Wananchi wa Kata ya Makata, wameulaumu uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale mkoani Lindi kwa kutelekeza mradi wa ujenzi wa Sekondari ya Wasichana Makata ambao ulitakiwa kukamilika miaka mitano iliyopita, JAMHURI limebaini.
Kukwama kwa mradi huo kumetokana na kupotea katika mazingira tata kiasi cha Sh milioni 14 ambazo zilichangwa na wananchi wa kata hiyo na Mbunge wa Jimbo la Liwale, Zuberi Kuchauka.

Mbunge huyo alichangia Sh milioni 10 kutoka katika fedha za Mfuko wa Jimbo kuunga mkono jitihada za wananchi ambao walikuwa wamechanga Sh milioni 4 kufanikisha mradi huo.

Wameliambia JAMHURI kuwa ujenzi wa sekondari hiyo umefutwa katika ajenda za halmashauri hiyo na badala yake shule ya sekondari ya mchanganyiko ya Ana Magoa, iliyopo Kata ya Mangilikiti itabadilishwa na kuwa Shule ya Wasichana ya Wilaya.
Wamesema kuwa halmashauri hiyo imekana kuhusika na ujenzi wa sekondari hiyo wakati awali iliwataka wananchi kuchangia fedha na kutenga eneo la kujenga shule hiyo na kuahidi kuwasaidia pale watakapoishia.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Makata, Ali Mbandi, amesema awali halmashauri ilisema imeingiza kiasi cha Sh milioni 40  kwenye akaunti ya ujenzi wa sekondari kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili yaliyotelekezwa.
Hata hivyo, baadaye ilikuja kubainika kuwa halmashauri haikuweka kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti bali walikuwa wanadanganywa.
“Ramani tuliyopewa ilikuwa ni ya kujenga madarasa mawili tu na sio ya sekondari nzima,  Kamati ya Ujenzi ndiyo iliyopewa jukumu la kutoa pesa katika akaunti hiyo na awamu ya kwanza ilitakiwa kuwa na madarasa manne,” amesema Mbandi.
Kutokana na kusimama kwa ujenzi wa sekondari hiyo, mifuko 65 ya chokaa na mbao 600 imeharibika na kusababisha hasara kubwa.
“Halmashauri imetuambia kuwa Sekondari ya Ana Magoa ambayo ni ya mchanganyiko ndiyo itakayobadilishwa kutoka Sekondari ya Kata ya Mangilikiti na sekondari ya wasichana ya wilaya;

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Makata, Titus Muyagi, amesema shule yake yenye wanafunzi 472 inakabiliwa na upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo ambapo yaliyopo ni manne tu.
Sera ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaelekeza kwamba tundu moja la choo linatakiwa kutumiwa na wanafunzi 22 wa kiume wakati wa kike ni 21.
Wakati wananchi wakisisitiza kupewa ramani ya ujenzi wa sekondari hiyo na halmashauri, Kaimu Mkurugenzi wa Wilaya ya Liwale, Omary Chingwile, amekana halmashauri kutotambua ujenzi wa sekondari hiyo.

“Sisi halmashauri hatuhusiki na hiyo sekondari kwa sababu ni mradi wao wenyewe. Fedha za ujenzi huo na taratibu zote wanasimamia wao wenyewe. Hakuna aliyewapa ruhusa ya kujenga hayo madarasa mawili na wala hakukuwa na makubaliano yoyote kati ya halmashauri na watu wa Makata ya kujenga shule hiyo.
Sababu nyingine ya kutokujenga shule hiyo ilitokana na kuwapo ujenzi wa Sekondari ya Kata ya Makata iliyopo Kijiji cha Mkundi na hivyo ilikuwa vigumu kwa halmashauri kuweza kugharamia ujenzi wa sekondari mbili kwa wakati mmoja.

