Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dk. Audax Rutabanzibwa, kwa miaka mitano sasa, ama ameshindwa, au amepuuza kuandaa mashitaka dhidi ya viongozi wa Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) cha Wazalendo cha mjini Moshi wanaotuhumiwa kuiba Sh bilioni 6.

Miongoni mwa watuhumiwa wa utafunaji fedha hizo ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Profesa Faustine Bee. Pamoja naye, watuhumiwa wengine ni wahadhiri na watumishi katika chuo hicho.

Dk. Rutabanzibwa ndiye aliyebaini upotevu wa fedha hizo, lakini wanachama wa Wazalendo Saccos wanahoji kigugumizi kinachomfanya asiwezeshe kufunguliwa mashitaka dhidi ya watuhumiwa.

Kumekuwa na madai kwamba kesi dhidi ya watuhumiwa imeshafunguliwa mahakamani, lakini JAMHURI imethibitishiwa kuwa hakuna kesi yoyote kwa miaka mitano sasa.

Wanachama wa Wazalendo Saccos wameieleza JAMHURI kuwa Mrajisi huyo ndiye aliyekagua na kubaini wizi wa kiasi hicho kikubwa cha fedha na kutoa mapendekezo ya kuchukuliwa hatua wahusika, ikiwa ni pamoja na kuwabana ili warejeshe fedha hizo zilizochotwa kwa mbinu ya ‘malipo hewa’.

Wanasema wamechoka kwa miaka yote kuambiwa kwamba kesi bado ipo katika hatua za uchunguzi za Jeshi la Polisi.

“Polisi wanachunguza nini kwa miaka yote hii tangu mwaka 2012 wakati kila kitu kipo wazi na baadhi ya wahusika wameeleza wizi ulivyokuwa unafanywa? Kwa nini uchunguzi ufanyike kwa miaka zaidi ya minne – kama hakuna hujuma ni nini?” Anahoji mmoja wa wanachama hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini kwa hofu ya chuo kumfukuza kazi.

 

Mrajis azungumza

Akihojiwa na JAMHURI mwishoni mwa wiki iliyopita, Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dk. Rutabanzibwa, anasema tuhuma zinazoelekezwa kwake za kuwalinda wahusika wa wizi huo hazina ukweli wowote.

Anasema kosa lolote la jinai linaporipotiwa kwenye vyombo vya dola, kuna taratibu zinazofanyika hadi kufunguliwa kesi zikihusisha Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka.

“Ni kweli nilifanya ukaguzi na kubaini wizi huo uliofanywa na Bodi iliyopita ya Wazalendo Saccos na taratibu za kuwachukulia hatua za kisheria zinazotekelezwa na vyombo husika; hawa wanaosema mimi nawalinda wahusika wa tukio hili ni akina nani?

“Utaratibu ndivyo ulivyo na iwapo litabainika kosa kwa wote waliohusika watafikishwa mahakamani na kama unahitaji kuelewa hatua iliyofikiwa hadi sasa mtafute Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbrod Mutafungwa, utapata ukweli wote kuhusu suala hili,” amesema Dk. Rutabanzibwa.

 

Kauli ya RPC Mutafungwa

JAMHURI imemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Mtafungwa, ili kuelewa kwa nini suala hilo limekwama ndani ya Jeshi la Polisi mkoani humo, baada ya kuripotiwa miaka karibu mitano sasa; na yeye amesema halielewi kabisa kwa kuwa bado ni mgeni.

Anasema wakati huo kulikuwa na kamanda mwingine wa polisi mkoani humo. Hata hivyo, ameahidi kulifuatilia ili kubaini ukweli.

 

Kauli ya Kaimu Mrajisi wa Mkoa

Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro, Shose Monyo, anasema tatizo la vyama vya ushirika kukumbwa na wizi wa aina hii ni kubwa.

Monyo anasema wizi uliofanywa na Bodi iliyopita ya Wazalendo Saccos kwa mikopo hewa ya wanachama, umesababisha baadhi ya wanachama waliostaafu kukatwa mafao yao yote kulipia mikopo ambayo hawakukopa.

Anasema Mbonea Maghimbi na washirika wake wamechukua fedha nyingi mno kwa mikopo hewa kwa kutumia majina ya wanachama na wasiokuwa wanachama wa Saccos hiyo, na kugawana fedha hizo na kusababisha matatizo kwa chama hicho.

