Wiki iliyopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilimpata rais mpya, Jamal Malinzi, anayechukua mikoba ya aliyekuwa Rais wa Shirikisho hilo, Leodegar Tenga, aliyeongoza kwa kipindi cha miaka ninane mfululizo.

Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Malinzi amesema kuwa anatarajia kuongoza kwa kuzingatia misingi yote ya uongozi pasipo na upendeleo wa aina yoyote.

 

Malinzi amesema kwamba mikakati yake ni kuhakikisha kuwa soka la Tanzania linasonga mbele zaidi ya pale ulipofikia uongozi uliopita.

Amesema kuwa pamoja na kuwa yeye aliwahi kuwa kiongozi ya ngazi za juu wa Yanga, anatarajia kuweka pembeni mapenzi yake na klabu hiyo na hivyo kuhakikisha anaongoza soka katika misingi ya haki sawa kwa kila mdau wa soka.

“Kwa sasa hivi kila mdau wa soka awe na amani sina timu nataka watu wacheze mpira, siku nikimaliza urais nitarudi tena Yanga,” amesisitiza Malinzi aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga kati ya mwaka 1999 na 2005.

Moja ya mikakati aliyonayo Malinzi ni kuwekeza zaidi katika soka la vijana wadogo, kuwa na mashindano ya vijana wenye umri tofauti katika ngazi mbalimbali hapa nchini.

Amesema kuwa kwa sasa kuna mipango ya muda mrefu na ile ya muda mfupi.

Kwa upande wa mipango ya muda mfupi, Malinzi amesema kuwa italenga mashindano yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

“Kwa sasa lazima tukubali kwamba hatuwezi kuacha mashindano yakapita, mfano tuna mashindano ya U-20 ya dunia, tuna Chalenji, haya tutashiriki chini ya ile programu ya muda mfupi,” amesema Malinzi.

Amesema kwa sasa ana wazo la kuunda jopo la makocha kutoka baadhi ya timu zinazoshiriki Ligi Kuu na hata wengine, ambao wana uzoefu ili kutoa mchango wao wa mawazo utakaozingatia utaalamu zaidi jinsi ya kuboresha Timu ta Taifa.

“Bado nina imani kwamba kuna makocha wengi tu ambao wana uzoefu, kwa hiyo wakitumiwa vizuri wanaweza kusaidia kuboresha timu yetu ya Taifa,” amesisitiza.

Amesema kuwa kuna haja ya kuwa na programu endelevu ambayo ina malengo yanayopimika na kuongezea kwamba utaratibu huo unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi ikiwamo Serikali.

 

“Programu endelevu zina faida zake, kwa mfano, nchi kama Zambia walifiwa na wachezaji wao wa timu ya Taifa mwaka 1993, wakachukua vijana wengine  waliokuwapo tayari wametengenezwa, mpaka sasa Zambia inaendelea kufanya vizuri katika medani ya soka,” amesema Malinzi.

Amesema kuwa kuna umuhimu wa kuwa na mashindano ya mikoa, ambayo yatashirikisha timu za vijana katika mikoa husika.

Kwa mujibu wa Malinzi, mashindano haya yatakuwa yakifanyika kuanzia ngazi ya vitongoji, kata, wilaya hadi kupata timu ya mkoa.

Kwa upande mwingine, Malinzi amesema kuwa kuna haja pia ya kuwa na michezo mbalimbali inayoshirikisha shule za sekondari kwa kuwa inasaidia kuinua vipaji.

“Kwa mfano, kuna michezo ya sekondari ilikuwa ikifanyika kule Bukoba ikifahamika kama hii, ilishirikisha sekondari za Bukoba, Ihungo, Kahororo, Nyakato na Omumwani (BUIKANO).

“Tunahitaji kuwa na mashindano kama haya ili kurudisha hadhi ya soka letu,” amesema Malinzi.

Ametoa mfano wa nchi ambazo zimefanikiwa kwa ajili ya mashindano ya sekondari kuwa ni pamoja na Uganda, ambayo amesema katika Afrika Mashariki kuwa ni nchi mojawapo iliyofanikiwa kuibua vipaji vingi katika soka.

Ili kufanikisha maendeleo ya soka, Malinzi amesema kuwa nchi inatakiwa iwe na mfumo wa aina moja wa kucheza mpira.

“Hapa ina maana ya kwamba tunaweza kuchagua nchi mojawapo kwa mfano Uholanzi tukawapeleka walimu wakajifunza huko ili wakirudi huku wanakuja kufundisha mpira wa aina moja,” amesisitiza.

Amesema kuwa mpira una mbinu nyingi ambazo mchezaji anatakiwa kuzifahamu kuanzia hatua ya kupiga mpira wenyewe na hata jinsi ya kupokea mpira.

Amesema kuwa walimu watakaokuwa wamepelekwa nje kusoma watapelekwa katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuanza kufundisha soka katika maeneo yao.

Malinzi amesisitiza kuwa mpira ni sayansi ambayo inabidi mchezaji aipate akiwa bado mdogo, hivyo amesisitiza kuwa kuna haja ya kuwa na walimu wenye uwezo wa kufundisha mpira.

“Leo hii Uingereza ina walimu 1,100 wenye leseni daraja A, Ujerumani wapo 5,500 na Hispania 12,000, Tanzania tunaye mmoja tu, kwa mujibu wa Ripoti ya TFF. Tanzania nzima ina walimu 2,000 tu wa mpira wa madaraja yote, je, tutafika? Amehoji Malinzi.

Ili kuweza kufikia mafanikio, Malinzi anawaomba wadau wa michezo kuwa wavumilivu kwa kusema kuwa kila kitu huwa kina mwanzo wake, kwa hiyo kinachotakiwa ni kuwa wavumilivu.

“Katika programu hizi na hasa zile za vijana ni kama vile tunapanda mbegu za mtama, hujui ipi itaota wapi lakini mwisho wa siku mbegu hizo zinaota, la msingi ni uvumilivu na ushirikiano,” amesema Malinzi.

969 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!