Baada ya kununua basi dogo (Hiace) la kwanza na kulisajili daladala, nilikutana na ulimwengu mpya wa changamoto za biashara za magari. Changamoto zilipozidi niliazimu kukutana na walionitangulia kwenye biashara hiyo ili nipate hazina ya ushauri.

Nikamfuata mzee wangu mjini Iringa aliyeanza biashara ya kusafirisha mizigo na abiria mwaka 1978. Mzee wangu baada ya kunisikiliza aliniambia sentensi moja tu na akasema huo ndiyo ushauri anaonipa na ambao utanisaidia. Alisema hivi, “Kijana wangu, ili umudu biashara ya magari hasa hizi daladala unatakiwa uwe mjeuri-jeuri kwa madereva, makondakta na wakati mwingine kwa matrafiki.”

 

Nikataka anipe ufafanuzi kuhusu hili, ndipo akaongeza ufafanuzi, “Hawa watu ninaokwambia usicheke nao ndiyo wanaoweza kukuliza ama kukufanya ufurahi. Ukizubaa katika hili usishangae kujikuta muda umepita, gari limechakaa na fedha za kununulia gari jingine huna.” Ushauri wa mzee wangu huyu niliufanyia kazi na ulizaa matunda.

 

Uzoefu wangu katika biashara hii ya daladala unachagizwa pia na nafasi ya uongozi niliyopata kushika kuanzia mwaka 2009 hadi Januari 2012. Nilikuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi ya Abiria Mkoa wa Iringa kinachojumuisha magari yote ya abiria ukiacha mabasi ya mikoani yaliyo chini ya TABOA. Nafasi hii iliniwezesha kufahamiana na kushirikiana na wafanyabiashara wengi wa magari ya abiria Iringa.

 

Hivyo nafahamu chungu na tamu za biashara ya daladala. Machozi yao nayajua. Ukiacha changamoto ya faida (ambayo nitaichambua kwa kina kwenye makala haya), biashara ya daladala ina “timbwili-timbwili” si mchezo. Madereva wanasumbua sana, faini za barabarani zisizoisha na uharibifu wa magari ni kama chachandu chungu kwenye biashara hii. Kati ya biashara nilizowahi kufanya, biashara ya daladala inaongoza kwa kupasua kichwa.

 

Miezi machache iliyopita wamiliki wa daladala Dar es Salaam waliwasilisha kusudio la kupandisha nauli za daladala kwa asilimia 300 mbele ya Baraza la Watumiaji wa Huduma za Usafiri. Baraza hilo pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) waliwagomea kwa sababu mbalimbali. Moja ya sababu hizo ni pamoja na mosi; wamiliki wa daladala walishindwa kuwasilisha taarifa za kifedha za biashara zao (Approved financial statements).

 

Pili, sababu walizozitoa kuhusu kupanda gharama walidai zilikuzwa mno na kukosa ushahidi wa bei katika soko. Baada ya kufuatilia mnyukano ule niliwahurumia sana wamiliki wa daladala kwa sababu wenye rungu la kuwasaidia hawajui viatu vya umiliki wa daladala vinavyobana na kuumiza.

 

Nimetafiti biashara hii katika mikoa ya Mbeya, Morogoro na Dodoma; huku Iringa nikiwa nimeifanya kwa vitendo. Sehemu karibu zote changamoto zinafanana ingawa kuna tofauti ndogo ndogo kutegemea na utamaduni wa maeneo. Sehemu hizi zote viwango vya fedha inayolazwa ni shilingi kati ya Sh 30,000 na 40,000 kwa siku kwa mabasi madogo (Hiace Super Roof). Kwa mabasi ya kati (Coaster) kiwango kwa siku ni kati ya Sh 50,000 hadi Sh 80,000 kwa siku. Sasa twende kimizania ya uhasibu hapa.

