Wanasiasa siyo wenzetu kwa maana nyingi tu, na siyo kwa sababu tu ya kuitwa waheshimiwa.

Kwanza, ni watu wenye kujiamini, wenye imani inayoambatana na uwezo mkubwa wa kusikia maoni tofauti kabisa na ya kwao, lakini wakaendelea kushikilia msimamo kuwa wanachofanya ni sahihi, na kuamini kuwa malengo yao ndiyo muhimu zaidi.

Utampambanua mwanasiasa kwa ubishi. Ubishi si jambo baya kama kusudio ni kuleta matokeo mazuri na yenye manufaa kwa jamii, ingawa upo pia ubishi wenye kusudio la kujinufaisha binafsi. Ubishi ni mojawapo ya sifa za msingi kabisa za mwanasiasa.

Zipo aina mbili za ubishi. Ubishi wa kutetea kwa kila hali mawazo na mipango anayoisimamia yeye, na ubishi dhidi ya mawazo na mipango ya wadau wengine wa siasa.

Huu wa aina ya pili ndiyo tunaouona kwenye mfumo wa vyama vingi vya siasa ingawa wakati mwingine unadhihirisha tu kwamba ni ubishi ambao hauna msingi kabisa na ambao hauleti manufaa yoyote kwa jamii.

Ipo sifa nyingine naiita usugu, uwezo mkubwa wa kusikia kila aina ya habari mbaya dhidi yake, mipango yake na maoni yake, lakini akiendelea kuwa na uwezo mkubwa wa kusonga mbele kama vile kazibwa masikio na kafunikwa macho.

Nimewahi kusikia simulizi ya mwanasiasa akielezea jinsi wapinzani wenzake kwenye kipindi cha kampeni za udiwani walivyopandikiza watu kwenye mikutano ya hadhara kwa kumuuliza maswali yaliyoanika na kumuacha na uwazi mithili ya kumvua nguo zote. Cha ajabu, njama ambayo ingemfanya binadamu mwingine wa kawaida kutafakari kusaga chupa na kusitisha uhai, yeye alizihadithia huku akicheka kuwa ni jambo la kawaida tu: ajali ndogo kazini.

Kwa kawaida binadamu tunashikilia misimamo mbalimbali juu ya masuala kadhaa ndani ya jamii: ya kisiasa, kiutamaduni, dini, na kadhalika na hatujali sana kuweka wazi misimamo hiyo. Tofauti na ilivyo kawaida, mwanasiasa yupo kwenye kundi la binadamu wanaojaribu kufurahisha watu wa misimamo tofauti, na hata wale wenye misimamo inayogangana.

Hata kwa wale wanasiasa wanaosema na kuonekana kuamini kuwa haiwezekani kuridhisha kila mtu, bado hulazimika kujaribu kuridhisha makundi kadhaa ndani ya jamii; suala ambalo linakinzana na hulka ya binadamu.

Mmarekani William Clay alielezea siasa kama mchezo ambao hauna maadui wa kudumu, na hauna marafiki wa kudumu, bali maslahi ya kudumu.

Ni dhana inayotoa maana kadhaa, mojawapo ikiwa kwamba watu hawatumbukii kwenye siasa ili kutafuta marafiki au kujenga uadui; watu wanadumu kwenye siasa kwa sababu ya kupima maslahi ya kisiasa wanayoyafuata kwa wakati husika, na kuyaoanisha na maslahi ya siasa yanayofanana na hayo.

Suala moja ambalo halitamkwi kwenye msimamo wa Clay ni kuwapo uwezekano kuwa hata maslahi nayo si suala la kudumu; maslahi yanaweza kubadilika. Hii ni sifa ya baadhi ya wanasiasa: hachelewi kuchupa baharini na kuachana na jahazi ambalo halibebi maslahi yake.

Jambo moja linaloweza kuleta tofauti hii ni kugongana kwa maslahi mapana na maslahi binafsi. Yapo maslahi ya kisiasa ambayo yanaweza kuwa lengo la kundi kubwa la wadau na suala ambalo lipo wazi kwa kila mmoja, lakini kuna maslahi binafsi ambayo hayako wazi na yanaweza kuwa yanafahamika na mwanasiasa peke yake au na kundi dogo la watu.

Unaposikia mwanasiasa kushutumiwa kuwa amesaliti wenzake bila shaka kilichotokea ni kugongana kwa kile yeye anachoona kuwa ni maslahi anayopaswa kuyalinda kwa wakati huo na kile ambacho wenzake wanaona ni maslahi muhimu kwao.

Na inapotokea hivi huu unakuwa mfano mwingine unaompambanua mwanasiasa na wanajamii wengine; mtu ambaye hakoswi usingizi inapotokea kufikia uamuzi wa kubadilisha mwelekeo wa maslahi yake ya kisiasa au maslahi binafsi, na kuachana na kundi ambalo ameambatana nalo kwa muda mrefu.

Haitakuwa sahihi kusema kuwa mwanasiasa wa aina hii ni mwanasiasa ambaye hafai, mtu ambaye hastahili hata kutupwa kwenye jalala. Tunaweza kusema hafai kama tunapata sababu zote zilizomshawishi kubadilisha muelekeo. Sana sana tukubali tu kuwa wapo watu nje ya ulingo wa siasa watakaosema kuwa ni mtu ambaye haeleweki. La uhakika ni kusema kuwa siasa ina wenyewe.

Ni mchezo ambao una kanuni na sheria zake zaidi ya zile zinazopitishwa bungeni; mchezo ambao unahitaji mashabiki, lakini mashabiki ambao hawana udhibiti wa uhakika juu ya wachezaji wa timu yao; mchezo ambao mechi yake haiishi; mchezo ambao mshambuliaji wa huku atahamia kule wakati mechi ikiendelea na ataanza kushambulia goli alilokuwa akilinda mwanzoni.

Siasa ni mchezo usiotabirika ambao kila siku unatuletea matukio ambayo, kwa wengi walio nje ya siasa, ni tanuli la maswali mengi bila majibu ya kutosha.

480 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!