Tazama kile kisichofanywa na wengine na ukifanye

Kila unakopita, kila unakokwenda utakutana na watu wanafanya mambo yanayofanana. Kufanya mambo yanayofanana na wengine ni ishara kuwa unachokifanya kina ushindani mkubwa. Kanuni za biashara zinasema, kama wazalishaji ni wengi, wanunuzi wanakuwa wachache na matokeo yake faida itakuwa ndogo.

“Unakuwa tajiri kwa sababu unafanya mambo ambayo watu wengine hawawezi kufanya. Mafanikio yanahitaji kujitoa. Lazima uwe tayari kujitoa,” ni maneno ya Robert T. Kiyosaki, mtaalamu wa mambo ya fedha na uchumi.

Moja ya kitu kitakachokuweka nafasi za juu au mbele ya wengine ni kufanya kile kisichofanywa na watu wengine. Kufanya yasiyofanywa na wengine ndiko kutakufanya uonekane kinara. Ukiweza kufanya hiki ninachokisema leo, ipo siku utakuwa kwenye sehemu fulani tofauti ya maisha, hautabaki kama ulivyo.

Mmoja wa watu ambao walitumia mbinu hii ni Kobe Bryant, mwanakikapu maarufu wa Marekani aliyezaliwa Agosti 23, 1978 na kufariki dunia katika mlipuko wa ajali ya helikopta Januari 26, 2020.

Bryant alichezea timu ijulikanayo kama Los Angeles Lakers. Unapotaja orodha ya wachezaji maarufu waliowahi kucheza mpira wa kikapu, utakosea sana usipomuweka Kobe Bryant katika orodha hiyo. Alijulikana kwa jina maarufu kama Mamba.

Kobe Bryant aliandika kitabu chake kiitwacho ‘Mamba Mentality’ kilichotoka Oktoba 2018. Katika mojawapo ya mahojiano aliyowahi kuyafanya alieleza kwamba ‘Mamba Mentality’ ni uwezo wa kufanya mambo kwa viwango vya juu na kulenga kuwa bora kwenye unachokifanya.

Kobe Bryant alifahamu kwamba ukitaka kuwa bora lazima utumie mfumo wa tofauti na wengine, lazima ufanye mambo kwa utofauti.

Pau Gasol, mmoja wa watu waliowahi kucheza timu moja na Kobe Bryant, anasema Kobe aliwahi kumwambia hivi: “Kama unahitaji kuwa mchezaji bora, lazima ufanye maandalizi, maandalizi na maandalizi zaidi.”

Pia anasema kwamba siku moja walikwenda kupata mlo wa jioni na baada ya hapo Kobe alimuaga kwamba anakwenda jimu. Hivyo alitumia muda wake mwingi kufanya mazoezi na kujiandaa.

Aliyewahi kuwa Kocha wake, Phil Jackson (1999-2001, 2005 – 2011) anasema Kobe alifika NBA (Ligi ya Kikapu ya Marekani) akiwa na kiu ya kuwa mchezaji bora wa muda wote. Aliweza kufanikisha hilo kwa kuwa mvumilivu na kuwa sugu.

Anasimulia: “Timu yetu ilikutana mara nyingi saa 2:30 asubuhi ili kufanya mazoezi ya mechi inayofuata. Jambo la kushangaza nilipofika sehemu ya kupaki gari langu nilikuta Kobe akiwa amepaki gari lake na anachapa usingizi. Yeye alikuwa akifika jimu saa 12 alfajiri ili kufanya mazoezi kabla ya mtu mwingine yeyote.

“Hii ni chata aliyoiacha miaka yake yote ya kazi yake. Kobe aliongoza kama mfano  kwa wana timu wenzake. Hawakuweza kwenda na kasi yake, siku zote walikumbana na changamoto ya mifano yake.

“Jambo linalonishangaza zaidi ni kwamba kitu kingine ambacho Kobe alitumia muda mwingi ni kutazama wengine wanachezaje. Si kutazama wanachezaje tu, bali kutazama ni mambo gani hawafanyi. Nafikiri katika kitu kilichomfanya aonekane mchezaji bora ni hiki.”

Ni kuulize wewe ndugu msomaji. Ni mara ngapi umeangalia kile ambacho wenzako hawafanyi na ukakifanya au unafanya kama wengine wanavyofanya?

Je, wengine hawafanyi nini kwenye kipaji ulichonacho ambacho wewe unakifanya? Je, wengine hawafanyi nini kwenye biashara kama yako ambacho unakifanya? Je, wengine hawafanyi nini kwenye huduma unayoitoa ambacho wewe unakifanya? Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza kwa mtu yeyote anayetaka kufanikiwa na kuwa wa viwango vya juu.

Njia mojawapo ya kufanya kile ambacho wengine hawafanyi ni kuukumbatia msemo wa  Gazeti la JAMHURI usemao: “Tunaanzia wanapoishia wengine.” Ukianzia wengine walipoishia tayari utakuwa unafanya kile ambacho wengine hawakifanyi.

Rafiki yangu Sarah Wilfred ni binti anayetengeneza viatu vya kuchomeka vinavyotengenezwa kwa ngozi maarufu kama vya Kimasai. Kitu cha kipekee ambacho Sarah anacho ni kwamba yeye baada ya kutengeneza viatu hivyo huwa anaviremba kwa kuvifunika na vitambaa vya vitenge. Viatu hivyo ni vya kitofauti sana na viatu vingine vya aina hiyo utakavyokutana navyo. Huyu ameanzia wanapoishia wengine.

Mwanamuziki Michael Jackson anajulikana kwa staili yake ya uchezaji wa kipekee inayojulikana kama ‘moonwalk’, ni staili aliyoiona kwa watoto wa mitaani lakini hakuwahi kuiona ikichezwa na wanamuziki wengine, akaichukua, kilichobaki ni historia. 

By Jamhuri