Wananchi tunataka mabadiliko

Siasa ni sayansi, ni taaluma pia. Sayansi ina ukweli na uhakika, na taaluma ina maadili, kanuni na taratibu zake. Siasa ni mfumo, mtindo, utaratibu au mwelekeo wa jamii katika fani zake zote za maisha.

Ni utaratibu uliowekwa au unaokusudiwa kuwekwa na chama kinachoongoza nchi, au kinachokusudia hivyo ili kukiwezesha chama hicho kunyakua au kudumisha uongozi wake.

Mtu aliyomo katika taaluma hii, yaani mwanasiasa, anatazamiwa awe na ukweli na uhakika katika kauli zake, mazungumzo yake na vitendo vyake mbele ya jamii. Kinyume cha taratibu hizi, mtu huyo si mwanasiasa. Ni zuzu wa siasa na hafai hata chembe katika mustakabali wa mambo ya siasa.

Wanasiasa ni watu wanaotazamiwa kuwa waadilifu. Wenye fikra na maono, wenye nguvu ya hoja, wenye kupingana bila kugombana, na wenye kutilia maanani mabadiliko ya fikra za watu. Kama vile sera za uchumi na maendeleo ya jamii.

Kwa vile taaluma yenyewe ni sayansi, pasipo na shaka mwanasiasa atakuwa amejijenga kimaadili na kitabia njema, kila wakati kudhihirisha kauli na mazungumzo yake kwa matendo hadharani kwa faida yake na kwa masilahi ya jamii.

Siasa si mchezo kama ‘kasimbago’ kila mtoto wa Kinyamwezi akacheza, wala si ngoma ya ‘ndekule’ kila kijana wa Kizaramo akaipiga. Siasa ni mfumo wa maisha na uhai wa binadamu. Hivyo, hadhari na tafakuri lazima iwekwe na mtu au mwanasiasa kabla ya kuihutubia hadhira iliyoko mbele yake.

Ni kweli kukaa karibu na ua la waridi utanukia harufu nzuri. Lakini haitakufanya wewe kuwa ua la waridi. Kuwa karibu na ‘kingunge’ wa siasa haikupi alama za kutosha kufaulu kuwa mwanasiasa. Ili uwe mwanasiasa lazima upate mafunzo ya taaluma ya siasa, na ikiwezekana uwe ua la waridi.

Watanzania sasa tuna elimu zaidi kuliko miongo sita iliyopita. Tunafahamu mambo mengi na tunahitaji mno mabadiliko. Lakini tuna uhaba wa maarifa na mbinu za siasa ambayo kwayo yanasababisha tuwe na uwezo hafifu kufikia mabadiliko tuyatakayo.

Ni kweli pia sasa Watanzania tupo wengi kuliko wakati tulipokuwa tukidai uhuru wa nchi yetu na tulipoanza kujitawala wenyewe. Miongo saba imepita, bado tuna kilio chetu cha kutaka mabadiliko yatakayoondoa dhuluma na kuweka usawa na haki kwa jamii.

Watu makini na muhimu wa kutufikisha kwenye mabadiliko haya ni wanasiasa, si mazuzu wa siasa.  Wanasiasa wanapothamini taaluma yao na wanapokiri jamii ya Watanzania inahitaji mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo ya jamii, kamwe hawachezi matusi na kejeli.

Watambue mchezo wao huo ni kashfa kwao na mauti kwa wananchi. Wananchi tunatambua zaidi uwezekano wa mabadiliko katika maisha yetu, na tunajiamini zaidi. Ndiyo maana hatulazimiki kukubali dhuluma zitokee katika nchi yetu ambamo taratibu zake kwa msingi ni za haki.

Wanasiasa, demokrasia maana yake si tu utawala wa walio wengi, demokrasia ya kweli lazima iheshimu maoni ya wachache na impe nafasi kila mtu kutoa mawazo yake kwa uhuru na uwazi, bila ya kuvunja sheria ya nchi, au kutumia nguvu.

Demokrasia ya kweli inataka watu wakubali kutokubaliana, na waendelee kujadiliana na kubishana kwa moyo wa kuvumiliana na kuheshimiana, siyo kutukanana. Kwa hiyo mabadiliko  yanafanywa  kwa njia ya demokrasia ya kweli.

Wanasiasa tambueni fika wananchi wa Tanzania tunataka demokrasia ya kweli na ambayo ni ya haki kwa wote, na wakati huo huo kulinda amani ya taifa letu, usalama na umoja.