Waliomdanganya JPM kibao chageuka rasmi

Miezi miwili tangu aliyestahili tuzo ya mfanyakazi bora wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), James Kunena, kupokwa fursa hiyo saa chache kabla ya kutunukiwa na Rais Dk. John Magufuli katika kilele cha mwaka huu cha Mei Mosi, hali si shwari ndani ya Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU).

Uchunguzi wa JAMHURI umebaini hali ya ‘hasira’ miongoni mwa wafanyakazi wa ngazi za chini dhidi ya uongozi wa juu wa chama hicho. Hali hiyo ya mvurugano, kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti hili unaothibitishwa na baadhi ya nyaraka, inasukumwa na mambo makuu matatu.

Moja kati ya mambo hayo matatu ni hilo la kupora ushindi wa mwenzao aliyestahili kuwa mfanyakazi bora. Aliyestahili tuzo hiyo ni James Kunena, lakini ‘uchakachuaji’ ukafanyika likapenyezwa jina la Focus Sahani, kutoka upande wa menejimenti ya TRC.

Jambo jingine ni viongozi wakuu wa TRAWU kushindwa kusimamia au kudai uhuishaji wa mkataba wa hali bora kati ya TRAWU na TRC, na jambo la tatu ni viongozi hao kushindwa kwa zaidi ya miaka miwili kutembelea wanachama na kuwapa taarifa ya mambo yanayohusu ajira zao.

Wanavyoshikana ‘mashati’

Katika kinachoweza kuelezwa kuwa namna wafanyakazi hao ‘wanavyowashika mashati’ viongozi wao wakuu ndani ya TRAWU, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa Juni 20, mwaka huu, wanachama wa TRAWU, chama kinachoundwa na wafanyakazi wa reli kutoka TRC kwa upande mmoja na TAZARA kwa upande mwingine, waliandika waraka kwenda kwa kila mjumbe wa kamati kuu ya chama chao hicho.

Wanachama hao kutoka kanda za TRAWU za Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Kigoma na Tabora licha ya kuandika waraka huo waliambatanisha pia na saini zao.

Ujumbe uliomo kwenye waraka huo kwenda kwa wajumbe hao wa kamati kuu ya TRAWU unawataka wajumbe husika kufanya uamuzi katika maeneo makuu manne.

Kwanza, kuitisha kikao cha dharura na kuwasimamisha na hatimaye kuwaondoa kwenye nafasi zao Mwenyekiti na Kaimu Katibu Mkuu.

Pili, chama kikabidhiwe haraka kwa wadhamini wake wakisimamie kipindi cha mpito. Tatu, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iombwe kufanya ukaguzi maalumu (special audit) kwenye hesabu za TRAWU.

Nne, waraka huo unataka uchaguzi uitishwe haraka kutengeneza safu mpya ya uongozi wa chama katika ngazi ya taifa.

“Ndugu wajumbe (kamati kuu) ni matarajio yetu kuwa hatua tulizopendekeza zitaanza kuchukuliwa mapema iwezekanavyo,” wanaeleza wafanyakazi hao katika waraka wao na kuweka ukomo wa utekelezaji kuwa ni wiki tatu tangu kuandikwa kwa waraka huo.

Na endapo matakwa yao yatapuuzwa kwa kutotekelezwa ndani ya wiki hizo tatu, wanasema wafanyakazi waliojiorodhesha watafanya uamuzi wa kutumia vifungu husika vya kisheria kuhakikisha matakwa yao yanatimia.

“Tutachukua uamuzi wa kutumia kifungu cha 61, 4-5 ambapo tutamtaka mwajiri asimamishe mara moja makato ya ada za chama kutoka kwenye mishahara yetu. Ni matumaini yetu kuwa tuliyoyaeleza yatatiliwa maanani na kutekelezwa,” inaeleza sehemu ya waraka huo wa wafanyakazi kwenda kwa kila mjumbe wa Kamati Kuu ya TRAWU na nakala kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na wahusika wengine akiwamo Mwenyekiti wa TRAWU taifa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini.