Chingwile amesema mwaka 2012 halmashauri iliwashauri wakazi wa Kijiji cha Makata kusitisha kazi ya ujenzi wa sekondari hiyo lakini hawakusikia.
“Kuthibitisha kuwa hawakufuata maelekezo yetu, Idara ya Mipango iliwashauri waombe ramani ya ujenzi wa sekondari hiyo katika ofisi za ujenzi za wilaya ila walikaidi.
“Sekondari ya Ana Magoa ipo siku nyingi na ilikuwa ya mchanganyiko ambapo wavulana walioko kwenye hiyo sekondari tutawahamishia sekondari ya Mangando. Kwa hiyo, sekondari ya Ana Magoa (Kipule) ndiyo itakuwa ya wasichana kwa wilaya nzima”.

Wakati Kaimu Mkurugenzi huyo akikanusha kuufahamu mradi huo na kuishutumu kamati ya ujenzi wa sekondari hiyo kwa kutoishirikisha halmashauri hiyo, JAMHURI limefanikiwa kuiona BOQ ya ujenzi wa madarasa mawili iliyotolewa na Mhandisi wa Ujenzi Wilaya ya Liwale Juni 20,2012 pamoja na sampo ya ‘master plan’ ya sekondari hiyo kutoka kwa Programu ya Uendelezaji Elimu ya Sekondari (SEDP).
Katika ufafanuzi wake Chingwile amesema kuwa Wilaya ya Liwale inakabiliwa na changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu ambazo ni pamoja na uhaba wa matundu ya choo na nyumba za kuishi walimu katika shule za msingi.
Amesema asilimia 80 ya shule za msingi katika wilaya hiyo hazina matundu ya vyoo vya kutosheleza wanafunzi. Shule nyingi zina wanafunzi kati ya 400 na 700 lakini matundu ya vyoo yanayokuwapo ni matatu tu.

Utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyoo umekuwa ni wa kusuasua kutokana na uhaba wa fedha za utekelezaji ambapo halmashauri ilipanga kujenga choo kimoja chenye matundu sita katika shule za msingi 20 katika mwaka wa fedha uliopita.
Hata hivyo, ujenzi wa vyoo haukuweza kutekelezwa kwa shule zote kutokana na uhaba wa fedha badala yake vimejengwa vyoo vyenye matundu chini ya sita kwa shule 8 ikilinganishwa na 12 ambazo hatukuweza kujenga idadi stahiki ya matundu.
Shule ambazo matundu sita ya vyoo yamejengwa ni Mkundi, Magereza, Nahoro na Mbuli.
Shule zilizojengewa matundu chini ya sita ni Ngumbu, Kibutuka, Nanjegenja na Makata na kwamba choo kimoja kinajengwa kwa gharama ya Sh milioni 2/-.
Amesema halmashauri hiyo ilitenga  Sh milioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika shule za msingi katika mwaka wa fedha uliopita.
Kuhusu nyumba za kuishi walimu wa shule za msingi katika halmashauri hiyo, amesema katika mwaka wa fedha uliopita ilipelekwa Sh milioni 2.2 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba mbili za walimu katika Shule ya Msingi Makata.

“Fedha nyingine ilielekezwa katika shule nyingine zenye uhaba wa nyumba za walimu. Tulipata fedha nyingine za ruzuku ya maendeleo (CDG) Sh milioni 4.5.
Kila mwaka wa fedha huwa tunaweka mkakati wa kujenga nyumba 10 za walimu ambapo mwaka huu wa fedha tumepanga kujenga nyumba mpya tano tu kutokana na uwezo mdogo wa kifedha wa halmashauri na udogo wa bajeti yetu ya elimu, ambapo fedha nyingi inaelekezwa kwenye mpango wa elimu bure,” amesema Chingwile.
Hata hivyo, hakutaja kiwango hicho cha fedha kinachoelekezwa kwenye elimu bure ama makadirio yake kwa kila mwezi.
“Inahitajika Sh milioni 28 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba moja ya walimu ambayo ina huduma ya umeme wa REA au sola. Huduma ya maji inategemeana na eneo husika ila maeneo mengi ya vijijini hayana mfumo wa maji ya bomba,” amesema Chingwile.

 

Na Francis KAJUBI

By Jamhuri