Waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza viatu cha Bora ambao waliachishwa kazi mwaka 1991, wameibuka na madai ya kiasi cha Sh bilioni 45. 

Wafanyakazi hao wanaitaka serikali iwalipe kiasi hicho cha fedha ambacho kinajumuisha pia malipo ya muda wa kusubiria kupewa haki zao.

Zaidi ya wafanyakazi 100 ambao waliachishwa kazi Bora kwa mujibu wa sheria walimlalamikia mwanasheria kwa kutowapatia haki zao kwa wakati na kusababisha malipo yao kuwa na malimbikizo makubwa kiasi hicho.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Pensius Luvumbi, amesema kuwa yeye aliajiriwa na Kiwanda cha Bora mwaka 1977 katika idara ya manunuzi.

Amesema ilipofika mwaka 1991 kiwanda kililazimika kupunguza wafanyakazi 1,000, kutokana na kuyumba kwa uzalishaji kulikotokana na kupungua kwa malighafi.

Luvumbi amesema wafanyakazi waliopunguzwa wakaanza kusubiri malipo yao kutoka kwa kampuni kama vile nauli za kuwarudisha vijijini kwao na gharama za usafirishaji wa mizigo yao, malipo ya awali ya PPF na fedha za usumbufu.

“Lakini tulikaa miezi 40 bila kulipwa. Baada ya hapo kampuni ikaamua kutupatia kiasi kidogo cha fedha kama malipo ya awali. Hakikufika hata laki moja. Tunaambiwa kuwa baada ya malipo hayo na akaunti iliyokuwa inatumika ikafungwa kabisa,” amesimulia Luvumbi.

Ameongeza kuwa baadhi yao waliamua kwenda Mahakama ya Kisutu kufungua kesi huku kundi jingine na yeye akiwemo wakiamua kwenda kwa waziri mkuu wa kipindi hicho kumfikishia suala hilo.

“Baada ya kusikia kilio chetu waziri mkuu alitupatia nyongeza ya fedha kama malipo ya nauli zetu na mizigo kutoka makao makuu ya wilaya hadi vijijini. Fedha hizo zilitoka kwenye mfuko wa ofisi yake,” amesema.

Amesema hata hivyo hawakufurahishwa na hilo, wakaamua kuungana na wenzao waliofungua kesi Mahakama ya Kisutu ambako kesi yao ilitupiliwa mbali na wakakata rufani hadi Mahakama Kuu ambako kesi hiyo ilitupwa tena.

Hata hivyo hawakukata tamaa, kwani walikata rufani katika Mahakama ya Rufani, chini ya jopo la majaji Agustino Ramadhani, Lewis Makame na Joseph Kisanga walioamua kuwa walipwe stahiki zao lakini tangu hukumu hiyo itolewe hawajalipwa. 

Amesema baada ya kupita muda mrefu, mwanasheria wao aliamua kulifufua suala hilo kwa kulipeleka kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro (CMA) ambako walitaka kulipwa posho ya kujikimu ya Sh 4,560 kwa siku, kwa miaka yote tangu mwaka 1991 walipoachishwa kazi hadi uamuzi utakapotolewa, malipo ya kiinua mgongo, fidia ya asilimia 31 ya gharama zitokanazo na pingamizi na gharama nyingine ambazo CMA ingeona zinafaa kulipwa.

Mfanyakazi mwingine, Omari Nyaru, amesema hivi sasa wanaishi maisha magumu kana kwamba hawakuwahi kulitumikia taifa.

Amesema kimsingi serikali ilipaswa iwajali wao kama inavyowajali wastaafu wengine.

“Tunahangaika kudai haki yetu, limekuwa ni tatizo kubwa kwa sababu hivi sasa hatuna uwezo wa kumweka wakili kwa ajili ya kutuwakilisha kwenye mambo haya,” anabainisha.

Akilizungumzia suala hilo kwa niaba ya mkurugenzi mkuu wa Kiwanda cha Bora, Mkuu wa Idara ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi, Sylivery Buyaga, amesema kuwa Kiwanda cha Bora hakihusiki na mafao hayo.

Buyaga amesema kuwa kiwanda hicho kilinunuliwa na wawekezaji waliopo mwaka 1994 baada ya serikali kushindwa kukiendesha na suala la wafanyakazi wa zamani halikuwa miongoni mwa makubaliano.

Ofisa Habari kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuli, amesema wamekwisha kupata taarifa za madai ya wazee hao na wanayafuatilia.

1065 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!