Siku  chache  baada  ya  maofisa wanaoendesha  Operesheni Okoa Mazingira iliyofanyika katika Kijiji  cha  Usinge wilayani Kaliua, kutuhumiwa kumuua, Kipara Issa (39), kwa tuhuma za kumiliki silaha kinyume na sheria, baadhi ya wanaume katika kijiji hicho wamelazimika kuzikimbia familia zao kwa hofu ya kukamatwa na maofisa hao.

Hatua iliyochukuliwa na wakazi hao wa Kijiji cha Usinge inatokana kuwapo kwa taarifa ya kuwa kuna orodha ya majina imepelekwa katika kikosi kazi kinachofanya operesheni hiyo na wanatafutwa na kikosi hicho.

Kikosi kazi hicho kinachoundwa na maofisa kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa  na  Maofisa  Maliasili na kuanza operesheni hizo Oktoba mwaka huu, kinawasaka watu wanaojihusisha na uwindaji haramu.

Kikosi hicho kinatuhumiwa kufanya ukatili kwa watu wanaotajwa kuhusika na ujangili. Imebainika kuwa wapo baadhi yao wamepata mateso hayo na kuathiri afya  zao.

Mzee maarufu katika Kijiji  cha  Usinge, John  Kijiko (65), naye anadaiwa kupigwa na kujeruhiwa vibaya  na maofisa hao, jambo lililofanya alazwe katika  Zahanati  ya  Usinge kutokana na kujeruhiwa  vibaya.

Mwingine aliyekutwa na kadhia hiyo ni Ishize Kimbunga (39), ayejeruhiwa vibaya kutokana na mateso makali aliyoyapata na hata kusababisha maumivu katika sehemu ya haja ndogo na kubwa.

Wanaume wakimbia makazi yao

Kutokana na hali hiyo, wakazi wa kijiji hicho ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini kwa sababu ya usalama wao, kwa nyakato tofauti waliiambia JAMHURI kuwa sasa wanaishi kwa hofu.

Hatua hiyo imewafanya wayakimbie makazi yao na kutelekeza familia zao kwa hofu ya kukamatwa na kuteswa.

 

Lusoleka  Daudi ni mmoja wa watu wanaotajwa katika orodha ya watuhumiwa wanaotafutwa na kikosi kazi hicho, ametoweka nyumbani kwake. Familia yake imeingia hofu ya kuwa huenda naye ameuawa.

Katika orodha hiyo yumo Ndiku Yaleli ambaye kwa muda mrefu yupo Jiji Dar es Salaam akimuuguza dada yake aliyelazwa katika Hospitali  ya Taifa  ya Muhimbili (MNH).

 

Wanakijiji cha Kijiji cha Usinge wanaituhumu orodha hiyo kuwa si sahihi kwani majina mengine yameingizwa kutokana na watu kuwa chuki na  majungu.

Hata  hivyo,  baadhi  ya  watu  wakiwamo  wanawake ambao waume zao wamelazimika kukimbia kijijini hapo wameyaomba mashirika yanayotetea haki za binadamu kuingilia  kati.

Wamesema wanashindwa kuishi kwa amani kutokana na operesheni hiyo ambayo wamedai kuwa kwa sasa inaendeshwa kwa maslahi ya watu binafsi kinyume na malengo yaliyopangwa.

“Yaani huwezi kuamini mimi mume wangu alikamatwa na kupigwa sana, tumefuatilia kumtoa mikononi kwa hao watu maliasili walitaka tuwape shilingi milioni mbili lakini tukawalilia hali kwa muda mrefu tukawapatia laki tano, wenzetu nao wamemtoa ndugu yao kwa shilingi laki nne na elfu sitini,” amesema mmoja wa wanawake walihojiwa na gazeti hili.

Hata hivyo, mwanamke huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini amelalamikia hatua hiyo ya kutoa rushwa, kwani imesababisha familia yake ishindwe kupata mlo kutokana na kukosa fedha.

Amesema walipata fedha hiyo baada ya kuuza mahindi waliyokuwa wamehifadhi.


“Sisi  ndugu  yetu  tumemtoa  kwa  shilingi  milioni  tatu  na hivi  sasa  bado  hali  yake  si ya kuridhisha,  analalamikia  zaidi maumivu  ya  kifua, mgongo, kiuno na miguu lakini  baya  zaidi  alikuwa akijisaidia haja ndogo iliyochanganyikana  na damu kidogo,” amesema  mmoja  wa  wanafamilia ya  kati  ya  watu  waliojeruhiwa  katika  operesheni  hiyo.

Mkazi mwingine aliyekumbwa na operesheni hiyo ni Mzee Lameck Mbonye (62) aliyekamatwa baada ya kusalimisha bunduki aina ya gbore. Hata hivyo hadi  sasa  familia  yake  hajui Mzee Mbonye alipohifadhiwa.

Hata hivyo, baadhi ya watu waliokamatwa na kupigwa katika  operesheni hiyo na  baadaye  kutozwa  fedha  ili  waachiwe  huru  kutokana na mazingira ya woga wamekuwa wakiridhika kutoa kiasi cha fedha wanazoombwa huku wakiona  kuwa  ni  haki  yao  kutoa  fedha  na  pengine  kuona  kana  kwamba  kufanya  hivyo  ni  kama  kusaidiwa  na  maafisa  wa  operesheni  hiyo  ili  waachiwe  huru.

