Wakati tarehe ya mwisho ya walimu wapya kuripoti katika shule walizopangiwa kufundisha ni Machi 9, mwaka huu, kama ilivyotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, walimu 53 kati ya 329 hawajaripoti katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka idara za elimu za shule za msingi na sekondari wilayani Kasulu, ni walimu 276 pekee waliozingatia kuripoti tarehe iliyotangazwa na wizara hiyo, na tayari wameshapokewa kwenye shule husika. Hata hivyo, Afisa Elimu wa Shule za Sekondari katika halmashauri hiyo, Patrick Athanasi, ameiambia JAMHURI hivi karibuni kuwa baadhi ya walimu wamekuwa wakikataa kupangwa kwenye shule zilizoko vijijini, wakihofia mazingira magumu ya kazi na ukosefu wa makazi bora na huduma nyingine muhimu za kijamii.


Lakini Athanasi amesema halmashauri hiyo ilijipanga mapema kuhakikisha walimu wapya wanapata stahili zao, yakiwamo malipo ya pesa za kujikimu na usafiri.


“Halmashauri imekamilisha zoezi la kuandaa kumbukumbu za utumishi za walimu walioripoti na kuzituma idara kuu ya utumishi mapema, ili kuepuka tatizo la kucheleweshewa mishahara yao,” ameongeza.


Kuhusu walimu ambao bado hawajaripoti, Athanasi ametoa wito kwa walimu hao kuripoti haraka na kama kuna mwenye tatizo linalomchelewesha atoe taarifa kwa mamlaka husika. Mwaka huu Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu walimu wapya 329, kati yao, 173 ni wa ngazi ya cheti, 42 ni wa ngazi ya stashahada na 114 ni wa ngazi ya shahada.


Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu yenye shule za msingi za Serikali 222 na shule za sekondari za Serikali 44, bado inakabiliwa na tatizo la idadi ndogo ya walimu.


By Jamhuri