Tatizo la ajali za barabarani limekuwa ni moja ya changamoto kubwa sana katika sekta ya usafiri wa barabara hapa nchini. Katika kipindi cha mwanzo wa mwezi Septemba, 2014 kumetokea ajali za barabarni kubwa zaidi ya mbili katika mikoa ya Mara na Tabora, ambako watu zaidi ya 40 walipoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa.

Aidha, takwimu zinaonesha kuwa ajali zimeongezeka kutoka matukio 23,578 ya ajali za barabarani kwa mwaka 2012 hadi kufikia matukio 23,882 yaliyotokea mwaka 2013. Hali hii inatakiwa kudhibitiwa kwa hatua za makusudi kuchukuliwa na wadau mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hili.

Kati ya wadau muhimu ambao wana nafasi kubwa ya kuchangia katika kupunguza ajali za barabarani, ni wamiliki wa mabasi au waendeshaji wa kampuni za mabasi.

Mengi yameelezwa kuhusu visababishi vya ajali na vinafahamika lakini hatua madhubuti hazijachukuliwa.  Kwa mujibu wa tafiti na takwimu zilizopo, imebainika kuwa dereva ndiyo chanzo kikuu au kisababishi cha ajali kwa asilimia 55.

Baadhi ya makosa yanayofanywa na madereva ni pamoja na kwenda mwendo kasi, kupakia abiria kuzidi kiwango, kuendesha gari huku wamelewa pombe, kutokufuata sheria za usalama barabarani, kutokuwa na ustadi wa kuendesha magari ya abiria na kutoheshimu watumiaji wengine wa barabara.

Ubovu wa magari unachangia asilimia 16 na mazingira ya barabara asilimia saba.  Lakini kwa ujumla wake, makosa yanayohusiana na binadamu katika kusababisha ajali, mchango wake ni asilimia 77.

Kwa kuwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wanavifahamu visababishi hivyo vya ajali, mimi ninaona wanao uwezo wa kudhibiti wafanyakazi wao, wanawajibika kutengeneza magari yao ili yawe katika ubora na wana nafasi ya kuamua  kuwaadhibu madereva au la, kutokana na makosa yanayoweza kuhatarisha usalama na maisha ya abiria na mali zao.

Katika utaratibu wa utoaji leseni za biashara ya usafirishaji abiria, wamiliki ndiyo wanaopewa leseni inayoambatana na masharti ya jinsi ya kutoa huduma ya usafirishaji.  Wamiliki ndiyo wanaopewa ratiba ya safari na kutoa maelekezo kwa madereva.  Kutokana na utaratibu huo, ni rahisi kwa mmiliki kumtambua dereva mkorofi ambaye anakiuka masharti ya leseni kwa kutokufuata ratiba za basi analoendesha ambayo inaashiria kuwa mhusika anaendesha kwa mwendo kasi.

Kwa mujibu wa masharti ya leseni ya usafirishaji inayotolewa na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), mmiliki wa basi kupitia  kwa wafanyakazi wake —  kondakta na dereva — wanao wajibu  wa kuhakikisha kuwa abiria anafikishwa salama  kwenye kituo  cha mwisho  wa safari  yake kwa mujibu wa mkataba wa tiketi.  Wajibu wa abiria  ni kulipa  kiwango halali cha nauli kwa safari husika.

Wajibu wa kwanza wa mmiliki wa chombo ni kuhakikisha usalama wa gari na abiria.  Wajibu wa Serikali kupitia vyombo vyake ni kuhakikisha msafirishaji anatimiza wajibu wake kwa mujibu wa masharti ya leseni na sheria za usalama barabarani.

Madereva au makondakta ni wakala tu wa mwenye gari na hawapunguzi mzigo wake inapotokea makosa ya wakala wake.  Kutokana na hali hiyo makosa yanayofanywa na madereva humuangukia mmiliki.

Hivyo basi, uendeshaji wa kizembe unaofanywa na dereva aliyeajiriwa kufanya safari kati ya mji na mji, unaweza kuunganishwa na makosa mengine na kumhusu mwenye gari aliyemuajiri.  Hii ni tofauti pale dereva anaposhuka kumpiga au kumtukana abiria.

Kama dereva anaendesha mwendo kasi ili awahi kufika kituo alichopangiwa, anaweza kuadhibiwa yeye mwenyewe na mwenye gari hasa pale anaposababisha ajali.

Ili kuepukana na hali hiyo, ni lazima kwa mmiliki wa gari kuwa na mamlaka kamili ya kumdhibiti dereva au kondakta wake kwa matendo yale yasiyoendana na maadili ya udereva au sheria za usalama barabarani.