 

Bei ya kununua basi dogo (Toyota Hiace Super Roof) pamoja na kusajili leseni, njia, na taratibu zote ili ianze biashara ni kati ya Sh milioni 20 hadi Sh milioni 25. Bei ya kununua basi la kati (Coaster) ni kati ya Sh milioni 35 hasi Sh milioni 45. Magari hayo yote ni mitumba kutoka Japan.

 

Tukokotoe hesabu ya basi dogo. Kwa upande wa mapato kama gari inalaza Sh 30,000 kwa siku ina maana kwa mwezi unakusanya Sh 840,000. Hesabu hizi ni kwa siku 28. Siku mbili kwa kawaida hutengwa kwa ajili ya kufanya ‘service’ ya gari inayofanyika kwa mwezi mara mbili – yaani kila baada ya siku 14. Tushuke kwenye matumizi.

 

Galoni moja ya kilainishi kizuri (oil) ni Sh 45,000, gharama ya kubadilisha sahani za breki ni Sh 25,000; vifaa ambatanishi vya ‘service’ ni karibu Sh 20,000. Ukichanganya na ufundi na ikiwa unafanya ‘service’ ya uhakika katika gari lako kila ‘service’ moja unatumia Sh 100,000 kwa makadirio ya chini sana. Katika kipengele cha ‘service’ kwa mwezi unatumia kama Sh 200,000.

 

Mshahara wa dereva kwa mujibu wa sheria za Sumatra zinazoambatana na masharti ya kupewa leseni, yanakutaka mmiliki wa gari ulipe kuanzia kima cha chini cha mshahara wa sekta binafsi ambao ni Sh 80,000. Kodi za serikali ikiwamo leseni ya barabara, leseni ya njia, zimamoto, mapato na ushuru wa manispaa/jiji ni wastani wa Sh 65,000 kwa makadirio ya chini.

 

Kodi hizi nyingi zinalipwa kwa mwaka, lakini hapa nimezigawanya katika mafungu ya miezi 12. Mwisho tujumlishe mshahara wa wewe mjasiriamali unayemiliki gari. Najua wajasiriamali wengi hawana utaratibu wa kutenga mishahara yao kwa biashara zao, lakini hata kama hutengi mshahara tukadirie kuwa unajilipa Sh 80,000 kwa mwezi.

 

Sasa ukichukua mishahara ukajumlisha na kodi ukajumlisha na gharama za matengenezo unapata matumizi ya Sh 420,000. Kwa haraka haraka unaweza ukadhani faida inayobaki ni Sh 420,000. Hapa ndipo wafanyabiashara wengi wa magari wanapofilisikia kwa kusahau jambo la muhimu kuliko yote.

 

Jambo hili la muhimu ni gharama ya uchakavu wa gari (depreciation cost). Gharama hii kitaalamu hutakiwa kujumuishwa kwenye kipengele cha matumizi. Tunaposema gharama ya uchakavu ni pale unapoelewa kuwa ikiwa gari linatembea, basi matairi yanazi kwisha, vyuma vinasagika na bodi inachakaa. Kinachoamua kiwango cha gharama ya uchakavu ni makadirio ya muda ambao gari lako litakaa kabla ya kuchakaa kabisa.

 

Kuna njia kadhaa za kitaalamu lakini hapa nataka nitumie njia rahisi ya “kijasiriamali” ili tuelewe vema. Mathalani, kama gari lako linapita kwenye barabara nzuri unaweza kukadiria kuwa uhai wa gari hilo utakuwa ni miaka mitano. Unachofanya unachukua thamani ya kununulia hadi kusajili gari ianze biashara, kisha unagawanya kwa miaka mitano.

 

Twende pole pole hapa. Tumesema wastani wa chini wa basi dogo ni Sh milioni 20 hadi ianze biashara. Ukichukua Sh milioni 20 ukagawanya kwa miaka mitano unapata Sh milioni 4 ambazo ndiyo gharama ya uchakavu kwa mwaka. Sasa chukua Sh milioni hii 4 kisha gawanya kwa miezi 12 unapata wastani wa Sh 333,000.

