WANA MBEYA KUPOKEA HUKUMU YA MBUNGE WAO SUGU LEO

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, leo inatarajia kusoma hukumu ya kesi ya kutumia lugha ya fedeha dhidi ya Rais Dkt John Pombe Magufuli, inayowakabili Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi pamoja na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu kusini, Emmanuel Masonga.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Desemba 30,2017 eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Jamhuri iliwasilisha mashahidi watano na kielelezo kimoja cha sauti iliyodaiwa kurekodiwa na shahidi wa tano, Inspekta Joram Magova.

Upande wa utetezi uliwasilisha mashahidi sita wakiwamo Sugu na Masonga waliokana kutamka maneno wanayoshtakiwa kuyatoa.

Washtakiwa walitetewa na mawakili Sabina Yongo, Boniface Mwabukusi na Hekima Mwasipu kabla ya kujitoa na sasa wanawakilishwa na Peter Kibatala.

Kwa mara ya kwanza, Sugu na Masonga walifikishwa mahakamani Januari 16 na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mkuu, Joseph Pande aliyeeleza upelelezi ulikuwa umekamilika na walikuwa tayari kuendelea na usikilizaji.