MWANZA

NA MWANDISHI WETU

Wanafunzi 12 wa Shule ya Sekondari ya Igokelo,
Misungwi, mkoani Mwanza wametiwa mimba ndani
ya kipindi cha miezi minane ya mwaka huu.
Wanafunzi hao ambao wako chini ya miaka 18
wameacha masomo. Pamoja nao, wanafunzi
wengine wameacha masomo baada ya kuolewa.
Januari hadi Juni, mwaka huu wanafunzi watano
walibainika kuwa na ujauzito na wengine saba
walibainika kati ya Julai na Agosti, mwaka huu.
Umbali mrefu na kukosa mabweni vinatajwa kuwa ni
miongoni mwa sababu za tatizo la mimba kwa
wanafunzi hao.
Sababu nyingine ni umaskini, tamaa, ukosefu wa
elimu inayohusu athari za mapenzi utotoni, wazazi
na walezi kuwatumia watoto kama vitega uchumi,
ukatili wa kijinsia na wanafunzi wenyewe kutokuwa
na uwezo wa masomo darasani.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Igokelo, Hamisa
Hassan, anasema wanafunzi wengi wanaotiwa
mimba ni wa kidato cha kwanza.
“Tatizo ni kubwa sana. Kipindi cha mwaka 2018
changamoto kubwa ni mimba hapa Igokelo.
“Miongoni mwa watoto hao tuliowapima, watoto
kama watatu wa kidato cha tatu, kidato cha pili
kama wawili na cha nne mmoja, wengine wote ni
kidato cha kwanza,

” anasema.

Anasema uongozi wa shule unashirikiana na Shirika
la Kivulini kutoa elimu ya madhara ya mimba za
utotoni na faida ya elimu.
“…Ukiangalia zaidi shida kubwa ipo kwa wazazi.
Ugumu wa maisha wa familia unasababisha wazazi
washindwe kuwapa mahitaji vijana wao, hali
inayosababisha watoto kujiingiza kwenye uhusiano
wa kimapenzi ili wapate mahitaji ya msingi,

anasema.
Anasema shuleni kwake Igokelo wapo watoto
wanaotembea kutoka Wenzamiso (kilometa saba),
kutoka Nyahiti (kilometa sita) na kutoka Nyangaka
ambako ni kilometa tano.
Anawataja waendesha bodaboda kuwa
wanaongoza kuwashawishi wanafunzi na
mwishowe kuwapa mimba.
Kijiografia, Igokelo yenye walimu 26, wanafunzi
wengi hupita maporini wakati wa kwenda na kutoka
shuleni. Hiyo ndiyo shule pekee katika kata hiyo
yenye vijiji sita.
“Humo kwenye mapori wanakutana na vishawishi
vingi, wengine wamepata ujauzito kwa kubakwa,

anasema Mwalimu Hassan.
Mwanafunzi anayetoka Kijiji cha Busolwa (jina
tunalo), inadaiwa kuwa amepata ujauzito baada ya
kubakwa wakati akitoka shuleni.
Mwanafunzi mwingine anayesoma kidato cha
kwanza (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka
17, Septemba 19, mwaka huu aliozwa na baba yake
mzazi, Jackson Songoma.
Songoma anayeishi Kijiji cha Mwajombo, anadaiwa
kupewa mahari ya ng’ombe watano.
Mmoja wa washukiwa wa mkasa huo, Samuel
Majige, anakiri kushiriki sherehe za kuozwa kwa
binti huyo aliyezaliwa Aprili 24, 2001.
Sheria ya Mtoto, Namba 21 ya mwaka 2009, na
Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 1989 wa haki za
mtoto, vinamlinda mtoto dhidi ya matukio hayo.
Tanzania iliridhia mkataba huo Julai 10, 1991.
Kipengele cha (ii) cha mkataba huo wa kimataifa,
pamoja na mambo mengine kinatamka mtoto anayo
haki ya kupata elimu. Kipengele cha (iii) kinataka
mtoto alindwe na wazazi / walezi / jamii na serikali
dhidi ya madhara.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, sehemu ya (vii)
inasema mtoto ana haki ya kupata huduma bora za
elimu, malazi na matibabu kwa ajili ya ustawi wake.
Polisi wilayani Misungwi wamewakamata
watuhumiwa watano kuhusu tukio la kuolewa kwa
mwanafunzi huyo.
Ofisa Mtendaji Kata ya Igokelo, anayehudumu pia
Tarafa ya Misungwi, Lucas Bukundi, amethibitisha
kuwapo tukio hilo.

