Salamu zangu ni za kawaida kwa sababu kwanza naamini katika upendo; pili, naamini katika undugu; Watanzania wote ni kitu kimoja na ni ndugu, tunapaswa kupendana sana.

Upendo tutakaokuwa nao ndio utakaotufanya tuwe na mshikamano na hatimaye tutavuka hili tuta kubwa na lenye majaribu makubwa ya kufikia malengo ya maendeleo.

Huwa nakufuatilia sana, hasa pale unapoonyesha katika uso wako kwamba kuna jambo limekukera au linakukera, unaonyesha kwamba kweli unakerwa na wakati mwingine unachukua hatua papo hapo bila kusubiri vijisababu vya kujitetea kwa baadhi ya watu.

Kimsingi sura hizo zinavaliwa na watu wachache sana ambao umewapa dhamana ya kukusaidia katika kazi zako, lakini lazima nikiri wazi kwamba wapo wasaidizi ambao bado unaona hawajakidhi viwango ambavyo ungelipenda wavifikie.

Leo nimeona ni vema nikajaribu kukukumbusha, na nina sababu ya kukukumbusha, kwa kuwa najua mambo mengi uliyonayo, tena si mengi tu, bali makubwa, kwa maana ya mustakabali wa taifa.

Unaweza ukawa unakumbuka makubwa lakini kuna madogo yanayopita chinichini, ni lazima watu wa karibu wayamalize hata kabla hayajafika kwako.

Wasaidizi wako wengi nao wamekuwa na mambo mengi, tena yale ya kati na madogo, lakini baadhi yao wamezidiwa na ndipo ninapoelewa somo la vita ya kiuchumi kuwa gumu kuliko ile ya AK-47. Nahisi mwelekeo wa uongozi wako unaweza ukaeleweka machweo, kwa namna ambavyo imekuwa vigumu kwa kada ya chini kabisa ya uongozi wanavyochukulia mambo kwa urahisi rahisi.

Siku za hivi karibuni umesikika ukisema wazi kabisa kwamba kuna mambo ambayo yalipaswa yafanywe na baadhi ya wateule wako lakini wapo kimya na wanayaangalia huku wananchi wako wakiwa na maswali mengi bila majibu. Nilielewa lakini kwa kuwa niko chini huku, pia bado naelewa tatizo kubwa la urasimu na utekelezaji kiasi cha kutaka kuwatoa kafara viongozi wao wa kati ama juu, hii ni vita kubwa sana.

Siku utakayowaalika wazee tunywe kahawa hata pale Mnazi Mmoja tutasema mengi, lakini hayatakuwa katika mpangilio kwa sababu kuna mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine yamevuruga utaratibu wa ubongo wetu na kuonekana kama tuna matatizo ya uzee na akili.

Kuna matatizo yaliyosheheni katika mfumo wetu wa ajira zetu za zamani kiasi cha kutufanya tukose haki mbalimbali za kiutumishi, wapo uliowapa dhamana lakini wanadundisha mafaili huku na kule kama mpira wa kona wakisubiri uje wewe utoe kauli juu ya hatima hiyo.

Wapo vijana katika ajira mpya ambazo wamezipata lakini wanayumbishwa kila siku kama vile nchi hii haina sheria, na kwamba labda jambo liwe kubwa na ulitolee uamuzi wewe, hii ndiyo Tanzania yetu. Wapo viongozi wenye uthubutu wa kukusaidia lakini nikiri wazi sioni kwanini uendelee kupokea matatizo ya wananchi kama unao wasaidizi ambao kimsingi walipaswa kuchukua hatua.

Nchi yetu imebarikiwa sana na kwa kweli ni tunu pekee ambayo tunapaswa kumshukuru Mungu kila siku, lakini kuna watu wachache ambao wanaharibu taswira na tunu hii kwa matakwa yao. Najua unatambua lakini hauna uwezo wa kompyuta kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

Ninaelewa unajua kuwa una maadui kutokana na baadhi ya hatua ulizozichukua, hapa ndipo ninapodhani kwamba labda baadhi ya wasaidizi wako wanataka uwe mbeba lawama na dhana ya uongozi wa kuchukua hatua wanajivua kwa visingizio kadhaa.

Mheshimiwa Rais, umekuwa ukimaanisha kwamba wewe ni kiongozi wa wanyonge, leo nataka nikwambie kwamba wanyonge wengine bado wananyongwa sana. Wanyonge hawa ni waajiriwa wenye vyeo vidogo na watumishi wa kada za chini mahali pao pa kazi, wafanyabiashara wadogo, wakulima wa mazao mbalimbali nchini na wastaafu wa zamani na wapya.

Una kazi kubwa ya kuwafikia kama hauna wasaidizi watakaoamua kuwa wazalendo wa kweli, na ndiyo maana tunaona wengine wakitumbuliwa na wengine kufikishwa mahakamani, huo ni msalaba wako wa kuwatumikia Watanzania, wengine hawataki kuubeba.

Kuna kitu nataka kusema, lakini sitasema, nami ni miongoni mwa wasema ukweli, nisije nikasema nikavuka mipaka nikawakwaza wengine na kuchuma dhambi, siku zangu si nyingi sana na pepo naipenda kuiona. Siku nikipata nafasi nitaandika yanayonikera kwa baadhi ya wasaidizi wako.

Mungu ibariki Tanzania.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.

779 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!