Shabiki na shabaki ni kama watoto wawili pacha. Ukikutana na shabiki utawaza umekutana na shabaki, na ukikutana na shabaki utaona umekutana na shabiki. Kumbe sivyo. Ni watu wawili wenye hulka na tabia tofauti. Wa kwanza ni mkweli na wa pili ni mwongo.

Ushabiki ni hulka ya mtu kupenda sana kitu fulani. Ushabaki ni tabia ya kupenda fujo, ugomvi au mzozo. Tabia mbili hizi zinawachanganya watu wanaopenda kushabikiwa, na wanaotaka kushabikia jambo fulani. Hiki ni kitendawili ambacho bado kuteguliwa na watu wenyewe katika shughuli zao za kutafuta sifa, heshima na madaraka.

Kupenda ni uamuzi wa mtu kufanya jambo kwa hiari baada ya kuridhika nalo. Unapopenda kupita kiasi ndipo inapojitokeza tabia ya ushabiki au ushabaki. Ni busara kutambua na kuzingatia maana ya kupenda, kabla ya kutumbukia katika tabia fulani.

Shabiki ni mkweli na muwazi katika kauli na matendo. Anatoa kasoro anapoona mambo hayako sawa na anasifia mambo yanapokuwa shahiri. Anakuwa muwazi katika kutetea na kusimamia haki inapatikana na inatendeka bila hiyana. Huyu ndiye mshabiki nimjuae na kumjali. Laiti watu wangemtabua, wasingelumbana hadi kupimana vifua vyao.

Shabaki ni mnafiki, mzushi, mdanganyifu na mgombanishi. Anapenda kuona watu hawaelewani, hawana amani na mioyo yao kujaa wasiwasi. Ana hila nyingi za kuunda mipango hasi na mwepesi kutetea mipango yake inapobainika ili aonekane yeye si mkosefu, aonewe huruma. Huyu ndiye shabaki, si mpendi, ni mtu hatari sana.

Shabiki na shabaki wanapatikana katika makundi mbalimbali: katika maeneo yetu ya makazi, kazi, siasa, michezo, starehe na burudani. Watu hawa wana maneno matamu na mvuto kwa watu. Mjenzi wa makundi ni shabiki na mbomoaji wa makundi ni shabaki. Watanzania tuwe makini tunapoamua kuwatumia watu hawa.

Mtu kumshabikia kiongozi wa siasa anayeshawishi na kuhamasisha wanachama kutetea, kutekeleza na kusimamia itikadi na malengo ya chama chake kwa nia ya kuleta maendeleo yao, ni jambo jema na sahihi. Ukweli kupitia mtu kama huyu, chama chochote kinafahamika, kinavuma na kinapata wanachama ambao ndiyo mtaji wa chama.

Kadhalika, kumshabikia kiongozi wa serikali anayetekeleza sera, mipango, sheria na ahadi za serikali kwa ajili ya raia na wananchi kupata maendeleo ya kiuchumi na kijamii si kosa. Ni sahihi na ni wajibu. Si busara hata chembe kumbughudhi mtu kama huyu, kwani anastahili heko, kwa sababu serikali inapata sifa ya kupendwa na kukubalika na watu.

Mtu anayejifanya ni shabiki kumbe ni shabaki ni hatari sana. Shabaki katika tabia yake anafanya usaliti, uchochezi na wakati mwingine anafanya uasi kwa chama chake, serikali au wananchi wenzake. Maendeleo kwake ni ugomvi na mzozo. Si maendeleo ya watu na vitu.

Hapa Tanzania mashabiki wameshiriki katika harakati za kudai uhuru wa nchi yetu na bado wamo katika kukabiliana na changamoto za maradhi, ufukara, ujinga na kutunza uhuru wetu. Ukweli watu wenye tabia ya ushabiki wanajenga umoja na mshikamano wa nchi na kusaidia viongozi kueleweka vema kwa wananchi.

Lakini katika harakati hizo na mapambano hayo, mashabaki (mashabuka) kwa miongo mitano na ushei sasa, tangu tupate uhuru wetu wanafanya jitihada kuharibu mifumo faafu ya uchumi na huduma za jamii kwa kuanzisha fujo, ugomvi na mzozo katika serikali, taasisi za dini na kwenye vyama vya siasa.

Watanzania tuwe waangalifu tunapochagua na kukaribisha wapenzi, marafiki na viongozi katika shughuli zetu mbalimbali za kibinadamu na kijamii ili kukwepa ushabaki unaofanywa na watu wanaovaa ngozi ya kondoo ilhali ni mbwamwitu. Naomba kukukumbusha, taifa lolote linajengwa kwa maelewano, makubaliano, uhuru, sheria na utamaduni wa wazalendo. Tafakari.

Please follow and like us:
Pin Share