Wafanyakazi hao vilevile wanadai kuwa viongozi wao wa sasa kitaifa wamekuwa wakikiongoza chama hicho kwa kujua au kutokujua, kinyume cha matakwa ya baadhi ya vifungu vya sheria ya ajira na uhusiano kazini, moja ya kifungu hicho wamekitaja kuwa ni 46 (1)-C cha Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004, kinachobainisha kuwa TRAWU inapaswa kuwa huru bila kufungamana na mwajiri yeyote.

Deogratus Magere ni mfanyakazi wa TRC ambaye kituo chake cha kazi kiko mkoani Tabora, amelieleza JAMHURI kuwa wanataka mabadiliko ya uongozi katika chama hicho ili wapate watetezi wapya, kwani viongozi waliopo kwa sasa hawafanyi kazi hiyo.

“Mimi ni mwajiriwa wa TRC kama fundi wa magari ya shirika, tangu mwaka 2013 kuna magari tuliyafanyia matengenezo, lakini hadi leo hatujalipwa. Tukipeleka hoja zetu TRAWU hazipati ufumbuzi, wala hatupatiwi majibu yoyote, hivyo ili kuondokana na hali hii tunatakiwa kubadilisha uongozi,” amesema Magere.

Gilbert Kabamba, mfanyakazi wa TRC mkoani Kigoma na mwanachama wa TRAWU amelieleza JAMHURI kuwa vita iliyopo kwenye chama hicho ni baina wafanyakazi wa TRAWU na uongozi wa chama hicho ngazi ya taifa.

Amesema viongozi hao wanawadharau wanachama wao, kwani hata baada ya kuwa wamewaandikia barua mbalimbali za malalamiko uongozi wa TRAWU taifa haujajibu barua hata moja, jambo lililoibua hisia za kusalitiwa kwa wanachama hao.

“Sisi hatuna shida nao, tunachotaka ni viongozi hao wawajibike kwetu kama tulivyowachagua kututumikia. Tuliwapa dhamana ya kutuongoza, kama wangekuwa wanakuja mikoani kupata maoni yetu kusingekuwepo na shida, wao waje mikoani kusikiliza kero, wasijifiche makao makuu ya chama.

“Viongozi hawa wanapita kuomba kura, wakishazipata hatuwaoni tena. Nafikiri sasa umefika wakati wa kufanya maamuzi ya msingi kwa ajili ya ustawi wa chama na wanachama,” amesema Kabamba.

Mwenyekiti wa TRAWU Taifa, Lomitu ole Saitabau, amelieleza JAMHURI kuwa malalamiko ya wanachama hao wameyapokea na wanayafanyia kazi na kwamba, kwa sasa wanajiandaa kuitisha kikao ambacho wanachama watatakiwa kuwasilisha ushahidi wa malalamiko yao.

“Mwandishi niko kwenye gari naelekea Dodoma, lakini nikueleze kwa ufupi tu barua ya malalamiko yao ninayo. Tutawaita kwenye mkutano huo ili watoe ushahidi kama utakuwa wa kuridhisha hatua zaidi zitachukuliwa,” anaeleza Saitabau.

Saitabau amesema wao kama viongozi wanafanya kazi kwa kuzingatia misingi na katiba ya chama, hivyo wanaolalamika hoja zao zitajibiwa kwa mujibu wa katiba hiyo.

“Wanachama kusema hawatutaki si jambo baya, wakija na ushahidi wa kwanini hawatutaki wajumbe wakiridhishwa nao tutaachia ngazi,” amesema Saitabau.

Kaimu Katibu Mkuu wa TRAWU, Nashoni Mariyeri, ameliambia JAMHURI kuwa wao kama viongozi hawafanyi kazi na magazeti na kwamba huenda wanachama wao wakapoteza haki zao.

“Taratibu zetu zipo, huwa tunafuata sheria na katiba. Wao kama wamekuja kwenye magazeti wamekosea sana. Pengine hayo wanayoyalalamikia wakiyaleta kwenye magazeti yanaweza yasifanikiwe,” amesema.

Kazi ya JAMHURI

Gazeti hili katika toleo lake namba 398 la Mei 14 – 20, 2019, lilichapisha kashfa ya kubadilishwa kwa mshindi wa tuzo ya mfanyakazi bora ndani ya TRC.

