Kataa kujikataa

Kukataa kujikataa ni mtihani. Kujikataa ni kujihisi wewe si mtu muhimu. Ukweli wewe ni mtu muhimu. “Kukosa kitu cha kukufanya ujisikie wewe ni mtu muhimu ni jambo liletalo huzuni mkubwa sana, ambalo mtu anaweza kuwa nalo,” alisema Arthur E. Morgan.

Kumbuka wewe si bahati mbaya. Wewe ni wewe. Hakuna ‘spea’ kwa ajili yako. Uliletwa duniani kwa lengo maalumu. Lazima ukatae kujikataa. Kwepa aina zote za kujikataa. Watu wengi wanajikataa bila kujua kama wanachokifanya ni kujikataa. Sababu mojawapo ya watu kuziba njiani kwenye mitaa ikabaki njia ya waendao kwa miguu na magari hayawezi kupita ni kujikataa. Mtu anakataa uwezekano wa siku moja kumiliki gari au watoto wake kumiliki gari. Kataa kujikataa. Wasikuite “kidomo,” ukalegeza midomo. Kujikataa ni kujiangusha.

“Mtego mkubwa sana katika maisha yetu si mafanikio, umaarufu au mamlaka, bali kujikataa,” alisema Henri Nouwen. Katika mtazamo huo baba huyo alifafanua: “Mtu anaponishtaki au kunisema vibaya tu, wakati ninapokataliwa tu, nakubaki peke yangu au kuachwa, najikuta nafikiria, ‘Huo ni uthibitisho tena kuwa mimi si chochote.’ Upande wangu hasi unasema, mimi si mwema…nastahili kusukumwa pembeni, kusahauliwa, kukataliwa na kuachwa.” Kujikataa ni adui mkubwa wa mafanikio na maendeleo ya mtu. Kama kuna kasoro au ‘kivuli’ cha kurekebisha kirekebishe, lakini usijikatae.

Kutokuwa na mipango mikubwa ni kujikataa. Umeumbwa kufanya makubwa. Kutojistahi ni kujikataa. Kutojipenda ni kujikataa. Kutojiheshimu ni kujikataa. Kutojiamini ni kujikataa. Kutojiwazia mazuri ni kujikataa. Kutojitakia mema ni kujikataa. Kuishi na chuki ni kujikataa. Kutojihurumia ni kujikataa. Kutojipenda ni kujikataa. “Kama mtu hajipendi, usimwambie akupende (Methali ya Manprussi). Kujikataa ni kutojiheshimu. Kinyonga anasema watu wengine wanakuheshimu kwa sababu unajiheshimu, ndiyo maana kinyonga anatembea kama mfalme. Kujikataa ni kujiona hufai. Kujikataa ni kuwa adui wa nafsi yako. Ukweli huu unabainishwa na methali hii: “Adui wa mtu ni mtu.”

Mwaka 1830 George Wilson alihukumiwa kunyongwa kwa sababu ya mauaji huko Philadelphia. Rais Andrew Jackson alimsamehe lakini askari magereza alipompa karatasi ya msamaha, Wilson alikataa msamaha. Suala hili lilipelekwa Mahakama ya Juu. Jaji Mkuu Marshall alitoa uamuzi huu: “Msamaha ni karatasi, thamani yake inategemea kupokelewa kwa msamaha kwa mhusika. Ni vigumu kufikiria kuwa mtu aliyehukumiwa kunyongwa atakataa msamaha, kama msamaha haupokelewi, si msamaha. George Wilson lazima anyongwe.” Alinyongwa kweli. George Wilson hakukataa kujikataa. Kwa ufupi alijikataa.

Kujilaumu ni aina ya kujikataa. “Lazima ukwepe si tu kuwalaumu wengine bali na wewe kujilaumu. Una mwelekeo wa kujilaumu kwa magumu unayokutana nayo katika masuala ya uhusiano. Lakini kujilaumu si aina ya unyenyekevu. Ni aina ya kujikataa ambapo unadharau au kukataa wema na uzuri wako,” alisema Henri Nouwen.

Mambo mabaya yote yanayotokea duniani hukuyasababisha wewe, acha kujilaumu. Mtu mmoja au wawili wasipokukubali, jua kuna maelfu ya watu wanaokukubali. Kataa kujikataa. Binadamu si pesa inayopendwa na watu wengi. Kutojithamini ni kujikataa. “Mtu ambaye hajithamini hawezi kuthamini chochote au yeyote,” alisema Ayn Rand.

Jikubali, jithamini, jipende, jiheshimu, jiamini, jisamehe na jitakie mema. Usikubali sumu na uongo wa kwamba huwezi kufanya la maana ikuingie akilini mwako. Baba anapokimbia majukumu ya kuwa baba anajikataa. Mama anapokimbia majukumu ya kuwa mama anajikataa. Kutofanya kazi (isipokuwa kama unaumwa) ni kujikaa, binadamu ni mtu wa kufanya kazi. Usipowasiliana na watu wengine ni kujikataa. Kiota kilivyo kwa ndege ndivyo mahusiano yalivyo kwa binadamu.

Please follow and like us:
Pin Share