Wakati vyuo vya elimu ya juu vimeanza mapokezi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wiki iliyopita, wanafunzi wengi hasa kutoka familia maskini bado wako nyumbani huku wakihofia kukosa masomo baada ya kukosa mikopo.

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (HESLB), imesema haitaweza kutoa mikopo kwa wanafunzi wote kutokana na uhaba wa fedha. Wiki iliyopita, wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini walipiga kambi kwenye ofisi za HESLB Dar es Salaam kuulizia hatima ya maombi ya mikopo yao.


Kwa mujibu wa gazeti la Serikali la Daily News toleo la Jumamosi iliyopita, wanafunzi wengi wamelalamika kwamba hakukuwa na uwazi katika ugawaji wa mikopo hiyo, na kudai kulikuwa na upendeleo katika mchakato mzima.


“Wengi wetu tunatoka familia maskini, tulisoma katika shule za umma kwa sababu wazazi wetu hawana uwezo wa kutugharimia maisha ya shule binafsi, lakini kinachotushangaza ni kwamba pamoja na mazingira hayo Bodi imeshindwa kutupatia mikopo,” alisema mwanafunzi kutoka kabila la Wamaasai aliyekuwa njiani kwenda Chuo Kikuu cha Elimu ya Ushirika na Biashara cha Moshi (MUCCoBS).


Kwa upande mwingine, taasisi za elimu ya juu zimesisitiza kuwa hakuna mwanafunzi atakayeruhusiwa kujiandikisha kabla ya kulipa ada ya mwaka mzima.


Kwa mfano, maelekezo ya fomu ya kujiunga MUCCoBS yanabainisha kuwa wanafunzi wanaofadhiliwa na HESLB hawataandikishwa bila kulipa kiasi cha fedha kinachotakiwa.


Wamelalamika pia kwamba kuna wanafunzi wawili kutoka familia moja walioomba mikopo, lakini ni mmoja tu aliyefanikiwa kupata huku mwingine akinyimwa.


Mwanafunzi mmoja aliyeomba kutotajwa jina, alielezea kushangazwa kuona dada yake wanayefanana sifa za kitaaluma akifanikiwa kupata asilimia 98 ya mkopo, lakini maombi yake yeye hayakufikiriwa.


“Nina marafiki kutoka familia tajiri ambao wamekwenda shule binafsi na ambao hawakufanya vizuri kuliko mimi lakini wamepata mikopo, wakati mimi nimekosa nafasi hiyo,” alisema mwanafunzi mwingine.


Wanafunzi wengine walisema wanajihisi kama wako mwishoni mwa barabara ambapo hawawezi kumudu gharama zote za masomo, wakibainisha kuwa wametoka familia maskini.


“Ni Mungu pekee anayejua ugumu niliopitia wakati nikisoma katika shule za msingi na sekondari, kwa sababu wazazi wangu hawawezi kulipa ada kwa wakati. Sasa niko katika harakati za kujiunga chuo kikuu, ni wazi kuwa gharama ni kubwa mno na wazazi wangu hawataweza kuzimudu,” alisema mwanafunzi mwingine.


Naibu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini kitengo ch taaluma, Profesa Seth Nyagawa, alisema chuo hicho hakitamkubali mwanafunzi yeyote hadi atakapolipa ada ya awamu ya kwanza.


“Tunawataka wanafunzi kulipa ada yote ya awamu ya kwanza,” alisema Profesa Nyagawa.


Alipoulizwa kama chuo hicho kiko tayari kupokea wanafunzi wenye matatizo ya kupata mikopo na kuwapa muda wa kuyatatua, Profesa Nyagawa alisisitiza kuwa chuo hakitamkaribisha mwanafunzi atakayeripoti akiwa mikono mitupu.

 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idris Kikula, alisema chuo hicho kinawataka wanafunzi kuripoti na vielelezo vya maombi ya mikopo kutoka HESLB.


“Tayari tumeshapokea fedha kutoka HESLB kwa wanafunzi kadhaa wa mwaka wa kwanza… tunawataka wanafunzi waliobaki waripoti wakiwa na vielelezo walivyoombea mikopo kutoka HESLB, vinginevyo wanapaswa kulipa ada yote ya awamu ya kwanza kabla ya kuripoti,” alisema.


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kitengo cha Utawala, Profesa Yunus Mgaya, alitoa tangazo Ijumaa iliyopita kwenye gazeti hilo la Daily News akisema kwamba wanafunzi wanapaswa kulipa ada kabla ya kuripori chuoni.


“Wanafunzi wametakiwa kulipa gharama yote ya twisheni Septemba 29, 2012. Hata hivyo, wote watakaoshindwa kufanya hivyo wataruhusiwa kulipia nusu ya gharama za twisheni,” inasema sehemu ya tangazo hilo.


Inaelezwa kwamba wanafunzi watakaoruhusiwa kujiandikisha, kupata malazi na huduma nyingine za chuo ni wale tu waliolipa ada.


Ofisa Habari wa HESLB, Cosmas Mwasobwa, alisema bodi hiyo imeweka tangazo kwenye tovuti ikiwataka wanafunzi wenye matatizo mapya kukata rufaa.


“Hatujafunga ukurasa wa suala la mikopo mwaka huu, tumeweka tangazo kwenye tovuti yetu kwa ajili ya yeyote mwenye matatizo mapya aweze kukata rufaa,” alisema.


Mwasobwa alisema HESLB haina nia ya kumnyanyapaa mwanafunzi yeyote, ila inakabiliwa na uhaba wa fedha kumudu mahitaji yaliyopo. Hata hivyo, hakuweza kutaja idadi ya wanafunzi walioomba mikopo na waliofanikiwa kupata mikopo ya masomo katika vyuo vikuu nchini mwaka huu.


“Bajeti yetu kwa mwaka huu wa elimu ni Sh bilioni 345. Tayari tumeshatoa mikopo kwa wanafunzi 29,000 wa mwaka wa kwanza. Kwa sasa tunasubiri rufaa tuone kama tunaweza kuongeza zaidi wanafunzi. Lakini hofu kubwa ni uhaba wa fedha,” alisema.


Aliongeza kwamba baadhi ya wanafunzi wana baadhi ya maelezo yanayokosekana kwenye fomu za maombi yao, jambo linalowafanya kukosa mikopo.


Alitoa wito kwa wanafunzi husika kutumia nafasi ya kukata rufaa ili kuangalia makosa yanayoweza kurekebishwa. Hata hivyo, fomu hiyo ya rufaa haihitaji kitu chochote kuhusu wanafunzi ambao hawakufikiriwa katika maombi ya mikopo.


Kuhusu madai ya wanafunzi wenye sifa za kitaaluma zinazofanana kupata majibu tofauti ya mikopo waliyoomba, Mwasobwa alisema Bodi ya Mikopo inapenda kupata vielelezo vya malalamiko hayo ili iweze kurudia kukagua kuona ilipokosea.


5939 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!