Katika habari hiyo gazeti lilieleza namna wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania na Zambia (TAZARA) na wale wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), mashirika ambayo kwa pamoja wafanyakazi wake wanaunda TRAWU, yalivyoendesha zoezi la kupiga kura kupata mfanyakazi bora kwa kila upande, lakini matokeo ya mshindi kwa upande wa TRC yaligeuzwa dakika za mwisho.

Katika shughuli za kilele cha Mei Mosi zilizofanyika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya, mgeni rasmi akiwa Rais Dk. John Magufuli, JAMHURI lilieleza jinsi mfanyakazi wa kada ya chini, James Kunena, alivyoshinda kuwa mfanyakazi BORA kwa mujibu wa kura zilizopigwa kupitia TRAWU.

Lakini kura hizo zilibadilishwa na viongozi wa TRAWU Taifa kwa kubadilisha jina la mfanyakazi BORA, na kumpa nafasi ya kushiriki sherehe hizo kama mshindi wa kundi la mfanyakazi HODARI ambaye hakustahili kuhudhuria sherehe hizo kwa mujibu wa taratibu za TRAWU.

Katika habari hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari “Wamdanganya Magufuli” ilielezwa: “Kashfa imegubika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi mwaka huu yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya.

“Kashfa hiyo imekikumba Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU). Ndani ya chama hicho, baadhi ya viongozi wake wanadaiwa kuwasilisha jina la kigogo asiyestahili kuwa mfanyakazi bora, akapewa mkono na Rais Dk. John Magufuli na kukabidhiwa cheti cha mfanyakazi bora na zawadi ya hundi.

“Katika mchakato wa upigaji kura, JAMHURI limethibitishiwa kuwa mfanyakazi wa kada ya chini, James Kunena, ndiye aliyeshinda kuwa mfanyakazi BORA kwa mujibu wa kura zilizopigwa kupitia TRAWU.

“Hata hivyo, kwa njia ya hila zilizofanywa na baadhi ya viongozi walifanya uchaguzi wa kumpata mfanyakazi HODARI, kwa hiyo kulikuwa na mshindi wa kundi la mfanyakazi BORA ambaye ndiye anastahili kuhudhuria sherehe za kitaifa za Mei Mosi na kukabidhiwa zawadi zake na mgeni rasmi. Mshindi wa kundi la mfanyakazi HODARI, kwa kawaida, kwa mujibu wa taratibu za TRAWU huhudhuria sherehe za Mei Mosi kikanda na hukabidhiwa zawadi na mgeni rasmi wa sherehe hizo za kikanda ambazo ni ndogo ukilinganisha na zile za kitaifa.

“Mshindi wa tuzo ya mfanyakazi BORA TRAWU kwa mujibu wa kura za wafanyakazi ni James Kunena, na mshindi wa tuzo ya mfanyakazi HODARI ni Focus Sahani, ambaye ushindi wake ulipatikana baada ya kura kupigwa kwa raundi tatu.

“Wafanyakazi wote tulijua kwamba Kunena ndiye mshindi wetu, na atakuwa katika sherehe za kitaifa Mbeya kukabidhiwa zawadi zake, jambo ambalo lingetupatia hamasa zaidi sisi wafanyakazi wa kawaida, lakini kinyume chake, akatangazwa Focus Sahani ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji TRC,” ameeleza mmoja wa watoa habari wetu aliyeshiriki mchakato wa kusaka mfanyakazi bora.

Ilivyokuwa Uwanja wa Sokoine

Dalili za mipango hiyo ya ‘kupindua’ mshindi zilianza kubainika wakati shughuli ikiendelea. Wakati wa kusoma majina ya washindi wa kipengele cha wafanyakazi bora kwa upande wa TRAWU – TRC akatajwa Focus Sahani badala ya James Kunena.

Sahani akasogea mbele ya Rais Magufuli na kukabidhiwa zawadi, lakini kutokana na hilo, Kunena akawa mkali, akawahoji viongozi wake, imekuwaje?

