Wahamiaji haramu waivamia Tanzania

*Wakongo, Wanigeria waongoza, wahusishwa wizi wa fedha benki, uuzaji dawa za kulevya

Wimbi la wahamiaji haramu linazidi kuitesa nchi, ambapo sasa raia wa Congo na Nigeria ndio wanaongoza kwa uhalifu huo.

Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Hokororo, ameithibitishia JAMHURI wiki iliyopita, akisema jitihada zaidi zinahitajika kukabili tatizo hilo.

“Tatizo hili ni kubwa, kwa mfano, kati ya Mei 4 hadi 9, mwaka huu tumewakamata wahamiaji haramu 48 hapa Dar es Salaam kutoka mataifa mbalimbali, na wengi wao ni kutoka Congo na Nigeria,” amesema Garace.

Kwa mujibu wa Afisa Uhamiaji huyo, kati ya wahamiaji haramu hao, 20 ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Nigeria (7), Burundi (3), Zimbabwe (3), Malawi (2), na mmoja mmoja kutoka nchi za Japan, China, Marekani, Somalia na Afrika ya Kati.

Pia Watanzania wawili walikamatwa katika msako huo wakituhumiwa kuwapokea na kuwahifadhi katika makazi yao raia wa kigeni kinyume cha taratibu na sheria za nchi.

“Mtanzania unapompokea mgeni na kuishi naye nyumbani kwako hapa nchini kinyume cha sheria lazima tukukamate kwa kosa la kuhifadhi wahamia haramu,” amesema Grace.

Ameeleza kuwa kabla ya kuwakamata hao 48, ofisi yake ilikuwa imewakamata wahamiaji haramu 42 kati ya Aprili 29 na Mei 3, mwaka huu jijini Dar es Salaam.

“Ukiwahoji hawa wahamiaji haramu wanakwambia wamekuja kutafuta maisha hapa Tanzania na wengine utakuta waliingia kihalali, lakini muda wao ulipoisha hawakutoka, wakaendelea kuishi nchini,” amesema.

Baadhi ya wahamiaji haramu hao, kwa mujibu wa Grace, wameshafikishwa mahakamani na wengine wametozwa faini ya dola 600 za Marekani (karibu Sh milioni moja za Tanzania) kila mmoja.

Uchunguzi wa Idara ya Uhamiaji umebaini kwamba baadhi ya wahamiaji haramu siku hizi wanakwepa kufikia kwenye nyumba za kulala wageni, badala yake wanapanga nyumba za kuishi jijini Dar es Salaam.

Inaelezwa kwamba baadhi ya Watanzania wamekuwa wakiwahifadhi na kuwakingia kifua wahamiaji haramu ambao huwalipa fedha nyingi.

Habari zinasema wahamiaji wengi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu ukiwamo wizi wa fedha benki na uuzaji wa dawa za kulevya hapa nchini.

Vyanzo vya habari vinasema baadhi ya wanawake Watanzania wamejenga uhusiano na wahamiaji haramu ambao huwalipa ujira mnono kwa ajili ya kuwasaidia kupata mianya ya kufanya vitendo vya uhalifu nchini.

Kwa mujibu wa habari hizo, baadhi ya wahamiaji haramu wamefanikiwa kununua viwanja na kujenga nyumba za kifahari, huku wengine wakiendesha biashara kubwa katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Idara ya Uhamiaji inaendelea kuwahimiza wananchi kujenga uzalendo kwa nchi yao na kuhakikisha wanawafichua wahamiaji haramu katika maeneo yao ili wachukuliwe hatua za kisheria.

“Tunawaomba wananchi watusaidie, taifa litafilisika, maana wahamiaji haramu na mambo yao ni haramu siku zote, hata biashara wanazofanya hazilipiwi kodi, wataifilisi nchi yetu,” alisema Grace.

Naibu Kamishna wa Uhamiaji (Upelelezi) Mkoa wa Dar es Salaam, Silvanus Mwakasekele, ametoa wito kwa raia wa kigeni wanaoishi na wenye nia ya kuingia na kuishi nchini kinyume cha sheria kujiepusha na uhalifu huo ili kuepuka kukumbwa na rungu la dola.

Hata hivyo, Idara ya Uhamiaji mkoani Dar es Salaam itaendelea kupata ugumu wa kukabili tatizo la wahamiaji haramu kama haitaboreshewa mazingira ya utendaji kazi ikiwa ni pamoja na kuongezewa magari kwa ajili ya shughuli za kuwasaka wahalifu hao.