Wanaowalinda wageni haramu wachukuliwe hatua

Katika gazeti letu la JAMHURI toleo la wiki iliyopita, tulichapisha habari ya uchunguzi iliyokuwa ikimhusu raia wa Pakistan, Ajaz Ahmed, mfanyabiashara haramu ya kuuza binadamu aliyefukuzwa nchini na kurejea tena kwa jeuri akiendelea na biashara hiyo.
Ahmed alifukuzwa nchini Oktoba 29, 2014 kwa kupewa amri ya PI (Prohibited Immigrant) na Idara ya Uhamiaji nchini, huku akiondolewa kwa ulinzi mkali na kupandishwa kwenye ndege kurudishwa kwao Pakistan.
Kabla ya raia huyo wa Pakistan kuondoka nchini, alitoa kejeli kwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji waliokuwapo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwamba pamoja kufukuzwa kwake, atarudi Tanzania kwani hakuna tofauti na chooni na baadhi ya maofisa amewaweka mfukoni.
Ahmed alibainika kuwa amewahifadhi raia wenzake wa Pakistan katika nyumba aliyokuwa akiishi eneo la Masaki, Dar es Salaam ambao alikuwa akiwasafirisha kwenda Afrika Kusini kupitia mpaka wa Tanzania na Zambia (Tunduma).
Licha ya Mpakistani huyo kuondolewa nchini, tena  chini ya uangalizi maalum, mtandao wake ulifanya mpango wa kumtorosha katika Uwanja wa Ndege wa Doha, ambako alipumzika kwa muda huku ndege aliyokuwa akisafiria ikiondoka bila ya yeye kuwamo.
Mtuhumiwa huyo wa biashara haramu ya kusafirisha binadamu duniani, akiwa katika maficho yake nje ya nchi, aliendelea kufanya mawasiliano mara kwa mara na mtandao wake unaowahusisha pia baadhi ya maofisa wa Idara ya Uhamiaji ambao ndiyo waliofanikisha mpango wake wa kurudi nchini.
Kwa ujeuri, mfanyabiashara huyo wa kuuza na kusafirisha binadamu aliyekaribishwa tena nchini ili kuendeleza uharamia huo, alinyang'anywa hati yake ya kusafiria yenye namba KH. 377690 iliyotolewa Karachi, Mei 12, 2013.
Sisi kinachotushangaza hapa ni raia wa kigeni kuendesha uhalifu ndani ya nchi yetu na kujigamba kuwa atarudi tena kwani Tanzania ni kama “choo” unachoweza kuingia na kutoka kama utakavyo.
Kauli hii inaonesha wazi udhaifu mkubwa walionao viongozi na watendaji wa Taifa hili waliochoka kiakili, na kukosa uzalendo na nchi hii, walichoamua ni kutanguliza rushwa kwanza na uongozi wa mazoea.
Kitendo hiki hakikubaliki kamwe, ni dharau kubwa kwa Watanzania. Sasa viongozi na watendaji hawa 'wachovu' wameweka bayana kwamba Tanzania ni shamba la bibi ambalo unaweza kuvunja sheria yoyote bila kuhojiwa na pengine utaungwa mkono na viongozi wengi wa Serikali.
Tunasema kama viongozi wetu wangekuwa wazalendo wa kweli kama alivyokuwa Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere, uhuni huu usingepata nafasi kamwe. Viongozi hawa wa sasa wako kwa ajili ya maslahi yao binafsi na siyo ya Taifa.
Kwa hili tunasema Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, ni lazima awajibike kutokana na kitendo hiki cha raia wa kigeni kuvunja sheria ndani ya nchi yetu kwa kuifananisha na choo ambacho unaingia na kufanya lolote utakalo bila kuhojiwa na mtu.
Kama Chikawe ni muungwana na mpenda nchi anapaswa kuwachukulia hatua mara moja maofisa wa Uhamiaji, walafi wa rushwa wanaowakaribisha wageni haramu ndani ya nchi yetu, vinginevyo ajiuzulu nafasi hiyo ya uwaziri ili apewe kiongozi mwingine mzalendo asiyependa ubabaishaji.
Rushwa ndiyo iliyotufikisha hapa Watanzania hadi kudharauliwa na wageni na wahalifu kama Ahmed, kutoka mataifa mengine huku Watanzania waishio nje ya nchi wengi wao wanaishia kunyanyaswa na wenyeji wao.
Hapa hatusemi kwamba Watanzania waishio nje ya nchi wajiingize katika maovu kama haya na mengine, bali waishi kwa haki na kuheshimu sheria zilizowekwa katika mataifa hayo.
Vile vile tunaitaka Idara ya Uhamiaji nchini kutofanya kazi zake kwa ubabaishaji na kutuletea aibu kama hii ya kumrudisha tena nchini, mtuhumiwa wa biashara haramu ya kuuza na kusafirisha binadamu kwa sababu za rushwa iliyokithiri ndani idara hiyo.
Wananchi tunapaswa kuitetea nchi yetu, na kulinda heshima na utu wetu bila kuwafumbia macho watu wachache walioamua kuihujumu nchi kwa kuendekeza vitendo vya rushwa na kuwakumbatia wageni wanaothubutu hata kutuporomoshea matusi Watanzania. Chikawe chukua hatua kwa wahusika ama uwajibike mwenyewe kutokana na kashfa hii.