DODOMA

EDITHA MAJURA

Shule ya Msingi Nzuguni ‘B’  ya mkoani Dodoma, inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa hivyo kuwalazimu wanafunzi kusoma kwa zamu.

Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo ndiye mlezi wa shule hiyo yenye wanafunzi 2,402, madarasa tisa na matundu nane ya vyoo.

Uchunguzi wa JAMHURI, umebaini kuwa ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa, wanafunzi wanaingia darasani kwa kupokezana kwa awamu mbili.

Pamoja na hilo, wakati mwingine wanalazimika kufundishiwa nje, chini ya miti na ubao uliotenegenzwa katika hali inayowezesha kuuhamisha kwa urahisi.

Afisa Elimu wa Wilaya ya Dodoma, Misungwi Kigosi, amesema changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa mjini humo ipo karibu kwa shule zote wilayani humo.

Amesema kutokana na hali hiyo, imeelezwa wanafunzi kuingia darasani kwa zamu na kufanyika ujenzi wa madarasa chini ya viongozi wa mitaa na kata.

Mbali na upungufu wa madarasa, wanafunzi wa shule hususani wanaotokea mtaa wa Nzuguni C, wanakabiliwa na hatari ya kufa maji wanapovuka kwenye korongo linalotenganisha eneo hilo na Nzuguni B, ilipo shule yao.

Mara kadhaa, wazazi na walezi wa wanafunzi hao wanawazuia watoto kwenda shule ama kurudi nyumbani nyakati za mvua kubwa.

Mratibu wa Elimu wa kata hiyo, Sospeter Ramadhan, amethibitisha kuwapo changamoto hiyo na kusema wameishaishirikisha Serikali ya mtaa wa Nzuguni C, ili watenge eneo kwa ajili ya ujenzi wa shule.

Kigosi amethibitisha kufahamu adha wanayoipata wanafunzi wa Nzuguni ‘B’ na kwamba amewahi kushiriki kuvusha watoto kwenye daraja lililokuwa limefunikwa kwa maji wakati wa mvua.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nzuguni ‘C’, Idrissa Bale, amesema wakazi wa mtaa huo wameafikiana kutoa eneo walilopewa na Taasisi ya Kilimo Tanzania (TASO) mwaka 2009 kutumika kwa gulio, lakini sasa litawekezwa kwa ujenzi wa shule.

“Eneo ni kubwa, limezungushiwa uzio na linafaa kwa ujenzi, hata mwaka jana Mkurugenzi Mtendaji (Godwin Kunambi), alifika tukampeleka akalikagua na kuridhishwa,” amesema.

Hata hivyo, Bale amemkariri Diwani wa kata hiyo, Aloyce Luhega, akisema uongozi wa manispaa unaamini kwamba eneo hilo bado lipo chini ya TASO, hivyo kubadili matumizi yake ni lazima kuihusisha taasisi hiyo.

Kuhusu ujenzi wa shule hiyo, Afisa Elimu wa Wilaya ya Dodoma, Kigosi amesema uongozi wa eneo hilo unapaswa kuainisha maeneo yanayofaa kwa ujenzi, kisha wafuate taratibu zilizowekwa.

Amesema taratibu hizo ni pamoja na kushirikisha nguvu za wananchi kuanzia ujenzi wa msingi mpaka kufunga `renta’, ili Serikali iwajibike kukamilisha sehemu inayobaki.

Diwani wa Nzuguni, Aloyce Luhega, alipotafutwa na JAMHURI kuielezea kadhia hiyo, hakupatikana kwa madai ya kuwa katika kikao na baadaye kueleza kwamba amesafiri kwenda kumuuguza dada yake.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge, amesema utatuzi wa changamoto hiyo ni kwa upande wa Nzuguni ‘C’ kujenga shule katika eneo hilo.

By Jamhuri