.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasulo, Yusuph Katula, akifafanua utaratibu wa kuomba vibali vya kuishi nchini kwa muda, amesema kwa kawaida mwombaji wa kibali cha kuishi eneo husika anapaswa ajadiliwe na kijiji baada ya kupeleka maombi kwenye Halmashauri ya Kijiji na si vinginevyo.

 

“Kijiji kinapomjadili na kumkubali wanampa muhtasari wa kikao kile ili apeleke Uhamiaji Wilaya, ambao nao hupeleka mkoani ambako hutoa ‘pamiti’ na huo ndiyo utaratibu tofauti na sasa, kwani Uhamiaji wanatoa vibali hivyo kama njugu na kuzidisha migogoro isiyo ya lazima kwani wahamiaji wa kijiji chetu hawakupata vibali walivyonavyo kwa kufuata utaratibu, wamevipata kwa njia ya panya, rushwa imetawala,” amesema.

 

Kutokana na hali hiyo, viongozi waliokuwa wakiongoza zoezi hilo [Operesheni Kimbunga] hawakuhusishwa kwenye uamuzi ili kujiridhisha na vielelezo vya wahamiaji haramu kwa aliye halali kuishi na asiye halali, badala yake wengi wa wahamiaji haramu waliachwa na Polisi wakishirikiana na Uhamiaji na hata walipohoji walitishiwa maisha na hadi sasa wanaishi kwa kuhofia usalama wao.

 

Akinukuu kumbukumbu za Serkali ya kijiji, alidai kuwa Aprili 24, mwaka jana, Serkali ya kijiji ilitoa orodha ya wafugaji wanaodaiwa kuvamia kijijini hapo, wakiingia na maelfu ya mifugo yao wakiwataka kuondoka na kuomba msaada kutoka mamlaka husika kwa maandishi kuwaondoa, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.

 

Ameongeza kuwa Desemba 12, mwaka jana, pia uongozi  wa wilaya ulijulishwa kwa taarifa ya kumtaka mfugaji mwingine kuingia kijijini hapo kwa nguvu naye kuondoka Desemba 28, kulitolewa taarifa kama hiyo, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa hadi sasa.

 

Diwani wa Kata ya Kasulo inayodaiwa kuongoza kwa kuathiriwa zaidi na wimbi la ufugaji usio na tija na wahamiaji wenye vibali pamoja na wale wanaotoka wilaya jirani na mikoa, wangeweza kudhibitiwa kama mamlaka za wilaya na mkoa zingeweza kuingilia katika kukisaidia kijiji mapema kabla ya hali hiyo kujitokeza.

 

Ameongeza kuwa hatua ya Idara ya Uhamiaji kutoa vibali kwa wahamiaji kutoka nchi jirani na kutumia vibali hivyo kuingiza maelfu ya mifugo katika kata hiyo na katika hifadhi za Kimisi, Biharamulo na Burigi kumekuwa chanzo cha mgogoro huo.

 

Ameongeza kuwa ukiondoa wafugaji kutoka wilaya na mikoa jirani wanaolalamikiwa kuingia kinyemela, wengi wanaolalamikiwa ni wahamiaji wanaoingia na mifugo yao ama baada ya kupata vibali, au uraia na kisha kuingiza mifugo yao bila ridhaa ya kiijiji.

 

Amesema kinachoonekana ni kwa baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waadilifu kutanguliza zaidi maslahi yao binafsi kunakotokana na mgogoro huo badala ya kuupatia ufumbuzi kwa maslahi ya wananchi, wilaya na Taifa.

 

Diwani Kiiiza amedai kuwa suala hilo siyo siri, kila kiongozi na wananchi wanatambua kuwa Idara ya Uhamiaji kupitia vibali inavyovitoa ndivyo vimekuwa vinatumiwa na wahamiaji hao kama kigezo cha kuingia na maelfu ya mifugo yao bila kuomba kuingia kijijini, wakitumia ubabe huku kukiwapo tetesi za kukingikiwa kifua.

 

Katika hatua nyingine, Idara ya Mifugo Wilaya imekuwa haichukui hatua hata inapojulishwa juu ya kuwapo uingizwaji wa mifugo kutoka nchi jirani au wilaya na mikoa jirani, badala ya kuchukua hatua yenyewe hubariki na hivyo wanakijiji kupitia Serikali za kijiji kugeuka yatima.

 

Mkuu wa Wilaya ya Ngara,  Costantine Kanyasu, ambaye amekiri kuikuta baadhi ya migogoro hiyo, alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusiana na malalamiko ya zoezi la kukamata na kuwarudisha kwao wahamiaji haramu kutawaliwa na rushwa, amekana Uhamiaji kugeuza zoezi hilo kuwa kitegauchumi chao huku akiahidi kufuatilia ili kubaini ukweli halisi.

 

Aidha, amekiri kupokea baadhi ya malalamiko, ingawa hata hivyo, amedai yalikuwa yakielekezwa kwa mamlaka nyingine kwa hatua na ofisi yake kupewa nakala kutoka kijijini hapo, na sasa atakachokifanya ni kuchukua hatua za haraka kuhakikisha tukio kama hilo halitokei tena.

 

Kanyasu aliyehamia wilayani hapa hivi karibuni, amekiri kuwapo kwa baathi ya changamoto zinazotolewa na wananchi, lakini zikiwamo za baadhi ya mamlaka kulalamikiwa kutowajibika juu ya tukio la mauaji. Uchunguzi wake unaendelelea.

By Jamhuri