Tanzania inaelekea kuwa nchi ya watu walalamishi, wanaolia siku zote kulalamikia matatizo mbalimbali vikiwamo vitendo vya rushwa, ingawa wengi wao ni vinara wa kushawishi kutoa na kupokea rushwa. Cha kushangaza ni kwamba watoa rushwa ndio mara nyingi wamekuwa watu wa kwanza kulalamikia na kulaani uovu huo baada ya ‘kulizwa’ na wapokea rushwa katika mazingira mbalimbali.

Kwa mfano, hivi karibuni liliibuka tukio la vijana kadhaa waliodai wametapeliwa fedha na watu waliowaahidi kuwanyooshea mapito ya kupata ajira kilaini katika Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa. Hata hivyo, baada ya kuona ‘wameingizwa mjini’ vijana hao hao waliotoa rushwa ili wasaidiwe kuajiriwa katika vyombo hivyo vya dola, walijitokeza kulalamikia tukio hilo huku wakilitupia lawama Jeshi la Polisi na Serikali kwa jumla kwamba vimeshindwa kudhibiti vitendo vya rushwa.


Mmoja wa hao alitubutu kujitokeza na kutamka hadharani kwamba yeye alitapeliwa Sh 800,000, akiwa miongoni mwa vijana 90 waliotoa rushwa ya fedha kwa watu walioahidi kuwasaidia wasajiliwe na kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Polisi katika Chuo Cha Polisi (CCP) kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro.


Madai ya kutapeliwa kwa vijana hao waliotaka kujiunga na CCP kinyemela yamekuja miezi michache baada kuzuka madai mengine ya vijana wengine kadhaa waliodai wametapeliwa fedha na mke wa mmoja wa vigogo wa Jeshi la Polisi. Inadaiwa tapeli huyo aliahidi kuwasaidia vijana hao waajiriwe katika kitengo cha Usalama wa Taifa.


Kwa hakika inasikitisha kusikia kwamba baadhi ya Watanzania wamefikia mahali ambapo wameporomoka kimaadili kiasi cha kufikia hatua ya kutumia njia ya mkato kutafuta ajira na mafanikio mengine, hadi kwenye vyombo nyeti vya Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa.


Huu ni mzigo mkubwa wa ujinga kutafuta ajira za chee katika vyombo vya dola. Hiki ni kipimo tosha kinachodhihirisha kuwa baadhi ya Watanzania hawajizatiti kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kupata mafanikio, badala yake wamejenga kasumba ya kutumia ‘njia za panya’ kutafuta maisha.


Pamoja na kweli usiopingika kwamba hali ya maisha nchini inaendelea kuwa ngumu mithili ya jiwe, lakini hicho hakiwezi kutumiwa na watu kama kigezo cha kufanya makosa ya kutoa na kupokea rushwa kwa ajili ya kupata ajira Polisi, Usalama wa Taifa na kwingineko kinyume cha sheria na taratibu halali.


Ni wazi kuwa vijana walioshawishi na kutoa rushwa pamoja na matapeli walioshawishi kuomba na kupokea rushwa hiyo, wote ni wahalifu wanaostahili adhabu kwa mujibu wa sheria. Juhuzi zaidi zinahitajika kukabili vitendo vya rushwa kwani ni miongoni mwa vikwazo vikuu vya maendeleo endelevu katika Taifa letu.


Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinapaswa kuendeleza umakini mkubwa katika kuajiri watumishi au watendaji wake kuepusha mwanya wa kenge kujiunga kwenye msafara wa mamba.


Waajiriwa wapatikane kwa sifa na vigezo vilivyowekwa. Njia za mkato, panya, milango ya nyuma, upendeleo wa udugu, ukabilia, udini na vitendo vya rushwa vidhibitiwe kwa nguvu kubwa wakati wa kuajiri watumishi wa umma.


Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliasisi Taifa hili katika misingi ya utumishi uliotukuka. Enzi za uongozi wake watumishi wa umma walifanya kazi kwa uadilifu, uaminifu, juhudi na maarifa. Hapakuwepo na watu wavivu waliokuwa na uchu wa kupata ajira na madaraka pasipo kufanya kazi kwa bidii huku wakifuata taratibu na sheria za nchi.


Kasumba ya baadhi ya watu kutofuata taratibu ndiyo imekuwa kikwazo cha mafanikio ya wengi, hususan vijana ambao hujiingiza katika vitendo vya uhalifu ukiwamo huo wa kutoa rushwa wapendelewe kuajiriwa huku wakijua hawakidhi masharti, sifa na vigezo vya kupata ajira wanazozitaka.


Matokeo yake ndiyo kama hayo ya mtu kutapeliwa hadi kiasi cha Sh 800,000 ambazo angezitumia kujigharimia mahitaji muhimu.


Ndio maana ninawafananisha vijana waliofanyiwa utapeli huo na wagonjwa wa ujinga mkubwa kwa sababu sifa na taratibu za kujiunga CCP-Polisi na Usalama wa Taifa zinajulikana kutokana na kutangazwa mara kwa mara kila inapohitajika, lakini wao kwa makusudi wakaamua kukiuka taratibu na kutaka kuajiriwa katika vyombo hivyo kwa njia ya mkato. Huo ni ujinga mkubwa. Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa siyo vichaka vya kila mtu kama ambavyo vijana hao walidhani.


Ni vyombo vinapaswa kutumikiwa na watu wenye waadilifu na wenye sifa zinazotakiwa. Kama wapo wachache walioajiriwa katika vyombo hivyo kupitia mazingira ya rushwa kuna siku wataumbuliwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa kisheria. Ifahamike kwamba vijana waliotoa rushwa ya fedha kwa ajili ya kufanyiwa mipango ya kuajiriwa katika vyombo hivyo vya dola huku wakijua hawana sifa zinazotakiwa, walifanya kosa la jinai na wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria. Kama ambavyo wanataka waliopokea rushwa yao hiyo waadhibiwe kisheria, na wao pia watambue wanastahili kushitakiwa maana mtoa na mpokea rushwa wote ni wahalifu.


Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (ASP) Advera Senso, tayari amewakumbusha wananchi kutambua kwamba mfumo wa ajira ndani ya Jeshi la Polisi unafuata kanuni na taratibu zake, si vinginevyo.


Aidha, ASP Senso ametoa wito kwa wote wenye malalamiko ya kutapeliwa na kutoa rushwa ya fedha kwa ajili ya kupatiwa ajira wajitokeze kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi unaoweza kufanikisha ushahidi wa kuwatia hatiani waliowafanyia utapeli huo.


Ugonjwa wa ujinga uliodhihirika kwa vijana waliotapeliwa na kutoa rushwa ya fedha ili wasaidiwe kupata ajira katika Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa, uwe fundisho na onyo kwa wengine wanaotaka kutenda kosa la aina hiyo.


Jamani, rushwa ni adui wa haki zetu, sote tushirikiane kuipiga vita kwa nguvu kubwa. Kwa pamoja tunaweza.

1455 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!