Wana Kagera tuungane kuifufua KCU

Kufuatia makala zangu nilizoandika kuhusu Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera (KCU), ambacho sidhani kama nitakuwa nimekosea kukiita marehemu, nimepokea maoni mbalimbali, mengi yakitaka niachane na mambo ya kuandika kuhusu chama hicho. Lakini leo nimeona niandike tena.

Kusema ukweli uliokuwa ushirika, maana kwa sasa ni kama haupo tena,  ulikuwa  mboni ya Wana Kagera. Umetoweka na kuwaacha vipofu! Kwa hiyo kama wanataka kuona tena, Wana Kagera hawana budi kuungana ili kukifufua chama hicho, kwa sababu ni kama tayari kimekufa kabisa, kasoro hakionekani kimezikwa wapi.

Ni jambo la kusikitisha sana kuona chama kikubwa kama KCU kinayeyuka kijinga namna hiyo. Kwa sababu nikirudi nyuma mimi mwenyewe ni zao la chama hicho tangu kikiitwa Bukoba Cooperative Union (BCU).

Chama hicho kilikuwa na kitengo chake kilichoitwa Balimi Education Fund, ambacho kilikuwa kinawalipia wanafunzi wote ambao wazazi wao walikuwa ni wakulima wa kahawa na ni wana ushirika.

Nilisoma elimu ya sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne, shule ya kulipia, pesa ikitolewa na chama hicho. Pamoja na hiyo, mzee mmoja mhandisi wa ndege, aliwahi kunieleza jinsi alivyosoma Uingereza masuala ya uhandisi akilipiwa na chama hicho. Aliniambia suti ya kwanza kuivaa alipokuwa akisafiri kwenda ng’ambo alinunuliwa na chama hicho.

Zaidi ya hapo watu wote ambao waliifanya Bukoba ikajulikana kama sehemu ya watu “Nshomile” hakuna hata mmoja ambaye atakosa kuitaja BCU kwamba ndiyo iliyoweka mkono wake katika kumfanya hivyo alivyo.

Mbali na elimu, wananchi wa Mkoa wa Kagera wameweza kuboresha maisha yao kupitia chama hicho. Wameongeza ukubwa wa mashamba yao, wamejenga kwa kukiangalia chama hicho. Wamenunua magari, pikipiki, baiskeli na kadhalika wakiwa wanakitumia chama hicho.

Kwa mantiki hiyo, ni nani asiyeona kuwa chama hicho kimetoa mchango wa aina yake katika kuinua uchumi wa watu wa mkoa huo kwa kiwango kikubwa?

Mwanzoni chama hicho kilikuwa na shule, kikianza na Shule ya Sekondari Balimi, ambayo mwaka 1979 ilipanuka na kugawanyika katika shule tatu, yaani Kishoju,  Kashozi na Mugeza.

Sina uhakika kama shule zote zinafanya kazi, ila shule moja ya Kishoju ambayo ilijengwa kwa pesa ya chama hicho cha ushirika, ilisalimishwa serikalini baada ya chama hicho cha ushirika kushindwa kuihudumia.

Ni kwa nini chama hicho kikashindwa kuihudumia shule hiyo? Panahitajika maelezo ya kina.

Mambo hayo yamewagusa wengi, na mmoja wa watu walioguswa sana akiyashangaa mabadiliko hayo ya kujitakia ni mzee Archard Felician Muhandiki. Huyo ni mtu ambaye kila akifikiria jinsi wakulima wa Kagera walikokuwa wamefikia kimaendeleo na hali yao ilivyo kwa wakati huu, anachanganyikiwa kiasi cha kukosa hata usingizi.

Anabaki kuangalia kwa masikitiko jinsi mchwa ulivyoingilia miundombinu ya maendeleo ya Wana Kagera na kuitafunilia mbali kiasi cha kuiacha bila mizizi, hivyo maendeleo kubaki tu kwenye historia.

Alijaribu kuingia kwenye uongozi wa chama hicho ili kutoa mbinu ambazo zingeweza kukinusuru kutokana na  maangamizi yaliyokuwa yanakinyemelea,  baadhi ya watu wakamzunguka na kumpiga vita ili atoke na aende zake.

Muhandiki ni mtaalamu wa masuala ya vyama vya ushirika ambaye alikuwa akishughulika na vyama vya aina hiyo katika nchi tatu, yaani Kenya, Uganda pamoja na Tanzania, akiangalia na kukagua jinsi vinavyopokea malipo, matumizi ya pesa na kadhalika.

Mtu wa aina hiyo kumpata anatakiwa alipwe pesa ‘kubwa’, ambapo hapa nchini iliundwa COASCO ambayo nayo kwa sasa  ina tuhuma tele. Lakini kwa upande wa KCU ilikuwa imempata bure, ila haikuona umuhimu wake au haikujua utaalamu alionao, hivyo kuamua kumsukumia mbali.

Kuna mtu mmoja ambaye sijui ni kwa nia nzuri au la, amenitumia ujumbe akinitaka nimpe Muhandiki ushauri wa nini cha kufanya kuona namna ya kuifufua KCU.

Tunaelewa kwamba mabadiliko haya ya ghafla yaliyo machafu kwa wakulima wote wa kahawa wa Kagera hayakunyesha kama mvua, ni mabadiliko yaliyo na watu walioyasababisha nyuma yake. Kwa mantiki hiyo Muhandiki si kwamba kazi ya kuufufua ushirika huo inaweza kumuwia nyepesi hata kidogo, ni kazi inayohitaji jumuiko la wakulima wote wa kahawa wa Kagera.

Tayari wapo wanaomuunga mkono Muhandiki, wakijitokeza wote anaweza kuwa na nguvu za kutosha na kuamua lililo la maana. Ni kwa faida ya wote, wala si kwa ajili ya Muhandiki pekee.

Kama aliweza kuhudhuria vikao vya chama hicho akitokea Dar es Salaam bila kukosa, tena bila kuhitaji posho, mtu atakosaje kuuona uchungu aliokuwa nao Muhandiki katika kutetea masilahi ya chama hicho kikuu cha ushirika?

[email protected]

0654 031 701