Wakazi wa Kitongoji cha Mkulila, Kijiji cha Wambishe wilayani Mbeya, wamekataa mradi wa umwagiliaji maji waliopelekewa na Serikali, wakidai hawakushirikishwa katika uanzishwaji wake.

Lakini pia, wananchi hao wamesema hawaoni faida ya kuwa na mradi huo kwa sasa katika kitongoji hicho. Mradi walioukataa wananchi hao umeigharimu Serikali Sh milioni 40.

 

Wananchi hao wamesema wanaridhika na huduma ya maji wanayoipata kwenye mfereji kwa kipindi chote cha mwaka.


Hayo yamebainika katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na ofisi ya wilaya, kuwaelimisha wananchi hao faida ya mradi huo. Hata hivyo, pamoja na kuelimishwa, wananchi hao wameupinga mradi huo huku wakitaka fedha za mradi huo zielekezwe katika mradi mwingine.

 

Maofisa umwagiliaji kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Malonga Msuya na John Kajange, walijikuta katika wakati mgumu kutokana na mwitikio hafifu wa wananchi hao.

 

Diwani wa Kata ya Ulenje, Noel Mwankwale, amewasihi wananchi hao kuwa wasikivu na kuukubali mradi huo, ingawa naye juhudi zake hizo ziligonga ukuta baada ya wakazi hao kuendelea kusisitiza msimamo wa kuukataa.

 

Kwa mujibu wa wananchi hao, Sh milioni 40 ni nyingi na kwamba haziwezi kutumika kugharimia ujenzi wa mfereji usio na tatizo.

Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Michael Mwaifwani, amesisitiza kuwa mfereji unaokusudiwa kukarabatiwa hauna tatizo lolote.

 

Christian Matengere, mkazi wa eneo hilo, naye ameitaka Serikali kujenga utamaduni wa kupata maoni ya wananchi kuhusu miradi wanayoipa kipaumbele cha kwanza. Mkutano huo uliahirishwa bila pande zote kufikia mwafaka wa suala hilo.

By Jamhuri