Rais John Magufuli, ameshatangaza wakuu wa mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Kwenye uteuzi huo kuna sura mpya, na sura nyingine zilizozoeleka. Tunawapongeza kwa imani ambayo Rais Magufuli ameionyesha kwao.

Kama ilivyokuwa kwa wateule wengine, Watanzania hawatarajii kuona wateule hawa wakifanya sherehe kama ishara ya ‘kuula’.

Watambue kuwa wameteuliwa kuongoza mikoa katika kipindi cha Rais ambaye ameshaonesha kuwa hana mzaha katika utendaji kazi.

Kwa miaka mingi wakuu wa mikoa na hata wale wa wilaya, kazi zao kuu zimekuwa za mapokezi ya viongozi wa kitaifa, sherehe na ziara zisizokuwa na tija. Ni wakuu wa mikoa wachache waliosimama kidete kuhimiza na kusimamia shughuli za maendeleo katika mikoa yao.

Wakuu hawa wanakwenda kuwatumikia wananchi ambao hali zao kimaisha zinakabiliwa na changamoto nyingi za ujinga, maradhi na umaskini. Pia kuna matukio mengi ya wananchi kuonewa bila kupata watetezi.

Wakuu wa mikoa wanakwenda katika mikoa yao wakiwa wanapaswa kutambua kuwa kuna uharibifu mkubwa mno wa mazingira, hasa ukataji miti ovyo, uharibifu wa vyanzo vya maji, mapigano kati ya wakulima na wafugaji, ujangili, ujambazi na matukio mengine mengi yanayowakera wananchi.

Wakuu hawa wawe tofauti na watangulizi wao ambao kubwa walilolijua ni kulalamika tu hata kwa mambo ambayo utatuzi wake ulikuwa katika uwezo wao. Hatutaki kusikia wakuu wa mikoa wanaolialia kwa ukosefu wa madawati, vyakula, madarasa, nyumba za walimu, maabara na kadhalika.

 Wasiende katika mikoa kutafuta kupendwa kwa kuruhusu mambo yasiyo na tija, badala yale wahakikishe wanawashirikisha wananchi kufanya kazi kama njia pekee sahihi ya kuwawezesha kuutokomeza umaskini.

Wawe wabunifu wa fursa za kiuchumi katika mikoa yao, badala ya kusubiri maelekezo kutoka Ikulu au ofisini kwa Waziri Mkuu. Mkuu wa Mkoa asiye mbunifu wa maendeleo, huyo hafai kushika nafasi hiyo.

Wananchi wangependa kuona kwa mara ya kwanza wakuu wa mikoa wakitumia muda mrefu vijijini kutatua kero za wananchi, badala ya kuishia kwenye semina, makongamano na warsha zisizokuwa na tija. Kero zote zinazopaswa kumalizwa katika ngazi ya mkoa sasa zimalizwe huko huko.

Mkuu wa Mkoa anayeruhusu jambo jepesi lifikishwe kwa Waziri Mkuu au kwa Rais, huyo ajione kuwa ameshindwa kazi, na kwa hiyo awapishe wengine wanaomudu kasi ya Awamu ya Tano.

Tunawatakia utendaji kazi mwema tukiamini wataweka mbele nia njema ya kuwatumikia Watanzania ili kwa pamoja tuwe na Tanzania mpya. Wawe walinzi wa rasilimali za nchi yetu, badala ya kuwa mawakala na makuwadi wa wawekezaji wezi. Rais Magufuli, amewaamini, msimwangushe.

By Jamhuri