Shilingi bilioni 2.27 zinadaiwa kutumika kinyume cha taratibu na
sheria ya fedha katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza.

Fedha hizo ni mapato ya vyanzo mbalimbali ambayo hayakuwapo kwenye mpango wa bajeti ya halmashauri hiyo wa mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Ripoti ya Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Kwimba ya robo ya kwanza ya Julai – Septemba 2018/2019 inasema fedha zilizotumika bila kuidhinishwa kisheria ni Sh. 2,274,635,105.23.

Tayari imeshawasilishwa kwenye Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Kwimba chini ya Mwenyekiti wake, Peter Ngasa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, fedha hizo zilitumika kama ifuatavyo:- RBF
Sh 477,605,855.86; P4R Sh 396,229,249.37.

Nyingine zimeelekezwa ngazi ya chini ya sekondari Sh milioni 537.2, ngazi ya chini elimu ya msingi Sh milioni 66 na ngazi ya chini ya afya Sh milioni 800.

“Mapokezi ya fedha nje ya bajeti iliyoidhinishwa yanaonyesha kwamba
katika maandalizi na utekelezaji wa bajeti hauonyeshi ukweli na uhalisia, licha ya matumizi makubwa ya rasilimali/gharama katika uandaaji wake,” inasema ripoti hiyo.

Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Marwa Christopher, anasema: “Tunashauri Serikali Kuu na Menejimenti ya Halmashauri kutekeleza mpango na bajeti kama ilivyopitishwa na kuidhinishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” inasena ripoti hiyo.

Mweka Hazina wa halmashauri hiyo, Peter Revelina, katika majibu ya hoja za mkaguzi huyo, amesema uongozi wake umeridhia ushauri wa mkaguzi.
Mwaka wa fedha wa 2017/2018 Kwimba ilipokea Sh 1,483,080,395.91
badala ya Sh. 1,111,057,000 zilizoidhinishwa katika bajeti. Hivyo Sh 372,023,395.19 (asilimia 34) ziliingizwa zaidi ya bajeti.

“Hii inaashiria kuwa bila kupitisha bajeti ya ziada, mapokezi ya fedha zaidi ya bajeti iliyoidhinishwa, yanaweza kuchangia kutumika vibaya,
kwa fedha hizo na watumishi wasio waaminifu. Tunashauri menejimenti ya halmashauri, kuchambua na kujua sababu zilizosababisha ongezeko hilo katika takwimu zao.

“Aidha, ni vema kuwasiliana na Hazina kuangalia kilichosababisha ongezeko hilo la fedha,” anasema mkaguzi huyo wa ndani, kupitia ripoti yake.

Katika hatua nyingine, Sh 180,510,013.37 za makusanyo ya ndani ya halmashauri hiyo zinadaiwa kutafunwa na baadhi ya watendaji Kwimba.

Fedha hizo ni makusanyo ya Julai – Septemba, mwaka jana ambako hadi Oktoba 1, mwaka jana  zilikuwa hazijaingizwa kwenye akaunti ya halmashauri.

Mkaguzi wa Ndani anasema amepitia nyaraka za makusanyo yatokanayo na vyanzo vya ndani na kubaini fedha hizo zipo nje ya benki.
“Fedha zote zinazokusanywa ni lazima zipelekwe benki, kwenye akaunti husika ya halmashauri kila siku. Au siku inayofuata, kama makusanyo hayo yalifanyika zaidi ya saa za kazi,” amesema.

Ofisi ya Mkurugenzi kupitia Mweka Hazina wake, imesema:
“Sh milioni 40 zimesharejeshwa na kupelekwa benki.

Jitihada za kuwasilisha kiasi kilichosalia zinaendelea.” Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba, Pendo Malebeja, ameliambia JAMHURI:
“Hili suala lipo kwenye vikao. Naomba uliache.”

Ripoti ya Mkaguzi wa Ndani inasema Kwimba haina uwezo wa kujiendesha bila kupewa fedha na Serikali Kuu. Uwezo wake wa kujitegemea ni asilimia 30.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya kwimba, Shija Malando, anasema, “Ripoti ya mkaguzi ni nzuri mno.

Zaidi ya milioni 180 zimepotea mikononi mwa baadhi ya watumishi wa halmashauri. Sisi hatutakubaliana na hali hii. Mimi na wenzangu (hakuwataja) tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais John Magufuli kukemea ufisadi. Tunataka hizi fedha zirudishwe.”

By Jamhuri