Anaviomba vyombo vya dola kuchukua hatua dhidi
ya watu wanaokatisha wanafunzi masomo kwa
kuwaoa au kuwapa ujauzito.
Ofisa Elimu Wilaya ya Misungwi, Dianah Kuboja,
hakupatikana ofisini kwake. Simu yake pia haikuwa
hewani wakati alipotafutwa.
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Misungwi, Juma Sweda,
anasema kukamatwa kwa watu hao, wakiwamo
baba mzazi wa binti na mume aliyeoa kumetokana
na taarifa zilizoripotiwa na Mtendaji wa Kata ya
Igokelo.
Amewaonya wazazi akisema wakibainika
watakamatwa na kushtakiwa mahakamani kwa
mujibu wa sheria.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan
Shana, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema muda
mwingi alikuwa akishughulikia tukio la kupinduka na
kuzama kwa pantoni ya MV Nyerere kisiwani Ukara,
wilayani Ukerewe.
Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally,
anasema mimba na ndoa za utotoni
vinasababishwa na wanaume kutelekeza familia
wakati wa mavuno na kwenda kustarehe na
makahaba ambao ni maarufu kama ‘nzige’
,

‘kisemosi’ au ‘kipapatio.’
Sababu nyingine ni wingi wa minada na baadhi ya
wanafunzi kukata tamaa ya masomo kutokana na
wazazi wao kuwatishia kuwalaani iwapo watafanya
vizuri kwenye mitihani.
“Kuna mtindo wanafunzi wanaokabiliwa na mitihani
huwa wanakwenda kuweka kambi kwenye miji ya
watu. Wavulana wanne na wasichana wanne. Na

wanasema kinachoendelea huko si kusoma.
Wanafanya mambo yao mengine.
“Na hii ni kama imehalalishwa na walimu na
wazazi,

” anasema.

Ally anasema baadhi ya wazazi huwaamuru watoto
wao wachore ‘madudu’ kwenye mitihani ili
washindwe kwenda sekondari, hivyo waweze
kuolewa.
Pia inadaiwa kuwa baadhi ya walimu kuwaadhibu
pale wanaposhindwa kukariri na wanafunzi
wanaokabiliwa na tatizo la ukosefu wa sare za
shule.
“Hivi vitu si tu vinawakatisha tamaa baadhi ya
wanafunzi kuendelea na masomo, bali vinawaathiri
hata kisaikolojia. Baadhi ya walimu wamezoea kuwa
na vitisho hasa wanapokuwa zamu ya kusimamia
wanafunzi shuleni.
“Na kwa sababu walimu hawana lugha ya kirafiki,
mtoto anabakwa njiani akifika shuleni hawezi
kusema anakaa kimya. Mwalimu akiuliza swali
akishindwa tu kujibu, fimbo. Huyu mtoto hatakaa,

anasema.
Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya
Kata ya Idetemya, wilayani Misungwi (jina
tunalihifadhi) anasema: “Kempu za kujisomea wengi
hawafanyi hivyo.”
Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya
Misungwi, Thomas Lutego, anasema mimba na
ndoa za utotoni ni tatizo kubwa.
Anasema Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi
inaangalia namna ya kukabiliana na changamoto ya

wanafunzi wa Sekondari ya Igokelo wanaotembea
umbali mrefu.
“Ipo bajeti ya kujenga mabweni. Lakini ile ya
kujenga sekondari zaidi hapa Igokelo haipo kwa
mwaka huu 2018/2019. Tunaamini upatikanaji wa
fedha ndio utakaosaidia kuleta maendeleo,

anasema Lutego.
Baadhi ya wazazi wametoa mapendekezo. Ester
Maduhu, Sayi Kija na Seleman Jacob,
wanapendekeza kila kata ijengewe sekondari mbili
ili wanafunzi wasitembee umbali mrefu.
“Ikiwezekana hata sheria ibadilishwe. Badala ya
kufungwa aliyempa mimba mwanafunzi,
mwanafunzi wa kike atakayebeba ujauzito
akamatwe na afungwe.
“Tukifanya hivi hata wao wanafunzi wa kike
wataogopa kujamiiana,

” anasema Saida Mohamed.

…tamati….

688 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!