Hili analibainisha mwenyewe Kunena katika mazungumzo yake na JAMHURI. Anasema: “Sikuelewa kilichotokea, nilisafirishwa kwenda Mbeya kwa kuwa ndiye mshindi wa kipengele cha mfanyakazi bora, nikashangaa mfanyakazi hodari ndiye anaitwa badala yangu, huyu mfanyakazi hodari alipaswa kushiriki sherehe za Mei Mosi kikanda ili apewe zawadi yake huko.

“Kutokana na hali hiyo ilibidi nimuulize Katibu Mkuu wa TRAWU (Taifa) kuhusu jina langu kuondolewa kinyume cha matakwa ya wafanyakazi walionipigia kura za ushindi. Akaniambia waliwasilisha jina langu, na kwamba nisubiri wafuatilie kilichotokea.

“Focus Sahani alikwenda kushikana mkono na rais na kupewa zawadi ya mfanyakazi bora, baada ya mimi kuhoji Katibu Mkuu akaniletea bahasha ndogo ya kaki yenye hundi mbili. Hundi ya kwanza yenye shilingi milioni mbili, na hundi ya pili ya shilingi laki tano. Nikauliza, vipi kuhusu zawadi ya cheti? Akasema ‘utapatiwa Dar es Salaam’.

“Hiyo iliniumiza sana kwa kuwa washindi wote walipewa zawadi na kushikana mkono na Mheshimiwa Rais. Sikutaka kuhoji sana kwa kuwa viongozi hao ndio walionisafirisha kwenda Mbeya, sikuwa na nauli ya kurudi. Nimerudi Dar es Salaam, wafanyakazi wenzangu wananilaumu…nimeingia katika mgogoro na wafanyakazi wenzangu walionipigia kura kuwa mfanyakazi bora kwa mwaka 2019. Wanasema nimehongwa pesa ili niondoe jina langu na kuwekwa jina la bosi wetu, Focus Sahani.

“Nimekanusha hili kwao, lakini hawanielewi, nimewasilisha malalamiko kwa wakubwa wangu wa chama ngazi ya mkoa na kanda, wanasema wanalifanyia kazi suala hili,” amesema James Kunena.

Gazeti hili limewasiliana na Focus Sahani, ambaye alimweleza mwandishi wetu kuwa yuko katika mkutano na atumiwe ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, lakini hadi tunakwenda mitamboni hatua zote hizo hazikuzaa matunda katika kupata maelezo yake ingawa juhudi hizo zinaendelea.

Katika kuzungumzia kadhia hiyo, Katibu Mkuu wa TRAWU – Taifa, Nashoni Mariyeri, ameliambia JAMHURI kwamba wote wawili – James Kunena na Focus Sahani walistahili kupata zawadi kwa kiwango sawa mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Magufuli.

Amefafanua kuwa, kutokana na muda kuwa mfupi na matakwa ya kutaka orodha ya wanaotakiwa kupewa zawadi kupunguzwa, James Kunena alikubali mwenzake amwakilishe kupokea zawadi hizo.

“Walikubaliana kwamba mwenzake amwakilishe. Kila mmoja aliandaliwa zawadi ya hundi ya shilingi milioni 2.5 pamoja na cheti,” amesema.

JAMHURI katika habari yake hiyo lilieleza kiini cha utata, kwamba: “Utata unaogubika sakata hili ni kwamba, cheti cha mfanyakazi (bora) kwa upande wa wafanyakazi wa reli kinapaswa kutwaliwa na watumishi wawili tu, mtumishi mmoja kutoka TAZARA na mtumishi mwingine kutoka TRC, kwa maana hiyo, ahadi ya kumtengenezea cheti kingine James Kunena cha ufanyakazi bora itaifanya TRC kutoa wafanyakazi bora wawili kwa mwaka 2019, jambo ambalo linatajwa kutokuwahi kutokea katika historia ya Mei, Mosi nchini.

“Shida iliyopo sasa ni kupata cheti halisi. National Best Workers (wafanyakazi bora) vyeti vyao hutoka Shirishiko la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), ushindi wa madaraja mengine ya chini (mfanyakazi hodari) hutolewa na ngazi za vyama vyenyewe si shirikisho.