Familia ya marehemu Kipara Issa yaingiwa na hofu

Kutokana na mauaji Kipara Issa (39) mkazi wa Usinge  familia  iliyoachwa na  marehemu  huyo   imeingiwa  na  sintofahamu  na  kukumbwa na  hofu  kubwa  dhidi  ya  wanajeshi  wanaoendelea  kupitapita  katika  Kijiji  hicho  cha Usinge.


Akizungumza  na  gazeti  hili,  mama  wa  marehemu  Kipara Issa, Magreth  Kajoro  amesema  licha  ya  kutopatikana  kwa taarifa  yoyote kutoka  Jeshi  la Polisi  inayohusu  uchunguzi  na  ufuatiliaji  wa  kifo  cha mwanaye,  kinachowatia hofu zaidi ni kuwapo kwa taarifa kuwa maofisa hao wanataka kupoteza ushahidi katika kesi hiyo.

“Kwa kweli Serikali  ingejaribu  kufuatilia  jambo  hili  maana  bado  hali  inatisha  sana, hapa  kwetu, mbali na mauaji waliyoyafanya na  sisi  wengine  kupigwa, lakini  bado  wanahitaji  kuwakamata  wengine  wawili  sijui  na  wao  wanataka wakawaue vilevile kama walivyofanya kwa Kipara?” amesema  Magreth.


Amesema wanaofuatiliwa kwa ajili ya kukamatwa na maofisa hao ni wanafamilia  wawili — Magwese  Yusuph (32) na  Gayi Said (41) — wote wafanyabiashara wa duka la  vifaa vya  baiskeli na  wakulima  wa  tumbaku  katika hicho.

RPC  Tabora

Alipoulizwa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna  Msaidizi (ACP), Peter Ouma, hatua zilizochukuliwa kuhusu mauaji ya Kipara Issa, pamoja na  kujeruhiwa  kwa  mke  wake, Tabu, alisema kwa sasa hana  uwezo  wa  kulisemea  hilo.

Amesema operesheni  hiyo ina wasemaji  wake  wakuu  licha  ya  kuwa  wapo  watu wanaendelea  kufanyiwa  yale  ambayo  wanalalamikia   yanatendeka  kinyume  na  haki  za  binaadamu.

 

“Nimekwambia  mimi  kwa sasa siwezi kuongelea hilo naomba kama una jambo jingine niulize nitakujibu lakini kwa hilo siwezi,” amesema Kamanda  Ouma.

Hata hivyo, aliiambia JAMHURI kuwa  atatoa maelezo  ya  kina  na msimamo  wa  Jeshi  la  Polisi, baada ya timu ya uchunguzi aliyoiagiza kukamilisha upelelezi wa tukio hilo.

Kauli hiyo ya Kamanda Ouma imechukua sura mpya na kuacha maswali mengi yasiyo na majibu kwa wakazi wa Usinge.

Malalamiko ya wananchi

Siku  chache  baada  ya  Kamati  ya Ulinzi  na Usalama Mkoa  wa  Tabora  kufika  Kijiji  cha  Usinge  kufuatilia  tukio la  mauaji  ya  Kipara  Issa  na kudhalilishwa kwa familia yake, Kamati hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa, ilipata fursa ya  kusikiliza malalamiko ya wananchi dhidi ya maofisa wa  operesheni  hiyo.

Mambo yaliyobainika katika operesheni hiyo ni kuwa nguvu nyingi ilitumika  visivyo halali, hivyo kamati iliahidi kuifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwakamata maofisa waliotenda ukatili huo uliosababisha  mauaji.

 

Ahadi hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa iliwajengea matumaini wananchi wa Usinge. Hata hivyo, baada ya kuondoka kwa kamati hiyo wananchi hao walishangaa kusikia kwenye kituo kimoja cha televisheni hapa nchini kikitangaza kuwa robo tatu ya wakazi wa Usinge ni wahamiaji haramu.

 

“Ndugu  mwandishi  badala  ya  sisi  kuoneshwa jambo kubwa kama hili la mauaji ya  wenzetu  hapa  kijijini  na  kero  tulizomwambia  mkuu  wa  mkoa, leo  hii  tunashangaa  kuziona picha  zetu  halafu  wanasema  eti  sisi ni  wahamiaji  haramu, kama  ni  hivyo basi  waje watuue tu ijulikane moja maana hatua sehemu ya kupeleka malalamiko  yetu,” amesema mkazi wa kijiji hicho, Samson Michael, na kuongeza:

 

“Mimi  nahisi  hata  wewe  mwandishi  ni  yale yale  si  ajabu  hata  haya  tuliyokwambia  yataishia  hapo hapo  kwenye  kalamu  na  hiki  kinasa sauti  chako, jamani hivi ninyi mkikaa  kimya  mnatufikiria  nini  sisi  walalahoi, au  na wewe utaendea chako halafu ukae  kimya?” Samson alisisitiza.

Hata hivyo baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Usinge wamepoteza  matumaini ya kurejea kwa hali ya utulivu na amani licha ya kuwa Serikali ya Mkoa wa Tabora kuwaahidi kuwa hakuna tukio jingine litakalojitokeza.

Hata hivyo, kamata kamata bado inaendelea kutokea kwa baadhi ya watu wa kijiji hicho na maeneo jirani, na hata wengine kufanya wakimbie familia zao.


By Jamhuri