Wiki iliyopita taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imewasilishwa bungeni. Taarifa hii inaonyesha kukua kwa deni la taifa la kuzidi trilioni 50. Imeonyesha kuwa wizara kadhaa zimekuwa na upotevu wa fedha za umma. Leo pia tumechapisha sehemu ya taarifa hizo ikionyesha Wizara ya Kilimo ilivyofuja fedha za mbolea.

Inaonyesha pia Benki ya CRDB ilivyokopesha hadi SACCOS ambazo hazijasajiliwa na kutofuata masharti ya riba. Pia taarifa hiyo inaonyesha deni la Serikali lililozidi muda liliostahili kulipwa. Hata hivyo, tumeshuhudia mawaziri kadhaa wakitumia nguvu kubwa kumjibu CAG pengine katika jitihada za kunusuru nafasi zao.

Sisi tunasema pamoja na nia nzuri ya mawaziri, tunadhani si mwafaka kwao kutumia muda mrefu kumjibu CAG badala ya kubana wanaofanya ubadhirifu. Kuna maeneo yako wazi katika ripoti hii yenye kuonyesha kuwa wizi umefanyika. Kutumia muda na mbinu kukanusha taarifa za CAG ni sawa na kujenga ukuta dhidi ya wabadhirifu.

Kwa miaka mingi tumeshuhudia watu, hasa wakurugenzi wa taasisi mbalimbali wakiharibu au kufanya ubadhirifu katika eneo moja, wamekuwa wanahamishawa eneo la kazi. Utaratibu huu umejenga usugu kwa watu wenye nia ovu dhidi ya mapato ya taifa. Tunaamini sasa umefika wakati yeyote anayetuhumiwa hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.

Nchi hii haitaendelea na kupiga hatua katika sekta ya viwanda kwa kujitetea, bali kwa kufanya kazi na kudhibiti wizi. Mtu anayefanya mipango ya kuchepusha fedha za umma zilizolenga kuendeleza kilimo, kukopesha wananchi au kununua vifaa vya elimu, huyo analenga kuharibu taifa. Anakuwa ni sawa na mkulima anayekula mbegu. Usitarajie mavuno ikiwa umekula mbegu.

Fedha za umma zinazotumika leo zinajenga msingi wa taifa bora la kesho. Serikali ipo kwa ajili ya kutoa huduma za jamii. Fedha hizi zinazoibwa au kufujwa ni mali yetu sisi wananchi. Kinachotokea ni kwamba tunaweza kudhani mhusika anaiba fedha za umma kumbe uhalisia anaiba fedha za wananchi zilizopatikana kupitia kodi.

Tunasisitiza kuwa si vyema taarifa ya CAG kujibiwa na mawaziri, badala yake watu waliotuhumiwa wapewa nafasi ya kufikishwa mbele ya sheria kufafanua jinsi walivyozitumia fedha hizo na kwa kufanya hivyo tutaongeza uwajibikaji na utawala wa sheria. Mungu ibariki Tanzania.

1208 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!