Neno ‘haliwezekani’ tafsiri yake hujafikiria sana

 

Suluhisho ni mtihani. Kila tatizo lina suluhisho, tatizo ni wapi upate hilo suluhisho. Kuna maoni tofauti juu ya suluhisho. Uri Levine anapendekeza: “Lipende tatizo, na si suluhisho.” Kuna ambao wanaona kuwa usijikite kwenye tatizo, jikite kwenye suluhisho. Mitazamo hii inafanya suluhisho kuwa mtihani. Kila tatizo limebeba suluhisho. Suluhisho ni njia ya kutatua tatizo. Katika kukabili matatizo ya maisha kuna ambaye anatoa suluhisho la kudumu kwa tatizo la muda mfupi, mfano kujiua. Kuna ambao wanaona kuwa si kila tatizo linahitaji suluhisho, matatizo mengine yanahitaji ukomavu, kukua na kuyazidi. Suluhisho ni mtihani.

Unaweza kutatua tatizo gumu kwa njia ambayo si ya kawaida ukizingatia kuwa njia hiyo iwe halali na ya haki. Katika visasili vya Kigiriki, Gordian, mkulima mdogo alipata kuwa mfalme wa Persia huko Asia. Alizoea kufunga nira ya ng’ombe wake  kwenye kibandawazi cha kukokotwa na farasi, ambavyo vyote alivitoa kwa heshima ya ‘mungu’ Zeus, kwa fundo gumu kulifungua.

Siku moja aliwaambia watu: “Kama mtu angefungua fundo gumu angekuwa mfalme wa Asia yote.” Hakuna aliyeweza, lakini Alexander Mkuu alikata fundo kwa kutumia jambia lake kama suluhisho lisilo la kawaida. Tunapata msemo: “Kata fundo la Gordian,” unaomaanisha tatua tatizo gumu kwa namna ambayo si ya kawaida.

Katika kutatua tatizo kwanza libainishe. Steve Jobs alisema: “Unapolibainisha tatizo kwa usahihi, karibu unakuwa na suluhisho.” Tatizo lieleze wazi kabisa. Liwekee mipaka. Bainisha sifa za tatizo. Fafanua tatizo. Albert Einstein, mwanasayansi na mwanahisabati mashuhuri alisema: “Kama ningekuwa na saa moja ya kutatua tatizo ningetumia dakika 55 nikifikiria juu ya tatizo na dakika tano nikifikiria juu ya suluhisho.” Kuweka vizuri tatizo ni nusu suluhisho ya tatizo. Umiza kichwa kupata suluhisho la tatizo.

Ukitaka kutatua matatizo yako,  kaa mbali na watu wenye mtazamo hasi, wanaona tatizo kwenye kila suluhisho. Kuwa sehemu ya suluhisho. “Kama wewe si sehemu ya suluhisho ni sehemu ya tatizo.” (Methali ya Kiafrika). “Kwa tatizo lolote lile, uwe sehemu ya suluhisho. Usikae tu na kuuliza maswali na kunyoshea vidole vikwazo,” alisema Tina Fey.

Ukitaka kutatua matatizo yako, fikiria na kuwa mbunifu. Usilaumu giza, washa mshumaa. Neno “haiwezekani” lina maana hujafikiria sana, ‘hujaumiza’ kichwa ukitafuta ufumbuzi wa tatizo. Sam Moore, aliyekuwa rais wa Kampuni ya uchapishaji ya Thomas Nelson Publishers alikuwa na bango kwenye ofisi yake lenye maneno: “Niletee suluhisho, na si matatizo yako.”

Ukitaka kutatua matatizo yako kuwa na imani na uwezo wako wa kutatua tatizo. “Hofu ni ukosefu wa imani katika uwezo wako wa kutengeneza suluhisho lenye nguvu,” alisema T.F. Hodge. Ukitaka kutatua matatizo yako kuwa na mtazamo wa lisilowezekana linawezekana.

“Inawezekana ni suala la mtazamo, suala la uamuzi, kuchagua kati ya yanayowezekana yenye sifa ya kutowezekana, wakati mojawapo linatoa sauti ya fursa, linakuwa suluhisho linalowezekana,” alisema Dejan Stojanovic.

Ukitaka kutatua matatizo yako nenda kwenye chanzo cha tatizo na si matokeo ya tatizo. Mfereji wa maji ukiwa unavunja nyumbani na ukawa na tatizo la nyumba kujaa maji, unaweza kukausha maji kwenye sakafu au unaweza kuziba na kurekebisha sehemu inayovuja. Nenda kwenye mzizi wa tatizo na si matawi ya tatizo. Neno “haliwezekani” lina maana haujafikiria sana.

1239 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!