Wanawake wajasiriamali kunolewa Dar

Kongamano kubwa litakalowawezesha wanawake kuunda mtandao wa wajasiriamali kutoka maeneo yote nchini litafanyika mapema mwezi ujao.

Waandaaji wa kongamano hilo, Open Kitchen chini ya asasi ya Amka Twende, wameeleza kuwa zaidi ya wajasiriamali 300 wanawake kutoka vikundi mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo litakalofanyika Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Open Kitchen, Upendo Mwalongo, amesema mafunzo ya ujasiriamali yatatolewa wakati wa kongamano hilo ili kuwawezesha wanawake kuwa na ujuzi wa shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato.

“Kongamano limelenga zaidi kuamsha ari ya wanawake nchini kupenda kujishughulisha na ujasiriamali ili kujiongezea vipato vya familia zao badala ya kutegemea chanzo kimoja tu,” amesema.

Mwalongo ameongeza kuwa kupitia kongamano hilo wamelenga pia kujenga mtandao mkubwa wa wanawake wajasiriamali kutoka maeneo yote nchini kwa lengo la kuchochea chachu ya wanawake kujifunza zaidi vitu vingine kupitia wajasiriamali wenzao.

“Unajua mkiwa pamoja kila mmoja atakuja na uzoefu tofauti na mwingine, kwa namna hiyo watu wanajifunza mambo mengi kupitia kwa wenzao,” ameongeza Mwalongo.

Huu ni mwaka wa pili kwa kongamano hilo kufanyika na mwaka huu litawashirikisha wanawake wajasiriamali kutoka vikundi vya wanawake wenye VVU kutoka Wilaya ya Temeke kama njia ya kuwahamasisha kupenda kujitafutia kipato kwa njia ya ujasiriamali.

“Tunafahamu kuwa tukishawapatia mafunzo ya ujasiriamali, mambo mengine kama vile kutafuta masoko ya bidhaa zao wanaweza kuyafanya kwa urahisi. Hilo litakuwa rahisi kwa sababu kati ya mafunzo tutakayotoa ni utafutaji wa masoko,” alibainisha.

Mwalongo alibainisha kuwa iwapo wanawake wajasiriamli watajiunga katika mtandao na kufanya biashara kwa kushirikiana itakuwa rahisi kwao kuwapata wafadhili wa kuwawezesha kupata mafunzo zaidi kama vile kutoka SIDO ili waongeze ujuzi katika shughuli zao.

Alibainisha kuwa kongamano la mwaka huu litakuwa na upekee wa aina fulani kwani litawahusisha pia wanaume.