Uchaguzi Mkuu wa Kenya ulimalizika jana kwa utulivu na amani, licha ya kuwapo kwa dosari ndogondogo, ikilinganishwa na wa mwaka 2007. Watu wengi duniani wameshuhudia na kusikia jinsi wananchi walivyojitokeza kwa wingi, kutumia haki yao ya kikatiba na kidemokrasia kuchagua viongozi watakaowaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Jumla ya wagombea tisa walijitokeza katika kinyang’anyiro cha urais, na ni ukweli usiopingika kuwa ushindani mkubwa ulikuwa baina ya wagombea wawili – Raila Odinga na Uhuru Kenyatta. Ni matumaini yetu kwamba Wakenya wamejiandaa kupokea matokeo ya uchaguzi huo na kuyakubali, tofauti na mwaka 2007. Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia leo, ingawa ya awali yanaonesha Raila Odinga ameibuka mshindi.


Uchaguzi ni sawa na mpira wa miguu. Kuna kushinda na kushindwa japo hakuna sare katika siasa. Wakenya wanatakiwa kuwa tayari kupokea matokeo yatakayotangazwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka.


Vurugu zilizotokea nchini Kenya mwaka 2007 kwa baadhi ya wanasiasa kukataa matokeo na kuzaa vifo vya watu wapatao 1,500 huku zaidi ya watu 10,000 wakikimbia makazi yao, hazina tija. Tumeshuhudia kampeni za kistaarabu mwaka huu kwa Kenya. Tunawapongeza wagombea wote kwa kukataa kuhubiri ukabila na ubaguzi wa kila aina.


Sisi JAMHURI tunawapongeza Wakenya kwa kushiriki uchaguzi huo kwa amani na utulivu, lakini pia tunahimiza kuheshimu na kupokea matokeo ya kushinda na kushindwa kwa amani. Hiyo ndiyo demokrasia.


Pia tunapenda kuvikumbusha vyombo vya dola vya Kenya, kuhakikisha vinatumia busara ya hali ya juu wakati wa kutekeleza jukumu lake la kulinda usalama wa raia na mali zao, katika kipindi hiki matokeo ya Uchaguzi Mkuu yanapotangazwa.


Watanzania tunapenda kuona jirani zetu Wakenya wanahitimisha Uchaguzi Mkuu kwa amani na kuwapa ushirikiano viongozi waliochaguliwa. Amani ni msingi wa maendeleo ya jamii.  Wakenya itunzeni.


1026 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!