Ni lazima mwenye gari amtambue na kumsimamia dereva aliyemkabidhi gari, vinginevyo mamlaka husika itachukua hatua kali zenye athari kwa wamiliki na biashara yao ya usafirishaji.

Kwa mujibu wa Sheria ya Leseni ya Usafirishaji, 1973 na Sheria ya Sumatra, 2001, Sumatra imepewa uwezo  wa kufuta au kusimamisha leseni ya msafirishaji endapo itaridhika kuwa kuna ukiukwaji wa masharti ya leseni.

Hata hivyo, kwa msingi wa utawala bora wa sheria, wamiliki wa vyombo hunyang’anywa leseni au kufutiwa njia kwa kuelezwa sababu zilizoleta uamuzi huo.

Kwa upande wa Sumatra, hatua kadhaa za dhati zimechukuliwa ili kukabiliana na matatizo ya usafirishaji ikiwa ni pamoja na ajali za barabarani.  Kama mdhibiti, Sumatra imekuwa ikitumia nyenzo mbalimbali ambazo kwa kiwango kikubwa zimesaidia katika kudhibiti sekta hii ya usafirishaji.

Leseni ni moja ya nyenzo muhimu ambayo Sumatra inatumia kusimamia au kufuta leseni kwa wanaokiuka masharti yake. Sumatra imetengeneza kanuni na taratibu ambazo zimelenga kuinua ubora wa huduma, usalama na nidhamu katika utoaji wake, zinaainisha pia adhabu zinazolingana na makosa.

Moja ya kanuni hizo ni Kanuni za Usafirishaji abiria (Passenger Road Transport Regulations), 2007. Maeneo muhimu ambayo kanuni hizi imeyatilia maanani ni pamoja na kila mwenye kuomba leseni ya usafirishaji kuwasilisha picha  na majina ya madereva na leseni zao pamoja na nyaraka nyingine, ili kuhakikisha kuwa mabasi yanaendeshwa na madereva wenye sifa na waweze kutambuliwa na askari wa usalama barabarani.

Wamiliki wa magari watawajibika kuwasilisha hati ya kuandikisha kampuni/biashara ya usafirishaji na ‘Memorandum or Articles of Association’ na mtu binafsi atatoa maelezo ya mmiliki na picha zake. Utaratibu huu utaimarisha udhibiti wa watu hawa wawili, yaani dereva na mmiliki ambao wanaweza kusaidia kupunguza ajali.

Aidha kanuni imebainisha kuwa safari yoyote itakayochukua zaidi ya saa 12 lazima kuwe na madereva wawili kupokezana ili kuongeza umakini kudhibiti ajali zinazotokana na uchovu wa madereva.  Mfano wa njia zinazohitaji zaidi ya dereva mmoja ni kama njia ya Arusha-Mbeya, Mwanza-Dar es Salaam.

Kutokana na kuwapo idadi kubwa  ya magari ya abiria ambayo ni machakavu na mengine kuwa na bodi zilizojengwa kiholela hivyo kuwa chanzo cha kuongezeka kwa ajali na maafa yake, Sumatra kupitia  kanuni hizi imesitisha utoaji leseni ya kusafirisha abiria kwa gari/basi lenye umri zaidi ya miaka 5 tangu liundwe.

Ili kuleta nidhamu na kupunguza makosa na madhara yanayosababishwa na uzembe ya kutozingatia sheria na kanuni za usafirishaji, viwango vya adhabu vimepandishwa kutoka kati ya Sh 50,000 na Sh 100,000 za zamani kwa kosa moja, hadi Sh 200,000 na Sh 500,000 kwa kosa.

Adhabu hizo zinaweza kuendana na vifungo. Adhabu hizo bado haziondoi uwezo wa Sumatra kufunga, kusimamisha au kufuta leseni ya mmiliki kwa njia moja au njia zote Tanzania bara.

Usimamizi endelevu wa kanuni hizi zote, pamoja na mikakati mingine ya Jeshi la Polisi, mshikamano wa wasimamizi, uboreshaji wa miundombinu na nidhamu ya madereva, tutaweza kupambana kikamilifu na balaa la ajali.

Wamiliki wana jukumu la msingi la kuhakikisha vyombo vyao vinakidhi viwango vya ubora na usalama ili kudhibiti wimbi la ajali katika nchi yetu.

Mwandishi wa makala hii ni David Mziray-Meneja Mawasiliano kwa Umma wa Sumatra. Amejitambulisha kuwa ni msomaji mahiri wa gazeti hili na anapatikana kwa namba za simu 0713 250550 na 0800110019/20. Hii namba ya pili huduma yake inapatikana bila kukatwa fedha za muda wa maongezi.

1975 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!