Inawezekana umefanya mambo mengi huku ukiweka juhudi katika kutafuta mafanikio lakini bado unapata matokeo hafifu. Habari njema ni kwamba wakati wako waja neema itakapokushukia.

Inawezekana nyota yako huioni asubuhi lakini kumbuka siku bado haijakwisha, nyota yako itaonekana kabla ya jua kuzama. Inawezekana wale uliosoma nao wanaonekana wametangulia mbele na wewe unajiona uko nyuma. Inawezekana wale uliokua nao na kucheza nao wanaonekana ni wa viwango vya juu na wewe upo chini.

Nikukumbushe tu mpendwa msomaji, kila mtu ana wakati wake.

Wakati wako ukifika mambo yote yatakuwa sawa. “Leo ni chungu, kesho ni chungu, kesho kutwa ni tamu, watu wengi hukata tamaa kesho jioni,” ni maneno ya bilionea Jack Ma, mwanzilishi wa Kampuni ya Alibaba na tajiri namba moja kutoka China.

Usikate tamaa, kwani wakati ujao unafurahisha. Naunga mkono hoja ya aliyetoa msemo wa “Yajayo yanafurahisha.”

Nayapenda sana maneno ya Mhubiri ambayo nimekuwa nikiyasoma na kuyatafakari mara nyingi kwenye maisha yangu, anasema: “Nikarudi na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.” (Mhubiri 9:11)

Kuna watu ambao nyota zao zinaonekana jioni badala ya kuonekana asubuhi, yaani yale waliyoyategemea huja kwa kuchelewa. Inawezekana na wewe pia yale unayoyatarajia bado hayajatokea lakini hiyo si sababu ya kukata tamaa.

Ukienda kwenye kituo cha daladala na kusubiri daladala na isitokee, si kwamba utaondoka kituoni, la. Utabaki na kusubiri mpaka basi litakapotokea. Maisha yetu yanahitaji kuwa kama ya msafiri kwenye kituo cha daladala pia.

Sixto Rodriguez, raia wa Detroit, Marekani, aliacha kuimba muziki baada ya albamu zake mbili kushindwa kuuzika vema sokoni. Baada ya miaka 30 umbali wa maili 8,000 alikuwa gumzo kubwa na mtu maarufu nchini Afrika Kusini.

Sixto Rodriguez akiwa na miaka 16 alianza kucheza gitaa la familia. Wazazi wake walikuwa ni wahamiaji kutoka Mexico, mji waliofikia ulikuwa mji wenye mateso kwa wahamiaji ingawa miji mingine ilikuwa na mateso makubwa kuliko Detroit, hivyo Sixto alikulia huko.

Mateso na unyanyasaji alivyopitia vikamfanya aanze kuimba. Mchana alikuwa mfanyakazi wa kampuni ya kubomoa na kurekebisha nyumba mbovu, usiku alikuwa mwimbaji anayeteseka.

Mwaka 1969 Rodriguez alikuwa akitumbuiza katika baa iliyojulikana kama The Sewer ndipo Theodore na Dennis Coffey walipomuona na kuanza kumsimamia kwenye kazi zake za muziki.

Mwaka 1970 alitoa albamu yake ya kwanza iliyoitwa ‘Cold Fact’ ambayo haikuuza vizuri. Mwaka 1971 Novemba alitoa albamu yake ya pili iliyokwenda kwa jina la ‘Coming From Reality’, kama ilivyokuwa ya kwanza haikuuza.

Baada ya albamu yake ya pili kuwa na mauzo kidogo, aliamua kuachana na muziki na kurudi katika kazi za ujenzi.

Fununu zinasemekena kwamba mwaka 1971 binti mmoja mwenye asili ya Kimarekani alikwenda kumtembelea mpenzi wake aliyekuwa akiishi Cape Town, Afrika Kusini na alikwenda na albamu ya kwanza ya Rodriguez Cold Fact.

Aliwashirikisha wenzake albamu hiyo rafiki zake nao wakaipenda na wakataka wapate yao lakini hawakujua wataipata wapi, njia nyepesi ilikuwa ni kuikopi albamu hiyo.

Nyimbo za Rodriguez zikaanza kusambaa na kupigwa Afrika Kusini huku Rodriguez mwenyewe akiwa hajui linaloendelea.

Kuna baadhi ya nyimbo zake zilifungiwa kwa sababu zilikuwa zinaongelea serikali ya kipindi hicho, kufungiwa kwake kukawafanya watu waendelee kutafuta nyimbo hizo. Jambo la kushangaa hakuna aliyejua msanii huyo kama yu hai.

Ilikuwa mwaka 1997, karibu miaka 30 baada kutoa albamu yake ya kwanza ambapo mwanae wa kike Eva alipokuja kukutana na tangazo lililokuwa likimtafuta Rodriguez kwenye tovuti moja. Eva aliandika kwenye tovuti hiyo: “Sitanii! Rodriguez ni baba yangu.” Baadaye walimtafuta Rodriguez na kumpata kwenye mawasiliano kupitia Eva.

Mwaka 1998 alialikwa kutumbuiza Cape Town siku mbili, Machi 6 na 7. Tiketi zote ziliuzwa na watu wapatao 5,000 walijaa uwanjani kumshuhudia Sixto Rodriguez. Sixto anatukumbusha kuwa nyota yako inaweza kuonekana jioni, usikate tamaa.