 

Fedha hizi tunaziingiza kwenye sehemu ya matumizi. Kwa maana hiyo jumla kuu ya matumizi yetu kwa mwezi inakuwa ni Sh 753,000. Ili uelewe faida halisi (net profit) unayozalisha kwa mwezi chukua mapato ya mwezi (Sh 840,000) kisha utoe na matumizi ya mwezi (Sh 753,000). Ukikokotoa hapo utaona faida halisi ya biashara ya daladala ikiwa una basi dogo kwa mwezi ni Sh 87,000 tu!

 

Najua hesabu hizi zitawashtua wengi watakaoshindwa kuzielewa na kwa kutozielewa wanaweza wasizikubali. Bahati nzuri ni kuwa nimeshafanya biashara hii huku nikiwa na digrii ya biashara kutoka chuo kikuu, hivyo naelewa ninachokisema hapa. Labda nitafsiri maana ya hesabu hizi za hapo juu kwa lugha nyepesi na ya picha.

 

Iko hivi; ukinunua gari la Sh milioni 20 leo, baada ya miaka mitano linaweza kuwa limeshachakaa kabisa. Wakati huo gari litakapochakaa unatakiwa uwe na fedha mkononi za kununua gari jingine kutoka katika biashara hiyo hiyo na ubakiwe na fedha nyingine ambayo ndiyo tutaiita “faida”. Zile fedha utakazorudishia gari lililochakaa ni mtaji ulioanza nao!

 

Kwa hesabu hizo hapo juu ambako tumeona faida halisi ya daladala ikiwa unamiliki “Hiace Super Roof” ni Sh 87,000. Kwa faida hiyo, itamkuchukua mjasiriamali miaka 19 ili afanikiwe kununua gari jingine la pili! Mliowahi kufanya biashara ya daladala mtakubaliana nami kuwa ukiona mtu ameongeza daladala ya pili ndani ya mwaka mmoja au miwili, basi uwe na uhakika kuwa fedha ya kununua gari la pili hajaitoa kwenye gari la kwanza kwa asilimia 100. Ni ama, amechukua mkopo, au fedha ameongezea kutoka vyanzo vingine.

 

Naomba nieleweke vema hapa. Sisemi kuwa biashara ya daladala hailipi, la hasha! Lakini faida halisi iliyopo kwenye daladala ipo tofauti sana na vile Sumatra na abiria wanavyoitazama au kuifikiria. Mtazamo na mawazo ya wadau hawa ndiyo yamekuwa yakisababisha kuwakatalia wenye daladala au kuwakubalia kwa mbinde kila wanapotaka kuidhinishiwa kupanda kwa nauli. Kumiliki daladala yataka uwe na moyo wa chuma!

 

Mathalani, kilainishi ambacho mwaka 2006 kilikuwa kikiuzwa Sh 19,000 leo kinauzwa Sh 45,000. Tairi ambalo wakati huo liliuzwa Sh 85,000 leo linauzwa Sh 165,000. Gari lililokuwa linauzwa Sh milioni 12 mwaka 2006 leo linauzwa Sh milioni 22 (Toyota Hiace Super Roof). Kwa mabadiliko hayo, nauli za daladala zilitakiwa zipande kwa asilimia 236. kutoka mwaka 2006 hadi leo.

 

Lakini hali ni kinyume, kwani maeneo mengi nauli ya daladala imeongezeka kwa kati ya Sh 50 hadi Sh 100 ongezeko la kati ya asilimia 25 hadi 50 tu. Ndiyo maana Sumatra na Baraza la Watumiaji walipowagaragaza wamiliki wa daladala kwa kufutilia mbali madai yao ya kupandisha nauli nilijichekea na kusikitika tu. Hata hivyo, sina neno na wala sina lawama kwa Sumatra wala Baraza la Watumiaji, kwa sababu wenye daladala wenyewe walishindwa kutoa utetezi wenye nguvu za hoja.

 

Ukitaka kuanza biashara ya daladala ni vema ukayajua haya. Tukutane wiki ijayo!

 

[email protected] 0719 127 901

 

By Jamhuri