Waliokuwa wafanyakazi wa Taasisi ya Kuzuaia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), walioenguliwa wameanza kupangiwa majukumu katika idara na taasisi nyingine za serikali.

Waliopangiwa vituo tayari ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Ekwabi Mujungu, ambaye amehamishiwa Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, kama msaidizi anayehusika na masuala ya utawala na Mbengwa Kasomambuto, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Uchunguzi, yeye amehamishiwa Ofisi ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Wengine ni Joyce Shundi, ambaye amehamishiwa katika Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, huko anakwenda kuwa Mchumi Mkuu; Alexander Budigila ambaye alikuwa Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, amehamishiwa Shirika la Umeme (TANESCO); Peter Billa, amehamishiwa Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini kuwa Ofisa Utumishi (GPSA); Eunice Mmari, amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu, Bunge na Watu wenye Ulemavu.

Watumishi wengine waliopangiwa vituo tayari ni Stephen Mbele, aliyehamishiwa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC); Mazome, amehamishiwa Ofisi ya Msajili Vyama vya Siasa, ambako anakwenda kuwa Mchumi Mkuu; Lazaro Mawingu amehamishiwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma; Danieta Tindamanyire, amehamishiwa Wizara ya Mifugo katika nafasi ya Mchumi Mkuu na Abubakar Msangi, amehamishiwa Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, ambako anakwenda kuwa  Mwanasheria.

Wakati Mushumbusi amehamishiwa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Mwarabu amehamishiwa Chuo Cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT); Ndibaiukao yeye amehamishiwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Robert Kitundu amehamishiwa kwenye taasisi ya utafiti wa chai; Mary Kidima amehamishiwa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na Juventus Baitu amehamishiwa Kituo cha Uwekezaji (TIC).

Fagio ndani ya Takukuru limetangazwa wiki ya kwanza ya Januari, ikiwa ni miezi mitatu tangu kuteuliwa kwa Mkurugenzi Mkuu mpya, Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani, ambaye wakati anaapishwa alikabidhiwa jukumu la kufanya mabadiliko ya kimuundo ndani ya taasisi hiyo.

Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani, alinukuliwa akisema ni kweli kwamba watumishi hao wamehamishwa huku akiwataja baadhi ya watumishi na nyadhifa zao.

“Baadhi ya watumishi hao ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Alex Mfungo; Mkurugenzi wa Upelelezi, Mbengwa Kasomambuto na Ekwabi Mujungu aliyekuwa Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma,” amesema Kapwani.

Amesema uhamisho huo ni wa kawaida, Kapwani ameeleza kuwa hiyo ni mara ya kwanza kwa Takukuru kuhamisha watumishi wengi kwa wakati mmoja.

“Yawezekana kwa Takukuru ikawa ni mara ya kwanza kuhamishwa kwa idadi kubwa, lakini kama mnavyofahamu, sisi kama watumishi wa umma hatulazimiki kufanya kazi katika taasisi moja tu.

“Tunapenda kusisitiza kuwa uhamisho huu ni wa kawaida kama ambavyo mmekuwa mkisikia unafanyika katika wizara au idara nyingine za serikali.

“Yawezekana kwa Takukuru ikawa ni mara ya kwanza kuhamishwa kwa idadi kubwa lakini kama mnavyofahamu, sisi kama watumishi wa umma hatulazimiki kufanya kazi katika taasisi moja tu,” amesema Kapwani.

Kapwani amesema uhamisho uliofanyika ni wa watumishi 40 ambao umehusisha ngazi ya wakurugenzi, wakaguzi wa kanda, wakuu wa Takukuru wa mikoa pamoja na wakuu wa vitengo na sehemu ya makao makuu.

 Walioshika nafasi za wakurugenzi waliohamishwa ni Kaimu Mkurugenzi wa Utumishi na Rasilimali Watu, Ayoub Akida na Kaimu Mkurugenzi wa Uchunguzi, Kassium Ephrem.

Rais John Magufuli alipokuwa anamwapisha Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Diwani Athumani, alimtaka kuuangalia upya muundo wa Takukuru ili uweke bayana majukumu ya Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru.

Jambo jingine ni kuhakikisha watendaji wa taasisi hiyo wanaoonekana kutofanya kazi kwa tija na kujihusisha na vitendo vya rushwa wanachukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kuondolewa kazini na kufikishwa mahakamani.

1862 Total Views 3 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!