Waislamu wachinje, sisi tule nguruwe wetu

Wiki iliyopita niliandika makala juu ya usaliti wa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwa yeye kuamua kuulisha umma uongo uliozaa madhara ya hali ya juu kwa wananchi wa Mtwara. Sitarudia nilichokiandika, ila niwashukuru wananchi na hasa wewe msomaji kwa mrejesho.

Nimepokea simu nyingi, ujumbe na barua pepe pengine kuliko wakati wowote tangu tuanzishe gazeti hili. Nawashukuru mno wasomaji kwa kueleza hisia zenu. Sitaweza kufafanua kila mmoja alisema nini, ila niseme karibu asilimia 95 ya waliowasiliana na mimi walinipongeza.

 

Sitanii, walinipongeza kwa kuamua kumfunga paka kengele. Hawakutarajia iwapo ningethubutu kumwambia Zitto kuwa katika hili hapana. Katika masuala ya nchi, siasa tuziweke kando. Alinichekesha msomaji mmoja aliyeniandikia hivi: “Kaka wengine wanatuchochea tupigane vita maana wanajua mambo yakiharibika kwetu watarudi kwao.”

 

Usiniulize ni nani mwenye uraia wa nchi mbili, ambaye hana uchungu na nchi yetu kiasi cha kutuchochea tupigane kisha arejee kwao. Ninalosema, gesi itunufaishe sote kama Watanzania. Nimemsikia Zitto ameanza tena uchochezi akidai Kigoma kuna mafuta, ila waelezwe watabaki na nini.


Sitanii, kichwa cha makala haya, kinasema: Waislamu wachinje, sisi tule nguruwe wetu. Nimelazimika kuandika makala haya baada ya kubaini sura ile ile ya upotoshaji katika jamii yetu. Mwanza kumeibuka kundi la watu wanaojiita Wakristo kuliko Waroma.

 

Kundi hili linashinikiza na kuhamasisha utengano katika jamii. Kundi hili limepeleka malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndekillo, likidai Wakristo waruhusiwe kuchinja. Waziri wa Uhusiano wa Jamii, Stephen Wasira, amefika pale akajaribu kusuluhisha mgogoro huu, inaelekea ameshindwa.

 

Nikisoma katika mitandao naona wakubwa huko Mwanza wameanzisha hadi bucha zao. Wanachinja wenyewe na kuwauzia Wakristo wenzao. Nimejaribu kufuatilia chimbuko la mgogoro huu. Wanasema Waislamu wanawadharau kwa kula nguruwe.


Eti Waislamu wanataka hata maduka ya nguruwe yaliyopo katika mitaa yao yavunjwe kuepusha kukwaza imani yao. Hapo ndipo ninapopingana na Waislamu sawa na nilivyopingana na Wakristo. Katika utawala wa Awamu ya Pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi, nchi yetu ilipata mgogoro kama huu.  Mzee Mwinyi alimaliza tatizo hili kwa busara ya hali ya juu.

Alisema anayetaka kula nguruwe ruksa, anayetaka kutoila ruksa. Huu ndiyo uhuru tunaoutaka Watanzania. Tusiingiliane katika imani. Nasema kwa muda mrefu na kwa mazoea siku zote, Waislmu ndiyo wanaokuwa wanachinja katika jamii yetu. Ingawa hakuna sheria ya kuruhusu hilo, nadhani ni utamaduni mzuri uliozoeleka.

 

Tuwaache Waislamu waendelee kuchinja, japo fursa hii isiambatane na kejeli dhidi ya dini nyingine, hasa matumizi ya neno KAFIRI. Neno hili lina ukakasi hapa nchini. Ikiwa tuna nia njema tujiepushe nalo. Tusilitumie.


Lakini pia kama ilivyozoeleka kuwa Waislamu ndiyo wachinjaji, na Waislamu pia wamezoea kuwa Wakristo na dini nyingine wanakula nguruwe. Ingawa hakuna sheria inayoruhusu au kuzuia ulaji wa nguruwe, basi tuuchukulie kuwa huu ni utamaduni unaowapendeza wanaokula mnyama huyu.


Tukishakubali misimamo na kuheshimu imani ya kila mtu, bila kutaka kulazimisha imani zetu ndizo ziwe juu ya imani za wengine, basi tutaishi kwa amani. Hata hivyo, tukijisahau na kudhani tunayo mamlaka dhidi ya imani nyingine tutajuta mbele ya safari.

 

Serikali nayo kwa upande wake isiruhusu vitu vya aina hii kutokea. Ikiwaacha wananchi wakaanzisha vurugu hizi zisizo na msingi, nchi itatumbukia kwenye vurugu zisizo za lazima. Ni lazima Serikali isimame imara kudhibiti matukio ya aina hii.

 

Mwisho nasisitiza; Waislamu wachinje, sisi tule nguruwe wetu.