Baada ya porojo nyingi na propaganda duni siku za hivi karibuni kuwa makubaliano kati ya serikali na Kampuni ya Barrick Gold Corporation ya Canada yamekwama, hatimaye pande hizo mbili zimekata mzizi wa fitina kuhusu suala hilo.

Hii ni baada ya kusaini mikataba tisa Ijumaa iliyopita Ikulu, Dar es Salaam na kuhitimisha mazungumzo baina yao kuhusu umiliki na jinsi ya kuiendesha migodi mitatu mikubwa ya dhahabu humu nchini.

Awali, migodi hiyo ambayo ni Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu, ilikuwa chini ya Kampuni tanzu ya Barrick ya Acacia Mining ambayo kwa hivi sasa haipo tena, baada ya Barrick kuanza kuimiliki kwa asilimia 100.

Umiliki huo ulikuwa sehemu ya masharti ya kutanzua mgogoro uliokuwepo baina yake na serikali baada ya kubainika kuwa Acacia ilikuwa inafanya shughuli zake kinyume cha taratibu, ikiwemo ukwepaji wa kodi uliokuwa unaikosesha nchi mapato makubwa.

Kusainiwa kwa mikataba hiyo ya aina yake upande huu wa dunia si tu kuwa ni ushindi mkubwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano, bali hata kwa taifa zima kwa ujumla, kwani kuanzia sasa hakuna atakayejaribu tena kutupunja au kutunyonya kupitia rasilimali zetu.

Kwa kukamilisha na kufanikisha jambo hili nyeti kwenye uchumi na maendeleo ya nchi, Rais Dk. John Magufuli na timu yake wanastahili pongezi za dhati na kuungwa mkono na kila anayeitakia nchi yetu mema.

Nani kabla ya hapa alikuwa hata na ndoto kuwa serikali ingeweza kuwa na umiliki wa asilimia 16 kwenye mgodi wa dhahabu kama itakavyokuwa hivi sasa? Pia isingeweza kufikirika kabisa kuwa taifa linaweza kugawana faida za migodi inayohusika nusu kwa nusu chini ya kampuni ya pamoja kama itakavyokuwa baada ya Twiga Minerals Corporation kuanza shughuli zake rasmi.

Pamoja na kubezwa sana huku ikitahadhalishwa kuwa itawachefua wenye mitaji, serikali ilisimama kidete kwenye suala hili na matokeo yake ni mafanikio haya makubwa tunayoyaona ambayo wengi hawakuyatarajia.

Zaidi ya faida zitakazopatikana kutokana na makubaliano kati ya Serikali na Barrick ambazo ni nyingi sana, pia tumejifunza mambo mengi na kuionyesha dunia kuwa nchi changa zikiamua zinaweza kula sahani moja na wawekezaji wakubwa ambao mara nyingi hupenda wafaidi wao tu.

Hata hivyo, wakati tukishangilia ushindi huu wa aina yake kwenye historia ya nchi yetu, swali kubwa linabaki kuwa wako wapi waliotuingiza kwenye huu mkenge na adhabu yao ni nini?

By Jamhuri