“Kwa maana hiyo, katika rekodi za wafanyakazi bora mwaka huu pale TUCTA, kutoka TRC hatakuwapo James Kunena kama alivyochaguliwa na wafanyakazi wenzake, atakuwapo Focus Sahani.

“Wakisema wampe cheti sasa, TRAWU haijapata kuwa na ‘Best National Workers’ watatu kwa mara moja, huwa ni mmoja kutoka TAZARA na mwingine kutoka TRC, sasa hicho cheti kinaweza kuwa ‘feki’.

“Cheti hiki cha kupeana baada ya Mei Mosi hakitaingizwa kwenye rekodi za mwaka huu,” ameeleza mmoja wa viongozi wa juu aliyeshiriki Mei Mosi mwaka huu mkoani Mbeya, ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini.

Akizungumzia kuhusu hoja za Katibu Mkuu wa TRAWU kwamba kulikuwa na makubaliano kati ya Focus na Kunena, kiongozi huyo naye amehoji: “Kama kulikuwa na makubaliano kwa nini James Kunena anahoji kuhusu haki yake kuporwa?

“Amekwisha kulalamika rasmi kwa Mwenyekiti wake wa Kanda ya Dar es Salaam TRAWU, kuna viongozi kadhaa wamekwisha kufikishiwa malalamiko haya, Mei 4, 2019 tulikaa kikao kilichohusisha mwenyekiti na katibu wa matawi mawili ya TRC, Tawi la Karakana na Tawi la Makao Makuu kujadili suala hili, tuliazimia apewe cheti chake cha mfanyakazi bora kama ilivyostahili.”

Taarifa zaidi zilizolifikia JAMHURI zinabainisha kuwa suala hilo halikuwafurahisha wafanyakazi wa kawaida wa TRC kiasi cha kutikisa ufanisi wao kikazi, wakiamini kuwa utashi wao wa kutaka mwenzao awe mfanyakazi bora umepuuzwa.

“Sisi tumemwinua mfanyakazi mwenzetu, akashikane mkono na Rais Magufuli, apewe zawadi zake na Mheshimiwa Rais. Matokeo yake mlala hoi mwenzetu ameenguliwa, tumesikitishwa sana na hili, tunaomba haki itendeke,” amesema mmoja wa wafanyakazi aliyepata kupiga kura ngazi ya tawi kumchagua mfanyakazi bora ndani ya TRAWU, akitaka jina lake lihifadhiwe ili kutoshughulikiwa kinidhamu na watendaji wa ngazi za juu.

Habari hiyo pia ilimpa nafasi Katibu Mkuu wa TUCTA, Dk. Yahya Msigwa, ambaye pamoja na mambo mengine kutoka kwake kwa wakati huo, JAMHURI lilitaka kufahamu, kwanza, barua iliyowasilishwa kwao kutoka TRAWU ilibainisha nani mfanyakazi bora. Pili, hundi iliyoandaliwa na cheti kiliandikwa kwa jina la nani.

“Siioni barua yao. Hawakuleta barua yenye majina hapa ofisini, walikuja Mbeya (kwenye kilele cha Mei Mosi) moja kwa moja, tulipata jina kwenye maadhimisho hayo,” amesema Katibu Mkuu huyo wa TUCTA, lakini alipoulizwa kufafanua kuhusu utaratibu wa ofisi yake kupata majina ya wafanyakazi bora kutoka vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini alijibu:

“Mimi (Katibu Mkuu TUCTA) ndiye ninawaandikia barua vyama vyote kuwataka wawasilishe majina ya wafanyakazi bora kwa barua. Nikishapokea barua, ndipo tunaandaa vyeti na zawadi. Orodha hiyo ndiyo inayosomwa katika kilele cha maadhimisho ya Mei Mosi.”

Kuhusu suala hilo la TRAWU alisema jina alilopewa katika hatua za mwisho ni Focus Sahani, na kama kuna kasoro nyingine si suala la TUCTA bali uongozi wa TRAWU.

Sherehe za kitaifa za Mei Mosi mwaka huu zilifanyika Uwanja wa Sokoine mkoani Mbeya, mgeni rasmi akiwa Rais Dk. Magufuli.