Anasema Bodi ya Saccos inatakiwa kufuatilia kwa ukaribu suala hilo linaloelezwa liko ‘mahakamani’, na kuwajulisha wanachama kila hatua ili kuwaondolea shaka ya kuendelea na chama hicho.

Anasema miamala ya fedha isiyozingatia utaratibu ilifanywa na waliokuwa viongozi wa Saccos kwa kumtumia Reuben Mwandambo, huku wakigawana fedha hizo kwa kuorodhesha wanachama hewa ambao walipewa mikopo ya mamilioni.

Wanachama hao wanasema wanapohoji kuhusu upotevu wa fedha hizo na wahusika kuachwa wakitamba kazini na mitaani, uongozi wa chuo umekuwa ukitishia kuwafukuza kazi.

Wazalendo Saccos ilikopa fedha kwa udhamini wa Chuo cha Ushirika Moshi kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2012 kutoka CRDB, KCBL, SELF, PPF na Oiko Credit na kusababisha upotevu wa Sh bilioni 6.

Ripoti ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, inaeleza kwamba chama hicho kilikopa kiasi kikubwa kutoka katika taasisi za fedha kilichofikia Sh 6,803,610,000 bila kufanya tathmini kutoka taasisi mbalimbali.

Mwaka 2008 hadi 2011 kilikopa  Sh 4,243,700,000 kutoka katika taasisi hizo za fedha huku mikopo yote kwa asilimia 50 ikitolewa bila kuzingatia taratibu; wakati asilimia 11.8 ya mikopo hiyo ikitumika katika urejeshaji wa mikopo kutoka taasisi moja na kwenda nyingine.

Bodi, Menejimenti na Kamati ya Usimamizi iliyokuwapo kati ya mwaka 2008 hadi 2012 ilihusika na upotevu wa Sh 3,381,899,103 ikiwa ni mikopo au malipo yasiyozingatia taratibu yanayofikia Sh 3,099,102,303 na upotevu wa Sh 254,516,890 na kusababisha kiasi hicho kikubwa cha fedha kuwa nje na hivyo kutorejeshwa.

Waliotajwa kwenye ripoti hiyo kuhusika na upotevu wa fedha hizo ni pamoja na Mbonea Maghimbi, Reuben Mwandambo, Emrode Kimambo, Dk. John Haule, Jasinta Tarimo, Ibrahim Shughuru, Gloria Chuwa na Paul Kibiriti ambaye ni askari polisi akihusishwa pia na uchukuaji wa fedha zilizokabidhiwa kwa Maghimbi.

Pia uongozi wa chama hicho unatajwa kushindwa kusimamia vizuri uendeshaji na usimamizi wa chama kwa kuzingatia sheria ya Ushirika, kanuni na miongozo iliyoko ndani ya chama ikiwa ni pamoja na sera ya mikopo na fedha.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika anaeleza kwamba dosari zilizobainika ni pamoja na kubadilisha utaratibu wa malipo kwa njia ya fedha taslimu badala ya hundi na kumtumia Mtunza Fedha Mkuu wa Chuo, Mwandambo, kuchukua fedha kwa kumhusisha askari (Kibiriti) asiyekuwa mtumishi wa chama, kubeba fedha na kuzifikisha sehemu ambayo si ofisi ya chama.

“Kumekuwa na mchezo wa kuiga saini za watu na kuchukua fedha na kuashiria uwepo wa matumizi yasiyokuwa ya halali, huku fedha nyingi zikilipwa kwa kutumia majina yasiyokuwa ya kweli na hivyo kutokuwa na uhakika wa mahali zilikopelekwa fedha hizo,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Sh 1,377,534,000 ni miongoni mwa matumizi yasiyokuwa halali na saini zilizoigwa za Kimambo zimehusika na upotevu wa Sh 618,970,000; na Dk. Haule Sh 758,564,000 na mhusika akitajwa kuwa Maghimbi.

Ripoti hiyo inaeleza kwamba mtiririko wa fedha Wazalendo Saccos si mzuri na hivyo kushindwa kutoa huduma zinazotakiwa. Hadi Juni 2012 ilikuwa inadaiwa Sh 4,792,559,064 kutoka katika taasisi zilizoikopesha.

