Majivuno yaliwabadili malaika wakawa mashetani. Unyenyekevu huwafanya watu wawe kama malaika – Mt. Augustino.

Kitendawili: Tega! ‘Ananifanya nichukiwe na kila mtu’. Jibu ni ‘majivuno’. Kitendawili: Tega! ‘Nikimmeza najisikia sana’. Jibu ni ‘majivuno’. Majivuno ni jeraha lisiloponyeka katika maisha. Majivuno ni jeraha linalonuka kama mzoga wa porini. Ni donda ndugu. Majivuno ni dereva wa shetani. Mwaka 2013, Jarida la ‘New People’ la nchini Kenya lilichapisha makala yangu iliyokuwa inaitwa, ‘Holy Family’. Padri Erickson Wangai wa Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi alibahatika kusoma makala ya ‘Holy Family’. Padri Erickson baada ya kuisoma makala ile, alinitumia ujumbe mfupi kwa njia ya barua pepe. Katika ujumbe huo aliandika hivi: “Binadamu hawezi kuishi bila upendo, lakini anaweza kuishi bila majivuno.’’

Katika makala hii nitapata fursa ya kutafakari umuhimu wa kuishi maisha ya upendo, na hasara ya kuishi maisha ya majivuno. Ninakualika wewe uliyepata fursa ya kusoma makala hii tusafiri pamoja katika hali ya ukimya na tafakuri mwanana. Mwanateolojia wa Kanisa Katoliki, Mt. Augustino wa Hippo anasema: “Majivuno yaliwabadili malaika wakawa mashetani. Unyenyekevu huwafanya watu wawe kama malaika.”

Swali ambalo unaweza kuniuliza ni hili: “Nifanye nini ili niweze kuishi maisha yanayoongozwa na unyenyekevu na si majivuno?” Usiwe na shaka, jibu linapatikana. Tunasoma hivi katika maandiko matakatifu: “Kila ajikwezaye atashushwa, na kila ajishushaye atakwezwa.’’ [Lk. 14:11].

Ukijishusha utainuliwa, ukijikweza utashushwa. Kwa upande mwingine mwanateolojia Augustino wa Hippo anatoa ushauri huu: “Mungu ni mwenye uwezo wa juu sana, jinyenyekeze atakushukia, lakini ukijitukuza atakukimbia.” Njia bora na salama ya kuishi maisha ya unyenyekevu ni kupiga magoti mbele ya msalaba wa Kristu ili tujifunze unyenyekevu kutoka kwake.

Yesu Kristo yeye ambaye alishuka duniani na kumkomboa mwanadamu kwa gharama ya mateso alikuwa mtii na mnyenyekevu. Tunasoma hivi kutoka katika maandiko matakatifu: “Tena alipoonekana ana umbo kama la mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii, naam, mauti ya msalaba.” [Fil. 2:8].

Dhambi kubwa sana ambayo iliwahi kutokea huko mbinguni na ambayo inatendeka hapa duniani ni ‘majivuno’. Majivuno yaliwabadilisha malaika  wakawa mashetani. Majivuno yalimwondoa malaika Lucifer mbinguni. Lucifer kabla  hajaondolewa mbinguni kwa sababu ya majivuno yake alikuwa malaika mkuu. Muulize kilichomtokea baada ya kuwa amekumbatia majivuno. Sababu ya shetani kuondolewa kutoka mbinguni ilikuwa hii: “…alitaka kuwa kama Mungu.” Nabii Isaya amendika hivi: “Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa ewe uliyewaangusha mataifa. Nawe ulisema moyoni, ‘Nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu. Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana na yeye aliye juu.’” [Isaya 14:12-14].

Kuna wakati shetani alikuwa malaika wa Mungu. Mungu akikupa umaarufu, usiutumie huo umaarufu vibaya. Shetani kabla hajaondolewa mbinguni alikuwa malaika mkuu. Ni kwamba yeye ndiye aliyekuwa waziri mkuu katika serikali ya Mungu. Akalewa madaraka ya uwaziri mkuu. Akajiona anaweza kuiongoza dunia na mbingu. Akatamani kuabudiwa kama Mungu Mwenyezi anavyoabudiwa. Akajiona anaweza kuumba. Akajawa kiburi na majivuno. Mwenyezi Mungu akachukizwa na nyendo za shetani, akamuondoa kutoka kwenye ufalme wake wa milele.

Mwandishi R. Newton anaandika: “Ngoja nikupe historia ya majivuno  katika sura fupi tatu. Mwanzo wa majivuno ulikuwa mbinguni. Mwendelezo wa majivuno ni duniani. Mwisho wa majivuno ni motoni. Historia  hii inaonyesha majivuno ambavyo yanaleta karaha.” Tuyakimbie majivuno. Tuyakatae majivuno. Tuupende unyenyekevu. Tuukumbatie unyenyekevu.

Majivuno yanakutoa sehemu nzuri na kukupeleka sehemu mbaya. Majivuno yanakutoa kwenye sura ya utakatifu na kukuvalisha sura ya ushetani. Majivuno hujenga ukuta kati ya watu, unyenyekevu hujenga daraja. Unyenyekevu ni mafuta  yanayolainisha na kuvuta uhusiano. Padri Dk. Faustine Kamugisha anasema: “Majivuno si ushindi hata kidogo.” Kanuni ya kwanza ya utakatifu ni unyenyekevu. Ya pili ni unyenyekevu. Ya tatu ni unyenyekevu. Na kanuni ya kwanza ya kushindwa ni majivuno. Ya pili ni majivuno. Ya tatu ni majivuno.

Please follow and like us:
Pin Share