Tofauti na wanasoka, hasa washambuliaji mahiri wanaocheza Ligi Kuu za Ulaya kama Hispania, England na Ufaransa, straika wanaocheza Ligi Kuu ya Soka hapa nchini mara zote wameonesha kuwa wa msimu mmoja, siyo vinginevyo.
Mathalani, aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga na Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) na kuibuka kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Soka ya Vodacom Tanzania Bara mwaka 2010/2011, Mrisho Ngassa, hakuwemo kwenye orodha ya washambuliaji waliofunga angalau mabao matatu hadi ulipomalizika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kwa msimu uliopita.

John Bocco ‘Adebayor’, mshambuliaji wa Azam FC aliyeibuka kinara wa ufungaji wa ligi hiyo msimu huo, ndiye alifungana mabao na mshambuliaji wa Yanga aliyetemwa msimu huu, Kenneth Asamoah, hadi ulipomalizika mzunguko wa kwanza.

Kila mmoja alizifumania nyavu za timu pinzani mara nane, huku mshambuliaji mwingine wa Azam FC, Gaudence Mwaikimba, akifunga mabao sita akifuatiwa na Emmanuel Okwi wa Simba aliyefunga matano.

Tofauti na msimu uliopita ambapo Bocco na Mwaikimba walikuwa kwenye chati, hali ya kwa sasa hairidhishi.

Hadi mzunguko huo wa kwanza unamalizika, Bocco alikuwa ametikisa nyavu mara tatu, huku Mwaikimba akiwa kama hayupo hata kwenye ligi na makocha wa Azam FC ‘hawana habari’ naye yoyote. Amekuwa akiingia uwanjani kwa kutokea benchi tena kwa nadra, nafasi ambayo bado ameshindwa kuitumia vyema.

Ligi hiyo ina timu 14 baada ya Polisi ya Dodoma, Villa Squad na Moro United kushuka daraja na nafasi zake kuchukuliwa na Polisi Morogoro, Tanzania Prisons na JKT Mgambo.

Timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo ni mabingwa watetezi, Simba, Yanga, Azam FC, Mtibwa Sugar, Coastal Union, Kagera Sugar, Ruvu Shooting, JKT Ruvu, African Lyon, Toto African na JKT Oljoro.

Mshambuliaji wa kulipwa wa Yanga, Didier Kavumbagu na wa Azam FC, Kipre Tchetche ndio wanaongoza kwa kupachika mabao manane kila mmoja hadi mzunguko huo wa kwanza unamalizika.

Hao wanafuatiwa na Amir Omar wa JKT Oljoro na Seif Rashid wa Ruvu Shooting ambao wamefunga mabao sita kila mmoja huku Felix Sunzu na Amri Kiemba (Simba), Daniel Lyanga (Coastal Union) na Hussein Javu (Mtibwa Sugar) wakitikisa nyavu mara tano kila mmoja.

Wakati Kavumbagu na Tchetche wameshafanya kama Bocco na Asamoah msimu uliopita, hali ni tofauti na ilivyo kwa Ligi Kuu za Ulaya, hususan za Hispania, England na Ufaransa.

Straika ambao wanaongoza kwa upachikaji mabao kwa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), Lionel Messi na Cristiano Ronaldo ambao pia msimu uliopita waliongoza kwa kutikisa nyavu hata sasa wanatesa kileleni.

Tayari timu zao zimeshacheza mechi 12 huku zikiwa nyuma kwa timu zote za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, ambapo zenyewe zimeingia uwanjani mara 13. Messi ndiye anaongoza kwa kupachika mabao 17 akifuatiwa na Ronaldo (mabao 12) na Radamel Falcao wa Atletico Madrid (mabao 10).

Hiyo inaonesha ukimwondoa Ronaldo, wenzake wote viwango vyao vimepanda kwani msimu uliopita Messi alifunga idadi hiyo ya mabao katika mechi 16 na Falcao alitikisa nyavu mara tisa.

Aidha, mshambuliaji wa timu ya Paris Saint-German (PSG) ya Ufaransa, Zlatan Ibrahimovic, ndiye anaongoza kwenye orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu ya Ufaransa kwa mabao 10 kutokana na mechi 13 alizocheza.

Hivyo, Ibramovic anaonesha kiwango chake kimepanda kwani katika msimu uliopita, wakati huo akiichezea AC Milan ya Italia alifunga mabao 12 katika mechi 18, hali ambayo ni kinyume cha wachezaji wa Ligi Kuu ya Tanzania bara ambao kila msimu viwango vyao hushuka.

Mbali ya Hispania na Ufaransa, Robin van Persie wa Manchester United ya England ambaye alimaliza Ligi Kuu ya nchi hiyo msimu uliopita akiwa kinara wa mabao, hivi sasa amefunga mara nane katika mechi 12 alizocheza.

Lakini kati ya wote, mshambuliaji mpya wa Liverpool, Luis Suarez ambaye msimu uliopita hakuwa lolote wala chochote, ndiye anaongoza hivi sasa katika ufungaji kwenye ligi hiyo. Tayari amewapeleka marikiti mara 10 makipa kutokana na mechi 12 alizocheza.

Washambuliaji wengine wa Ligi Kuu za Ulaya ambao pia viwango vyao vimepanda ama havijashuka kama inavyokuwa kwa washambuliaji wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ni pamoja na Demba Ba wa Newcastle United na Maroune Fellani wa Everton za England.

Wengine ni Pierre Emerick wa Saint Etienne, Wissam Ben Yedder (Toulouse), Yoan Gouffran (Girondins Bordeaux), Bafetimbi Gomis (Olympique Lyon) na Mevlut Erding (Stade de Rennes), zote za Ufaransa.

Washambuliaji waliopanda viwango au kubaki kama vilivyokuwa msimu uliopita ndani ya La Liga nchini Hispania ni Aduriz wa Atletico Bilbao, Tomer Hemed (Real Mallorca), Alvaro Negredo (Sevilla), Gonzalo Higuain (Real Madrid), Ruben Castro (Real Betis), Helder Postiga (Real Zaragoza) na Oscar (Real Valladolid).

Kulewa sifa, kuendekeza starehe zikiwamo za unywaji pombe, kupunguza mazoezi, kudharau makocha na viongozi wa timu, ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kuporomosha viwango vya washambuliaji wanaocheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Wshambuliaji jirekebisheni.

 

By Jamhuri