Marejesho ya mikopo kwenda nje kwa mwezi ya Sh 146,527,175.76 ambazo chama hicho kimeshindwa kulipa huku kikiwa na uwezo kurejesha Sh milioni 45 pekee ambazo nazo kimeshindwa kuzilipa na kuwakwepa wadai kwa kuacha kuweka fedha katika akaunti yake ya CRDB.

Chama hicho kimeshindwa kutekeleza baadhi ya vifungu vya sheria kutokana na ufisadi huo huku Sheria ya Ushirika Na. 20 ya mwaka 2003 na Kanuni zake za 2004 zikieleza kwamba chuo kilipojiingiza moja kwa moja kuwa mdhamini wa Saccos ndiyo ukawa mwanzo wa wizi wa fedha hizo.

Bodi, Menejimenti na Kamati ya Usimamizi iliyokuwa madarakani kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2012 ilimtumia Mtunza Fedha wa Chuo, Mwandambo, kufanya kazi za uhasibu upande wa Saccos na kumtambulisha rasmi benki kama mhusika wa utoaji na uwekaji fedha katika akaunti ya chama hicho.

Majina ya wanachama hewa na wengi wao si ya wafanyakazi wa chuo hicho, yaliingizwa na kupewa mikopo huku fedha hizo zikidaiwa kuwanufaisha watu wachache wakiwamo viongozi wa Saccos na wa chuo.

Ripoti ya uchunguzi ya Mrajis ilibaini madudu mengine ya chama hicho kwamba daftari la wanachama halikutunzwa ipasavyo, hivyo kushindwa kuelewa idadi kamili ya wanachama ambao ni watumishi wa chuo na wale wasiokuwa watumishi. Pia namba moja ilitolewa kwa mtu zaidi ya mmoja.

Bodi ya Uongozi na Menejimenti havikuwa na kumbukumbu sahihi za wanachama kwa mujibu wa Kanuni namba 27, 44 (n), 51 na 15.

Upotevu huo wa fedha unazihusisha moja kwa moja benki za KCBL, NMB, CRDB na KCB ambazo ziliidhinisha hundi za malipo kutoka Wazalendo Saccos bila kufanya uhakiki wa saini zilizowekwa kwa ajili ya kuchukulia fedha. Saini hizo zilikuwa tofauti na zilizokuwapo kwenye benki hizo.

Akaunti namba 4036600238 katika Benki ya NMB, kati ya Juni 13 hadi 17, 2008 kwa nyakati tofauti, Mwandambo alilipwa Sh milioni 115.8 kwa hundi zilizosainiwa na Maghimbi (aliyekuwa Mwenyekiti wa Saccos) na Dk. Haule.

Akaunti namba 01J104298101 iliyoko CRDB – Septemba 2008 kwa nyakati tofauti, Mwandambo alichukua Sh milioni 317.96 kwa hundi zilizosainiwa na Maghimbi, Dk. Haule na Kimambo.

Kutokana na wingi wa mikopo isiyozingatia utaratibu, baadhi ya wajumbe wa Bodi na Kamati ya Usimamizi na watendaji, wamekuwa wakichukua mikopo zaidi ya mara tatu na kufikia mara 31 kinyume na taratibu za uendeshaji wa Saccos na kutozingatia uwezo wa mkopaji kurejesha; na hivyo kuvunja Kanuni za Ushirika namba 90 (1), 94 (1) na 96.

Wengine wanaotajwa kwenye ripoti ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika wakihusishwa na upotevu wa fedha hizo ni Jasinta Tarimo, aliyekuwa Meneja wa Saccos, Shughuru akiwa Mtunza Hazina na Chuwa aliyekuwa Mtunza Fedha.

Tume iliyokuwa ikichunguza tuhuma za upotevu wa fedha hizo zilizokopwa na Saccos hiyo bila kuzingatia taratibu ikiwa chini ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika kati ya mwaka 2012 hadi 2013, ilibaini pia mkopo wa shilingi zaidi ya bilioni 1 kutoka kampuni ya Oiko Credit ambao ulikopwa kwa njia zisizoeleweka na uongozi wa chama hicho.

Mikopo mingine ambayo haikuzingatia taratibu iliyokopwa na Saccos hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja tu wa 2011 ni Sh milioni 316.97 kutoka NMB; Sh milioni 262 (KCBL) na Sh milioni 102.26 kutoka CRDB.

By Jamhuri